Tollywood movies sasa inakuna na roho sita...ni mapinduzi mengine kunako game ya filamu Bongo
Kampuni mama ya kutayarisha, kudurufu na kusambaza sinema Tanzania inayokwenda kwa jina la Tollywood Movies, sasa imechukua dhamana ya kusambaza movie mpya ya kutisha iitwayo Roho Sita, Joseph Shaluwa anashuka nayo.
Roho Sita ambayo imetayarishwa na Koga Film chini ya Mkurugenzi wake Thomas Simon, itakuwa sinema ya kwanza ya kutisha ambayo matukio mengi yanaonekana halisi tofauti na nyingine zilizotangulia.
Mkurugenzi wa Filamu za Tollywood Movies, Hamie Rajab, aliliambia Ijumaa kwamba, katika sinema zote za kutisha za Tanzania, hakuna iliyowahi kuifikia ubora wa Roho Sita.
“Mpaka Tollywood tumeamua kuichukua basi mashabiki waamini kwamba kitu kimetulia, ni sinema ya kwanza ya kutisha ambayo kila kitu kinaonekana halisi, kubwa zaidi ni kwamba program iliyotumika katika uhariri ni ya kisasa duniani, ndiyo maana imeifanya kuwa bora na yenye kiwango cha Kimataifa. Wadau wasubiri kidogo, siku si nyingi ngoma itaingia mtaani,” alisema.
Baadhi ya wakali walioonyesha uwezo wao katika kitu hicho ni pamoja na Ndumbangwe Misayo, Charles Magali, Juma Kankaa, Chuchu Hans na Evans Komu ambao wameigiza katika kiwango cha hali ya juu huku uhusika ikiwa ni kitu cha kwanza.
******* ************************
KR :Leo tunarudi kulekule kwetuKutoka ndani ya kundi la TMK Wanaume Family, msanii Rashidi Ziara a.k.a KR amesema na ShowBiz kwamba, leo Ijumaa wanaanza ziara ya kupiga shoo katika vitongoji kadhaa vya Dar es Salaam maarufu kama Uswahilini ambako anakutaja kama nyumbani kwao kwakuwa wasanii karibu wote wa kundi lake wamekulia pande hizo.
Msanii huyo alisema kuwa wanayo kila sababu ya kujivunia uswahili kwakuwa wanaamini mashabiki wao wengi wapo huko, ndiyo sababu inayowafanya waanzie ziara yao ya kutoa shukrani na kuwaaga mashabiki wao huko kabla ya kuendelea na safari katika mikoa mingine.
“Ziara hiyo ambayo tumeipa jina la ‘Kitaa hadi kitaa’ itaanzia pande za Yombo Buza, ndani ya Ukumbi wa Ghadafi, kesho Jumamosi tutaelekea Chanika kwa shoo itakayofanyika ndani ya Ukumbi wa GFC Motel,” alisema alisema KR.
********
Dar es Salaam Hands up Ni Kinondoni au Temeke?
Kutoka ndani ya mpambano huu, wa kijanja, Dar es Salaam Hands Up (Dar es Salaam Mikono Juu) ambao unazishirikisha wilaya tatu za mkoa wa Dar es Salaam, baadhi ya wasomaji na wapenzi wa burudani Bongo wameomba shindano lisogezwe mbele ili wapate nafasi ya kutuma kura zao kwa umakini zaidi.
Sisi kama waandaaji tumelipokea ombi hilo kwa mikono miwili na kwamba tutatoa wiki moja tu ya zoezi hilo kabla ya kuitangza wilaya ambayo itaibuka na ushindi kati ya Kinondoni na Temeke ambazo zilifanikiwa kuingia fainali baada ya Ilala kutolewa siku kadhaa zilizopita.
Tunawaomba muendelee kutuma kura zenu mkituambia ni wilaya ipi kati ya Kinondini na Temeke ina wasanii wakali wa muziki wa kizazi kipya kwa kuandika ujumbe mfupi na kututumia kupitia simu namba 0787-110. Mpambano huu ambao umetokea kuwavutia wapenzi wengi wa burudani karibu nchi nzima unatarajia kuleta changamoto ya ukweli kwa wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya.
*********************
Ni CK wa pili
Akiwa anafanya vyema na kazi yake yenye jina la ‘God Boy’, huku jina lake likiwa linaonekana kuwa juu kupitia chati kadhaa za muziki wa kizazi kipya Bongo zikiwemo Bamiza za Radio Magic FM, msanii Nickson Saimoni kutoka pande za A-Town alisema na ShowBiz kwamba, muziki kwake siyo kipaji tu bali ni kitu ambacho amekifanya kuwa sehemu ya maisha yake.
Akipiga stori na safu hii juzi, msanii huyo ambaye ni mdogo wa mwana Hip Hop, Johmakini alisema kuwa, japo yuko bize na masomo ya Chuo Kikuu akichukua shahada ya Sayansi ya Jamii bado ameweza kujipanga na kupiga ishu kadhaa kunako game ya muziki wa kizazi kipya.
“Siyo masomo tu, hata kama nitamaliza shule na kufanikiwa kupiga kazi nyingine, muziki utakuwa pembeni yangu. Nashukuru hivi sasa napata mashavu kadhaa ya kupiga shoo mbalimbali kupitia kazi nilizofanya ikiwemo hiyo ‘God Boy’. Baada ya shule natarajia kudondoka na albamu yenye jina la ‘The mamas proud’, ndani kuna wasanii kama Johmakini, Mapacha, Rama D, Yusuph, G-Nako, Jacks The Trader, Yusuf na wengine kibao,” alisema.
compiled by mc george
No comments:
Post a Comment