Monday, June 1, 2009

Wasomi wetu wanapogeuka wafagiaji mabanda ya kuku

Na Andrew Mushi

NIMECHOCHEWA kuandika makala haya kufuatia mjadala ulijitokeza kati yangu na rafiki yangu Nkwabi anayeishi, kusoma na kufundisha Uingereza.


Huyu bwana ni mwalimu wa Hisababati na Fizikia, na ndio anavifundisha Uingereza. Mjadala ulianza pale tulipokuwa tunakatiza katika mitaa ya chuo kikuu cha Birmingham hapa Uingereza tukaona jengo moja limeandikwa (Physics and Astronomy). Kwa Kiswahili cha haraka haraka maana ya haya meneno ni Fizikia na Elimu ya Anga za juu.


Kuona maneno ya Physics and Astronomy ilizusha mjadala mkali sana lakini unaorutubisha akili kati yangu na huyu rafiki yangu. Bwana Nkwabi alianza kwa kusema wenzetu Waingereza wanachokisoma wanakifanyia kazi kwa vitendo ndio maana wanaweza kupeleka vyombo mwezini na katika anga nyingine za mbali, achilia mbali mambo mengine luluki makubwa wanayoyafanya. Elimu ya Waingereza inaendana na uhalisia wa mambo. Hawaandai mitaala ya masomo ili tu kujiridhisha.

Nikupe mfano mwepesi, wiki jana nilienda shuleni kwa binti yangu anayesoma shule ya awali, kumchukua baada ya muda wa masomo kwisha. Kwa kawaida kwa sheria za Uingereza watoto wa shule za awali, na msingi lazima wapelekwe shule na kufuatwa kurudishwa nyumbani na wazazi au walezi wao. Hii ni ili kuakikisha usalama wa watoto.

Nilipofika shuleni nikakuta mapokezi wameweka machine mbili ndogo za kuangulia vifanga vya kuku na wakawa wanaanguliwa. Ukubwa wa kila machine ni futi moja kwa futi moja.

Kwa hiyo watoto wakawa wanoana vifanga wa kuku wanavyoanguliwa. Bila kuambiwa chochote watoto wanajifunza vitu vingi sana. Mie mwenyewe binti yangu japo ana miaka miwili na nusu, alianza kuniuliza maswali mengi sana kuhusu mayai, kuku, ndege na kadhalika.

Bwana Nkwabi akaigeukia Tanzania, na kusema wasomi wetu, hasa akimaanisha maprofesa na madakitari wa falisafa wanachojifunia ni ‘papers’ ngapi wameandika na kuwasilisha katika makongamano. Nami nikachapia kwa kusema pia wanaona sifa na fahari kwa wingi wa kuku na ngombe wanaofuga na bar wanazomiliki. Naye akachombeza, sasa kwa mtindo huu ni saa ngapi tutaona elimu yao ikitembea barabarani.

Kutoka hapa tukajadili je ni kwanini wasomi wetu wanashindwa kutafsiri elimu walio nayo katika bongo zao ikaonekana na jamii na kutunufaisha kama Taifa. Tukakimbilia jibu rahisi na labda la kichovu kwa vile hatukupenda kufikiri kwa kusema wasomi wetu hatuwapi rasilimali pesa na pia nafasi. Ila hatukujadili je kwanini wasingepewa hizi pesa za EPA badala ya kuwachia akina Green na Kagoda Industrial wazisunde wavavyotaka.

Sikuvunjika moyo maana nilikumbuka nchi ya Ghana, ambayo ni waafrika wenzetu.
Wao mitaala yao imeelekezwa kumuanda Mghana kufanya kazi pahala popote duniani. Ndio maana katika katika kazi kubwa na mashirika ya kimataifa hutakosa Mghana.

Kwa jinsi hii siwezi kushangaa Kofi Anan wa Ghana alifanikiwaje kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, maana ni matunda ya mikakati ya makusudi kielimu.

Katika mada hii nitajaribu kujadili na kuchokoa kuwa licha ya kisingizio cha kutokupewa pesa na nafasi bado wasomi wetu wanaweza kutoka katika vyumba walivyojifungia na kutumia mianya mingi iliyopo na kuweza kutafasiri elimu yao katika vitendo.

Ila ni lazima tuanze na msingi nzuri na imara Nitajaribu kujikita katika elimu ya msingi na kiasi fulani elimu ya awali kujadili tufanye nini. Maana naamini tukishakuwa na msingi na mitaala mizuri huko chini, sekondari, vyuo vya kati na hata nyuo vikuu haitakuwa kazi ngumu, maana itakuwa ni jadi yetu.

Pa kuanzia ni kuifanyia ukarabati mkubwa mitaaala yetu ili iendane na hali hali halisi ya kiuchumi na dunia na zaidi izingatie mazingira yetu. Nitatoa mifano michache ili ichokoze kufikiri kwetu.

Nianze na mfano wa somo la historia, badala kungangania kujua historia ya kila pahala duniani. Somo la historia lifundishwe na kuakikisha mwanafunzi anaijua historia ya nchi yetu barabara.

Tunawacheka Waingereza au Wamarekani watoto wao wanapokua hawajui historia au mambo ya nchi nyingine, ila ya kwao wanayafahamu kama sala ya Bwana. Wanaona haiwasaidii chochote watoto wao kuimba kama kama kasuku mambo ya kila pembe ya dunia, wakati yalio uhani kwao wanayajua nusunusu.

Mfano mwingne ni somo la Jografia. Kwa jinsi linavyofundiswa sasa hivi halimuandai na kumfanya mtoto aelewe mazingira ya Jografia ya Tanzania na jinsi ya kupambana nayo.

Mtoto atakariri wee Tanzania kuna mito, maziwa, milima, madini kiasi gani, bas! Tungeenda hatua moja zaidi na kumfanya aone je, hivi vitu vinagusaje maisha yake moja kwa moja.

Mathalan, badala ya kujifunza juu ya Tanzania kuna bahari, mito na maziwa mangapi, mtaala unaweza kwenda mbali zaidi kwa kutoa mwanya watoto wakajadili kwa kina ni jinsi gani hayo maziwa na bahari vinaweza vikatumika kusaidia kuinua maisha ya maeneo ya watu husikika.

Wakati huo watoto wa maeneo mengine nao wanajadili kwa kina Jografia ya eneo lao na jinsi ya kuitumia vizuri kwa manufaa yao.Hata kama ni mtoto wa darasa la awali bado kitu kama hiki kitamsaidia sana badala ya kukimbilia kukaririsha watoto wetu vitu vingi visivyo na kichwa wala mkia.

Masomo mengine kama hisabati, kiswahili, maarifa na hata uraia navyo tusivifanyie ajizi. Mfano, somo la uraia, tuligeuze kimwandae mtoto kuwa raia makini na mzalendo anayeipenda nchi yake.

Badala ya kukariri habari ya bunge, vikao vya vyama siasa na mifumo ya uongozi na kuishia hapo hapo tuvuke mpaka twende kwenye uhalisia wa mambo.
Mfano, kwa shule zilizo karibu na halimashauri au makao makuu ya wilaya. Mtaala uruhusu watoto wapate nafasi ya kutembelea wakati wa vikao vya madiwani na kuona wanavyoendesha vikao vyao.

Na pia wapewe nafasi waongee na madiwani na waulize mswali, namna hii watajua jinsi siasa na uongozi unavyoendeshwa. Na kwa upande wa walio mbabali na makao makuu ya wilaya, wakati wa vikao vya wa vijiji, kuwepo na fursa ya kuona jinsi hivi vikao vinavyoendeshwa.

Kwa lugha nyepesi, maadam kila shule hapa nchini iko ndani ya kijiji na au mjini, basi kuwepo na kipengele kinachosistiza watoto wajue kwa vitendo jinsi uongozi wa kijiji unavyofanya kazi.

Kwa mtoto kuelewa mfumo wa uongozi wa kijiji chake na jinsi unavyofanya kazi, unaampa nafasi ya kujiskia mwakajiji/mtaa. Na kwa jisi hii anaweza kutumia haya maarifa akayahusisha na ngazi ya wilaya, mkoa taifa na hata umoja wa mataifa.

Afya nalo ni eneo linaweza kushughulikiwa katika mitaala ya shule za msingi na likawa na mafanikio mengi sana katika maisha. Mfano, mtaala unaweza kutoa nafasi kwa watoto kufahamu huduma za afya zilizoko ndani ya maeneo yao.

Hospitali, vituo vya afya, zahanati zimetapaka kila mahali. Watoto watembelee hizi sehemu wajifunze zinavyonya kazi. Wajadili na waganga na wauguzi walio katika haya maeneoa ni jinsi gani watoto wanaweza wakawa na afya njema bila kwenda hospitali.

Watoto kupata nafasi ya kuongea na wauguzi na waganga na hata kuona wanavyotibu watu, kuona maabara zinavyofanya kazi, itakuwa na matokea mazuri sana kwa watoto wetu. Mathalan, watoto wakitembelea hospitali na muuguzi akawaelezea umuhimu wa kuchemsha maji ya kunywa, labda wakaonyeshwa kwa darubini vidudu walio katika maji yasiochemshwa na badaye yakachemshwa wakaonyeshwa yalivyo salama. Nina uhakika baada ya hapo hakuna mtoto atakunywa maji bila kuchemsha.

Ninaweza kutoa mifano mingi sana, lakini ujumbe ninaojaribu kuletwa kwako ni kuwa tutumie vitu vinavyopatikana katika maeneo yetu kujifunza na pia kuwapa nafasi watoto kuvielewa. Nataraji wizara ya Elimu watazingatia changamoto hii, na pia sisi wananchi tuwashinikize watunge mitaala ya kutukomboa badala ya hii ya sasa inayotudumaza kila kukicha!

1 comment:

Anonymous said...

Hongera kwa kuandaa makala nzuri na yenye kutufungua macho!
Mdau, RG30, Berkshire