Wednesday, June 3, 2009

VIJUE VYAKULA BORA NA FAIDA ZAKE MWILINI-2

Wiki iliyopita tulianza makala haya kwa kuangalia vyakula muhimu na umuhimu wake katika ustawi wa afya zetu, ambapo tuliona baadhi ya vyakula hivyo, kama vile Samaki, Maharage ya Soya, Karanga, Karoti, mapapai, n.k na leo tunaendelea kuangalia vyakula vingine kama ifuatavyo:- Kumbuka chakula ni uhai, lakini pia chaweza kuwa sumu kama hakiliwi ipasavyo na jinsi ulivyo kunatokana na unavyokula.

KITUNGUU SAUMU
Hiki ni kiungo cha mboga, licha ya kuonekana kama ni kiungo cha kuongezea ladha tu ya chakula, lakini ni miongoni mwa vyakula vyenye faida kubwa katika afya zetu. Kitunguu saumu husaidia kuyeyusha damu mwilini hivyo kumuepusha mlaji na kushikwa ugonjwa wa moyo pamoja na presha. Kitunguu hiki pia hutoa kinga kwenye ini na huondoa maumivu ya viungo. Kula angalau kitunguu kimoja mara moja kwa wiki.

ABDALASINI
Hiki nacho ni kiungo cha kuongezea ladha na rangi kwenye chakula, lakini nacho kina faida zaidi ya hiyo. Abdalasini, ambayo inapatikana kwa wingi katika masoko mbalimbali nchini, hufaa sana kutumiwa na wagonjwa wa kisukari, kwani hurekebisha kiwango cha sukari mwilini kwa kiwango cha hadi pointi 50. inapendekezwa kutumiwa angalau nusu kijiko cha chai kila siku mara mbili.
TANGO
Watu wengi hulipuuza tango na wengine hawajawahi kula kabisa kwa sababu siyo tamu sana mdomoni, hata linapochanganywa kwenye kachumbari huepukwa. Hii yote inatokana na kutokujua umuhimu wa mboga hii. Inaelezwa kuwa tango linapoliwa husaidia sana kusaga chakula tumboni hivyo kumuwezesha mlaji kupata choo laini. Halikadhalika, tango linaweza kutumika katika kuboresha ngozi ya uso kwa kupaka, kwani huondoa vipele na kuifanya ngozi kuwa nyororo. Ni zuri linapoliwa na maganda yake na unaweza kula kiasi utakachoweza.

ASALI
Kama kuna chakula kitamu na kizuri duniani, basi ni asali. Hiki ni chakula cha asili ambacho kimekuwepo enzi na enzi na kimesifiwa hata katika vitabu vya Mungu. Asali ina uwezo wa kudhibiti sumu mwilini, ina uwezo wa kumfanya mtu mnene kupungua uzito na mtu mwembamba kuongezeka uzito hadi kufikia uzito wa kawaida. Asali huupa nguvu mwili haraka, huifanya ngozi kuwa nyororo, huzuia asidi, husafisha damu na ina uwezo wa kuua vijidudu mwilini. Lamba asali kijiko kimoja cha chai asubuhi kabla hujala kitu chochote. Kwa kuwa asali ni tamu lamba mara 3, wagonjwa wa kisukari wanashauriwa kuila kwa tahadhari.

TENDE
Tende, ambayo ni maarufu sana katika nchi za arabuni na ukanda wa mwambao wa Tanzania, ni miongoni mwa vyakula vyenye faida kubwa mwilini. Sifa ya kwanza ya tende ni uwezo wake wa kuupa nguvu moyo dhaifu na kuupa nguvu mwili (energizer). Wale wenye matatizo ya moyo kukosa nguvu tende zitawasaidia. Tende nayo ni mlo tosha unaopaswa kuwepo katika orodha ya milo yetu ya kila siku.

Katika maisha tunayoishi hivi sasa, ili mtu kuupa mwili wako kinga imara dhidi ya maradhi mbalimbali na ya hatari, hatuna budi kuzingatia ulaji wa vyakula mchanganyiko vya asili na kuacha kupenda kula vyakula visivyokuwa na faida katika miili yetu ambavyo mara nyingi tunapenda kuvila, kwa sababu ni vitamu mdomoni.

No comments: