Monday, June 1, 2009

WIKIENDA SHOWBIZ!

ROHO SITA Sokoni leo
Ile muvi ya Kibongo iliyotokea kujipatia umaarufu mkubwa kabla haijaingia sokoni, ‘Roho Sita’ inadondoka mtaani leo ikiwa kwenye DVD, VCD na VHS kama tulivyokuwa tikiwahabarisha kupitia magazeti yanayochapishwa na Kampuni ya Global Publishers.

Mkurugenzi wa Filamu za Kampuni ya Tollywood Movies, ambayo imechukua dhamana ya kuisimamia muvi hiyo, Hamie Rajab alisema kwamba, kutoka kwa kazi hiyo sokoni kutawapunguzia malalamiko waliyokuwa wakiyapata kwa wapenzi wengi wa tasnia hiyo ambao walikuwa wakiiulizia kwa muda mrefu.

“Nadhani sasa kila mpenzi wa filamu ‘atainjoi’ baada ya kutoka kwa filamu hiyo, nadhani hata zile kelele ‘filamu ya Roho Sita itatoka lini’ sasa zitapungua. Napenda kuwahakikishia wapenzi wa filamu kwamba, kila kitu kilichokuwa kikiandikwa kuhusu kazi hiyo ni cha ukweli, zaidi ni watu wainunue na kuangalia jinsi watu walivyoumiza vichwa katika kufanikisha sinema hiyo ya kusisimua,” alisema Hamie.
Baadhi ya mastaa waliofanya kweli ndani ya muvi hiyo ni pamoja na mrembo Chuchu Hans (anayeonekana katika pozi pichani)ambaye sura yake imekuwa ikibadilikabadilika na kutisha, Ndumbangwe Misayo ‘Thea’, Charles Magali na wengine kibao.

Filamu hiyo inapatikana katika Duka la Tollywood Movies lililopo mtaa wa Agrey Kariakoo na maduka mengine ya sinema nchini. Kwa wanunuzi wa jumla wanaweza kuwasiliana na Kampuni ya Tollywood kwa simu namba 0754 267461. Wahi nakala yako sasa!
********************************************
TEARS ON VALENTINE DAY: Kuibua vipaji, Movie Star Scouting yasogezwa mbele
Filamu mpya ambayo inakuja hivi karibuni kutoka ndani ya Kampuni ya Tollywood, ‘Tears on Valentine Day’ iliyoandikwa na mtunzi Eric Shigongo inatarajia kuibua vipaji vya wasanii chipukizi ambao wataungana na baadhi ya mastaa waliopo kunako tasnia hiyo kisha kufanikisha zoezi zima la uandaaji wa muvi hiyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Filamu za Kampuni ya Tollywood Movies, Harmie Rajabu wamelazimika kuandaa filamu hiyo ambayo inatakiwa kutoka kabla ya mwezi Agosti mwaka huu na kusitisha lile shindano kubwa la kutafuta vipaji, ‘Movie Star Scouting’ ambalo lilikuwa lifanyike nchi nzima hivi karibuni.

“Tumelazimika kusimamisha lile shindano la ‘Movie Star Scouting’ kwa muda ili tupate muda wa kuandaa filamu hii huku tukipata muda wa kuliandaa vizuri shindano hilo ambalo tutalifanya baada ya kazi hii kukamilika. Tunachofanya hivi sasa ni kutafuta wasanii chipukizi wa Dar es Salaam ambao watashiriki kwenye filamu hii, wale wanaodhani wanakipaji wanatakiwa waje kununua fomu za ushiriki kabla ya kufanyiwa usaili na kuingia kazini.

“Fomu zinapatikana katika ofisi za Tollywood zilizopo Sinza, nyuma ya kituo cha mafuta cha Bamaga kwa bei ya shilingi 5,000, wasanii chipukizi tutakaowapata baada ya kuwafanyia usaili wataungana na wakongwe kama Johari, Kanumba, Jokate, Ray na wengine wengi katika filamu hiyo ya Tears on Valentine Day. Baada ya kazi hiyo itafuata nyingine yenye jina la ‘Mwisho wa Uhai Wangu’ ambayo itawajumuisha chipukizi wengi kutoka mikoani watakaopatikana kupitia shindano la ‘Movie Star Scouting,” alisema Harmie Rajabu.

Mwisho Mkurugenzi huyo alisisitiza tena kuwa, fomu zinapatikana katika ofisi za Tollywood zilizopo Sinza, Bamaga, wanaweza kuwasiliana nao kupitia simu namba 0784 211107 au 0784211108.
********************************************


TMK FAMILY KUWAFARIJI WAATHIRIKA WA MABOMU MBAGALA LEO
Kutoka pande za Temeke, safu hii imedondeshewa ishu kwamba, kundi la TMK Wanaume Family leo litaachia wimbo mpya maalum kwa ajili ya kuwapa pole waathirka wa mabomu Mbagala, Dar es Salaam wenye jina la ‘Hili Tatizo’.

Akipiga stori na Abby Cool & MC George Over The Weekend, kiongozi wa kundi hilo, Said Hassan Fella alisema kwamba, kazi hiyo iliyopo kunako staili ya huzuni imefanyika kupitia Studio za Soundcrafters chini ya mtayarishaji Enrico.

Hiyo inaonesha ni jinsi gani washikaji walivyoguswa na ndugu zao hao wa Mbagala. Je, kwa wasani wengine ikoje?
*************************************


P-SQUARE WA BONGO WAMBURUZA STEVE WHITE STUDIO
Wasanii wawili mapacha, Jonson na Jackson Mwomboke wanaofananishwa na P-Square wa Nigeria ambao hivi sasa wanapaa hewani na ngoma yao ‘Usife Moyo’ wamejipa ufagio kwa kusema kuwa walimburuza Prodyuza Steve White aliyewarekodi kwa kufanya sehemu kubwa ya kazi hiyo wao tofauti na wasanii wengine ambao wamekuwa wakiwasikiliza zaidi watayarishaji.

Ndani ya safu hii vijana hao wanaofanana kwa karibu kila kitu walisema kwamba, walitaka kumuonesha mtayarishaji huyo kwamba miaka kadhaa waliyokaa kwenye game ya muziki ikiwemo kuusomea pale kwenye nyumba ya kukuza na kuendeleza vipaji (THT) tayari wamekomaa na wanaweza kufanya vitu vingi kama wao badala ya kuburuzwa na watayarishaji muziki kama ilivyo kwa wasanii wengine wa Kibongo.

“Steve White’ ni mtu wetu wa karibu ambaye anatufahamu siku nyingi lakini tulipoenda kurekodi katika Studi za Bion alipokuwa anafanyia kazi mwanzo tulitaka kuonesha kuwa sisi tumekomaa katika game, tukamwambia akae pembeni kazi yote tutaifanya wenyewe yeye aje amalizie mwisho kwenye mix tu. Kwa hiyo vitu vingi tukafanya sisi ndiyo maana kazi ikatoka bomba,” alisema Jonson ambaye ni Dotto.

Vijana hao ambao tayari wana albamu moja inayokwenda kwa jina la ‘Usife Moyo’ waliyoikabidhi kwa ‘Wadosi’ wamewataka baadhi ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya wasikubali kuburuzwa na maprodyuza badala yake wawe wanajaribu kuumiza vichwa wenyewe ili kupata kazi wanazohitaji badala ya kusubiri kutengenezewa kila kitu na watayarishaji. Safu hii ilijaribu kumcheki Steve White hewani kupitia simu yake ya mkononi ikawa haipatikani. Lakini tunaahidi kwamba tutamsaka popote alipo ili atuambie ni kweli ‘madogo’ hao walimburuza studio? Tutatoka na ishu hiyo wiki ijayo.
***************************************************


PASTOR WAMBURA ATIMKIA DAR NA FAMILIA YAKE!
Msanii wa nyimbo za Injili aliyejipatia umaarufu kupitia wimbo wake, ‘Bwana ndiye Bwana’ akitumia staili ya sebene, Steven Wambura a.k.a Pastor Wambura aliyekuwa na maskani yake mkoani Arusha, ameamua kutimkia Dar es Salaam ambapo amepiga kambi na familia yake.

Akiwa ndani ya ofisi za gazeti hili na familia yake, muda mchache baada ya kushuka Dar, msanii huyo alisema kwamba kikubwa kilichomfanya akimbie nyumbani kwao Arusha na kuja kunako jiji la Lukuvi ni sapoti ya muziki wake anayoipata ikiwemo kuangusha neno la Mungu kwenye makundi ya vijana wengi waliokimbilia mjini na kujikuta wakiishia kufanya vitendo viovu.

“Siyo kwamba nimehama Arusha moja kwa moja, kule ni nyumbani lakini shughuli nyingi za muziki wangu huwa nazifanyia sehemu mbalimbali ikiwemo hapa Dar es Salaam ambapo nimekuwa nikialikwa mara kwa mara kwa ajili ya mikutano ya Injili huku nikitoa neno la uzima kwa vijana wengi,” alisema Wambura ambaye tayari ana albamu moja yenye jina la ‘Bwana ndiye Bwana’ ambayo ina jumla ya nyimbo nane.
*********************************************


WAREMBO WAONESHA NYETI
Issa Mnally na Richard Bukos

Mwandaaji kukamatwa na polisi, warembo kuonesha sehemu zao nyeti jukwaani, vurugu kuchukua nafasi kati ya mamisi na waratibu ni baadhi ya matukio ya aibu yaliyofunika kinyang’anyiro cha kumsaka Miss Bagamoyo 2009-2010.

Katika shindano hilo lililofanyika Jumamosi iliyopita kwenye Ukumbi wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo, warembo Sarah Noah na Mariam Bakari walionesha sehemu zao nyeti kwa nyakati tofauti na kusababisha hadhira kulipuka kwa mayowe.

Mariam akiwa katika ‘shoo’ ya kujitambulisha, alipanda jukwaani na kivazi ambacho kiliacha wazi sehemu kubwa ya makalio yake, wakati Sarah yeye alipagawa na mayowe ya mashabiki na kujifunua kwa mbele, hivyo kubaki wazi sehemu kubwa ya ‘ustaarabu’ wake.

Mbali na hilo, Mratibu wa Onesho hilo, Charles Buriani alikamatwa na polisi kabla ya kuanza kwa shindano baada ya kushindwa kulipia gharama za kambi ya warembo wake katika Hoteli ya Iringa View Vision.

Tukio lingine la aibu, ni kukosekana kwa zawadi ukumbini, hivyo kusababisha warembo walioshinda na washiriki wote kukamatana mashati na waandaaji wa shindano hilo.

Katika hilo, Mratibu wa Kamati ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga ametupiwa lawama kwa kumpa kibali Buriani wakati akiwa hana sifa, pia analaumiwa kuchukua mamlaka ya msimamizi wa mkoa wa Pwani, Clifford Ndimbo ambaye ndiye mwenye dhamana ya kuteua waratibu wa wilaya kwenye eneo lake.

“Sijui kitu kuhusu huyu mratibu wa Bagamoyo, labda aulizwe Lundenga kwa sababu ndiye aliyempa kibali. Nakubali kwamba sheria inataka mimi ndiye nitoe kibali kwa waratibu wa wilaya,” alisema Ndimbo.

Mbali na mtifuano huo, Salma Suleiman ndiye aliyevalishwa taji la Miss Bagamoyo, wakati warembo walioonesha nyeti, Mariam Bakar na Sarah Noah walinyakua namba mbili na tatu.

Wakati Bagamoyo kukiwa ni mtifuano, Shindano la Miss Universe Tanzania lililochukua nafasi Jumamosi iliyopita kwenye Ukumbi wa Mikutano, Mlimani City, Dar es Salaam halikuwa na swali baada ya kufanyika kwa amani na warembo kupatikana.

Aliyeshinda Taji hilo 2009-2010 ni Illuminata James, mshindi wa pili ni Everline Almas wakati Hidaya Maeda alitoka namba tatu.

No comments: