Sio kila muathirika wa UKIMWI ni mzinzi , muhini au alipata ugonjwa huo kwa njia ya ngono au njia zingine zinazohusiana na zinaa au uzinzi , sio kwamba kila mgonjwa wa ukimwi ametaka kupata ugonjwa huu au alitegemea kupata ugonjwa huu , Lakini ni ukweli usiofichika kwamba wengi wa waathirika walijua au walikuwa na uelewa kidogo wa janga lili na mengine yanayoendelea .
HADITHI FUPI
Jana usiku nilitembelea bar moja mwananyamala inaitwa MK , nilikaa chini karibu na kituo cha basi nikawa namsubiri rafiki yangu Fulani , pembeni yangu alikuwa dada mmoja mrefu amekaa na mwanaume mmoja , wanakunywa wanapigana mabusu na kadhalika
Yule msichana akatoka pale kwenda juu , na mimi nilitoka kwenda msalani ufika huko juu nikakuta yule msichana ameingia choo cha wanaume na mwanaume mwingine wanafanya ngono ya chap chap huku yule mwanaume mwingine ameachwa chini pale na bia yake kaambiwa amekuja msalani .
Nilipotoka pale nikakutana na rafiki yangu mwingine hapo hapo juu , ghafla yule msichana akaitwa na mwanaume mwingine kule kule juu , akakaa nae akaagiza kinywaji kisha akamwambia yule mwanaume kwamba amepata simu ya dharura anarudi nyumbani kwake kidogo atarudi
Kumbe harudi nyumbani anarudi chini kwa yule kidume wake aliyemwacha pale , akaa kidogo pale akavamia jukwaa la kusakata rhumba akaanza kusakata rhumba pale na vijana wenzake huku maisha yanaendelea wakaanza kupenda namba za simu pale pale .
Sikujua kama wale wavulana wanajuana au hawajuani au yule msichana ni changudoa anajiuza au hajiuzi lakini alichokuwa anafanya hakikubaliki hata kidogo na kuvunja maadili kwa kiasi kikubwa .
MAISHA YA NGONO
Kijana mdogo yuko zake secondary labda form 2 hivi , anaanza mahusiano ya kimapenzi na mtu , akifika form 4 labda yuko na mpenzi mwingine halafu tuseme huyu kijana sio mwaminifu kwa mpenzi wake ni mtu mwenye tamaa za kimaisha na kadhalika , akimaliza form 4 anaenda A Level ambako anakuwa mbali na mpenzi wake huko alipo anapata mpenzi mwingine , kama ni sehemu mbali sana hawezi kuwasiliana na wazazi wake kama anashida mbali mbali , basi anaweza kupata wapenzi wengine wa kusaidia mambo yake ya kimaisha na kimasomo .
Huyu kijana wakati wa likizo anarudi nyumbani anakutana na yule mpenzi wake wa nyumbani wanafanya mapenzi na kufurahia maisha yao ya mapenzi , kijana kamaliza ALEVEL anaingia chuoni huko nako anakutana na changamoto kibao za kimaisha na anakutana na vishawishi kibao na anakubaliana na vishawishi hivyo anaingia mtegoni napo anafanya mapenzi na anasa zingine .
Akimaliza chuo anatafuta kazi , mtu aliyempatia kazi alimwomba rushwa ya ngono anatoa ngono , kule kazini kidogo anakuwa na uhusiano wa kimapenzi na bosi wake au wafanyakazi wenzake mbali mbali , bado mpenzi wake anaye .
Kijana huyu anaamua kuingia katika ndoa , wanaishi lakini ghafla wanaaanza kumuumwa na kusumbuliwa na maradhi , kupimwa wanakutwa na UKIMWI , sasa kivumbi kinaanza kumtafuta mchawi ni nani .
Kama unavyoona hapo kijana ameanza mapenzi siku nyingi sana na amekuwa na wapenzi mbali mbali wakati wote huo alikuwa hapimi kuangalia afya yake mpaka alipoingia katika ndoa ndio anapima kujua afya yake tena baada ya kuonekana afya yake iko shakani
Kwahiyo vijana wengi na watu wengi wanaishi na virusi kwa zaidi ya miaka 10 au 5 bila wao kujitambua kama wanaukimwi na kama afya zao ziko salama ili waweze kupanga maisha yao mazuri ya mbeleni , hali inazidi kutisha sana .
KUANGALIA AFYA
Wengi hatuna mazoea ya kupima afya zetu kwa ujumla , mfano mimi nina ratiba ya kuangalia afya yangu kila miezi 2 , hiyo imeshawekwa katika ratiba yangu ya maisha yangu siku zote , kwa jumla ya miaka zaidi ya 10 mfululizo sijawahi kusumbuliwa na ugonjwa wowote zaidi ya mafua ambao ni ugonjwa wangu sugu vyengine siumwi .
Kijana yuko katika mahusiano na mtu hataki kujua afya ya mwenzake , sasa najiuliza kama wanapenda kuishi wote kwa miaka 30 ijayo kwanini usijue afya ya mwenzako kwa faida zako wewe ? siku yoyote anaweza kusumbuliwa na hiyo afya yake kama humjui au kama ulikuwa hauna taarifa si ndio unaanza kuona mzigo kumbeba mwenzako na ndio mnakimbiana ?
Kupima afya iwe ni wajibu wa kila mtu haswa vijana ambao taifa linawategemea kwa ajili ya shuguli zaidi sasa hivi na hata siku zijazo , kama vijana hawataki kupima afya zao , taifa haliwezi kujua na halitamudu kuwahudumia vijana wote walioadhirika kwa sababu ya takwimu ndogo au za uwongo walizokuwa nazo .
UKIMWI SIO MWISHO WA MAISHA
Kama unaenda kupima ukajua umeathirika ongea na mpenzi wako nae ajue kuhusu kilichokusimu , uwe wazi kwa mpenzi wako kuhusu mambo haya , wengi hawataki kusema na badala yake wanavunja ndoa au mahusiano na kwenda kuanza maisha mengine na wapenzi au wanandoa wapya
Wengine wanafikia hata hatua ya kwenda makanisani kubadilisha dhehebu na kuokoka , nimeona makanisa mengi ya kilokole siku hizi yamevamiwa na watu waliokata tamaa wameathirika wanaenda kutumia kioo cha ulokole kujisafisha huku wanaendelea na dhambi zao kwa kasi ile ile
Niliwahi kwenda katika msiba mmoja , huyu kijana alikuwa mwathirika , alipoona anakaribia kufa akaamua kwenda kuokoka na kufuta uvumi mitaani kwamba jamaa alikuwa yuko safarini na alikuwa mbeba silaha za maangamizi , kweli mchungaji akampokea yeye mchungaji si anataka sadaka tu ? hataki zaidi ukitoa sadaka wanafanya sala na kukupa huduma zote
Huyu kijana akafariki baada ya wiki 3 hivi , katika mazishi yake mchungaji akamsifia kijana yule kwamba alikuwa kijana mwerevu , mfanyakazi hodari na msikivu , lakini mungu amemchukuwa ghafla kwa ugonjwa wa malaria tunasikitika sana lakini nasi tunaenda huko huko , wote tutaitwa na muumba kwenda kwa njia kama ile tuliyojia nayo
Mchungaji akamaliza kwa hutuba yake , na hapo vijana waliokuwa pembeni wanasikiliza wakaingiwa na ushawishi kwa kwenda nao kujificha makanisani walivyojua wameadhirika , na ni kweli makanisani siku hizi wamejaa wazinzi , waasherati kuliko kipindi chochote cha maisha watu wanatumia makanisa na ulokole wao kuuhadaa ulimwengu .
MSIMAMO WA MAISHA
Wakati Fulani nikiwa secondary mwalimu wangu alifundisha somo Fulani la kujitambua , anasema kijana lazima ujue kwanini umezaliwa , kwanini uko hapo ulipo sasa hivi , unatakiwa ufanye nini kwa maisha yako na wengine wanaokuzunguka na mwisho wa siku ufanye nini kuwa na msingi bora wa maisha yako ya mbeleni .
Kama hauna msimamo wa kujua wewe ni nani na majukumu yako katika dunia hii , pia huwezi kuwa na msimamo wa maisha ya kimapenzi na uhusiano na mpenzi wako , katika kutumia kinga au zana wakati wa kufanya vitendo vya ndoa incase ukitakiwa kufanya hivyo .
Kuna tatizo lingine la vijana wengi kutokuwa na msimamo kuhusu maisha yao yote kuanzia ya kimapenzi na mambo mengine , katika hili siwezi kumshambulia kijana peke yake , tuangalie wazazi wao wanafanya nini au walifanya nini kuhakikisha kijana wao anakuwa mtu mwema na kumweka katika maadili yanayofaa ili kukabiliana na maisha huko mbeleni anapoenda .
Baba yetu alikuwa na mazoea ya kutuita mimi na ndugu zangu wengine kuongea na sisi kila baada ya mwezi mmoja , kuuliza unafanya nini , una mipango gani na kama umeshindwa kitu ni kitu gani umeshindwa , na je kama unataka msaada kutoka kwake wa aina yoyote ile .
Baba yangu ni kati ya wazazi wachache wanaojali sana familia yake na watu wake wa karibu katika mambo yake popote anapoenda na kutembelea , wazazi wengi wanatakiwa wawajengee watoto wao uwezo wa kuwa wawekezaji wazuri na wazalishaji wazuri katika stali zao za maisha .
Kama mtu ukilelewa vyema ukawa na msimamo wake wa maisha hautaweza kuhujumiwa katika mambo mengi tu hapa duniani moja wapo ni hilo la vishawishi vya anasa mbali mbali katika maeneo unayotembelea .
CHANGAMOTO KWA VIJANA
Tunajua kwamba ukimwi upo na utaendea kuwepo hatuna budi kuwa na misimamo yetu haswa ya kujua afya zetu kwa njia ya kupiima ili tuweze kuwa wema na wenye malengo na maisha yetu ya baadaye , ukishapima na kujua majibu yako lazima utakuwa na msimamo Fulani katika maisha yako , lazima utakuwa na mabadiliko Fulani katika maisha na mwenendo wako
Lakini mwisho wa siku suala la ukimwi ni binafsi sana , huwezi kwenda kuongea na kumuelimisha mtu kuhusu UKIMWI kama yeye mwenyewe hajaamua kujielewa na kujitambua majukumu yake katika jamii inayomzunguka .
Nawapa pole wale wote waliadhirika na ugonjwa huu popote walipo lakini wawe na matumaini na maisha mema hapo mbeleni , siwezi kuwalaumu au kuwaponda sio wote wamepata ukimwi kwa kujitakia , wengine wameambukizwa na wapenzi wao wasio waaminifu , wengine bahati mbaya mahospitalini au katika ajali zingine makazini au sehemu wanazotembelea
Wengine ni kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu ugonjwa huu , wengine ni misimamo yao haswa waliokuwa katika mahusiano hata ya ndoa na wengine ni wenyewe wameamua kujitoa mhanga kutokana na maisha kuwabana au kusumbuliwa na msongo wa mawazo
By Yona Fares Maro
I.T. Specialist and Digital Security Consultant
1 comment:
NAKUBALIANA NA WEWE MTOA HADITHI HII HALI IMEKUWA MBAYA SANA ...ILA WATU HAWATAKI KUAMINI HIVYO, KUNA FAMILIA MOJA (JIRANI YANGU) BABA, NA WATOTO 6 WOTE WAMEFARIKI KWA JANGA HILI LA UKIMWI, FIKIRIA HAO WATU WALIKUWA WANALIKUWA WANA WAPENDI WAO, BAADHI WAMEONA NA KUACHA TENA...JAMANI NAWAASA WATANZANIA WENZANGU...USIMUAMINI MTU, USIMUONEE AIBU PIMA KABLA YA KUKUTANA KIMWILI, ILA TATIZO LA WABONGO (BAADHI) LEO AKIPIMA, AKIONEKANA MZIMA KESHO AKILEWA ANABEBELEA MZOGA.
Post a Comment