Tuesday, November 17, 2009

Madhara ya unene kiafya


You are what you eat

UNENE umekuwa ni tatizo kubwa na sawa na janga la dunia. Tatizo hili limekuwa adui mkubwa wa binadamu kwa sababu limesababisha matatizo mengi ya kiafya na limeshapoteza maisha ya watu wengi hadi sasa. Kwa lugha nyepesi, unene wenye madhara kiafya ni ule wa kupita kiasi (tipwa tipwa) ambao hutokana na kuzidi kwa mafuta mwilini na mara chache husababishwa na vinasaba vya kurithi (genes).

Kitaalamu, kuna maneno mawaili ya lugha ya kiingereza yanayoshabihiana katika kuelezea unene, Over Weight na Obese.Inaelezwa kuwa mtu akizidi uzito wake wa kawaida kwa asilimia kati ya 10 hadi 19 anahesabika ni overweight. Aliyezidi kwa asilimia 20 na kuendelea huyo anakuwa ni obese na kama inavyoeleweka, uzito wa kaiwada wa mtu unategemea urefu, umri na jinsia yake.

Hivyo basi, unene wa kupindukia huwa ni matokeo ya kujikusanya kwa wingi kwa mafuta mwilini. Nishati inayoingia ikiwa kubwa kuliko ile inayotoka, matokeo yake huwa ni kurundikana kwa mafuta kwenye mwili na unene huwa ni machakato wa tataritibu ambao hautokei kwa wiki moja ama mbili 2. Watu wenye tabia ya kula sana bila kufanyakazi wala mazoezi ndiyo wanaopatwa na tatizo hili. Kanuni ya kudhibiti unene iko wazi.

Ukitaka kupunguza unene, kula kidogo, fanyakazi sana au mazoezi na ukitaka kunenepa, kula sana, usifanye kazi wala mazoezi na ukitaka kubaki hapo ulipo, kula kulingana na kazi unazozifanya au mazoezi unayoyafanya. Unene ni mbaya, huharibu afya ya mtu, kimwili na kiakili pia. Vile vile huwa ni adha unapojumuika na watu wengine ambao mara nyingi huwadhihaki watu wanene. Lakini mbaya zaidi, unene una karibisha magonjwa mengi hatari, yakiwemo ya moyo, kisukari, kiharusi, presha, n.k.

DONDOO MUHIMU KUJIEPUSHA NA UNENE
Weka utaratibu wa kula chakula kisichokuwa na mafuta na chenye mafuta kipunguzwe au kiondolewe kabisa katika orodha yako ya vyakula. Acha kula na kushiba kupita kiasi. Hakikisha siku zote unakula kiasi, usile mpaka ukashindwa kuhema. Unapokuwa kwenye sherehe mbalimbali, pendelea kula vyakula vya asili, kama matunda, saladi ya mboga na jiepushe na tabia ya kula vyakula vyote vilivyopo mezani. Kula kiasi kulingana na shughuli unazozifanya.

Kama ni mtu wa kukaa ofisini, usile sawa na anayefanyakazi nyingi za kutembea kwa siku. Pia fanya mazoezi kila siku, hata ya kutembea tu.

No comments: