Tuesday, December 29, 2009

Matatizo ya usingizi: Unaweza kuyatibu kwa chakula


Wataalamu wanatuambia kuwa mwanadamu anahitaji kupata usingizi mzuri ili kuondoa madhila ya mchana na kuimarisha afya yake. Mtu anapokosa usingizi au anapokuwa na usingizi mwingi kupita kiasi, hali ya afya yake huweza kutetereka.

Matatizo ya usingizi ni nini?
Matatizo ya usingizi yanaelezwa kuwa ni ile hali anayokuwanayo mtu ya ama kukosa usingizi au kuwa na usingizi mwingi kupita kiasi kwa kulala kila wakati au kwa muda mrefu. Usingizi ni sehemu muhimu sana ya afya bora ya mtu kama ilivyo katika suala la lishe bora.

Mtu anapokuwa amelala, mwili hupata muda wa kufanya ukarabati muhimu katika sehemu mbalimbali za mwili kama vile chembe za uhai, mfumo wa kusaga chakula, mapigo ya moyo, upumuaji, n.k. Usingizi mzuri unahitajika pia katika ukarabati wa mfumo wa kinga ya mwili na fahamu.

Mtu mzima na mwenye afya njema anapaswa kulala kwa muda wa saa 6 – 8 kwa siku, kinyume na hapo afya yake inaweza kuathirika kwa namna moja ama nyingine.

Sababu za matatizo ya usingizi
Kuna sababu nyingi zinazosababisha matatizo ya usingizi (Sleeping Disorders), ikiwemo kubadili mfumo wa maisha kwa kufanya kazi za shifti, kusafiri kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine yenye muda tofauti. Mfadhaiko wa akili, msongo wa mawazo au matumizi ya dawa kali ya tiba.
Tiba mbadala ya matatizo ya usingizi
Ingawa ni jambo muhimu kuonana na daktari kwanza iwapo una tatizo sugu la usingizi, lakini kuna vitu vingi unavyoweza kuvifanya nyumbani kukabilina na tatizo hilo na hatimaye kupata tiba mbadala.

Awali ya yote, unatakiwa ujiwekee ratiba ya kulala ambayo ni lazima uiheshimu. Lala na uamke kwa mujibu wa ratiba uliyojiwekea ili mwili uzoee hali hiyo.

Kabla ya kupanda kitandani, tafuta mbinu za kupumzisha akili kwanza, kama vile kujisomea, kuangalia televisheni au kutembea kwenye bustani au kufanya jambo lolote linaloweza kutuliza akili na mwili.

Matatizo mengine ya usingizi yanaweza kutatuliwa kwa kujua njia sahihi ya ulalaji. Kulala kifudifudi siyo kuzuri kwani kunaweza kukwamisha mzunguruko wa hewa mwilini kwa sababu ya kuziba kwa njia za hewa. ulalaji sahihi ni ule wa kulala kiubavu ambao huruhusu mzunguruko mzuri wa hewa na damu mwilini.

Chakula kama tiba
Chakula tunachokula, hasa kile cha muda mfupi kabla ya kwenda kulala, kina athari kubwa kwenye suala zima la kupata ama kutokupata usingizi. Hivyo inashauriwa kuepuka unywaji pombe, uvutaji sigara na ulaji wa vyakula vyenye ‘caffeine’ kama kahawa ambavyo huondoa usingizi.

Vyakula vinavyochangia usingizi mzuri unavyopaswa kula kabla ya kupanda kitandani ni pamoja na ndizi mbivu, maziwa ya moto au mtindi pamoja na bidhaa nyingine zitokanazo na maziwa.

Nyingine ni mboga za majani, vyakula vya nafaka zisizokobolewa (whole grains), karanga, parachichi na mboga za majani. Wakati inaeleweka kuwa ni muhimu mtu asilalale na njaa, lakini pia tahadhari ichukuliwe mtu asipande kitandani akiwa ameshiba kupita kiasi!

Mbali ya kuzingatia suala la lishe, inashauriwa pia kutumia njia zingine za kuufanya mwili kupumzika (body relaxation) kama vile kuchua mwili (body massage), kufanya ‘meditation’ ili kuondoa msongo wa mawazo. Pia ni vyema kulala katika mazingira yasiyo na kelele wala usumbufu wa aina yoyote, ukizingatia hayo tatizo lako la kukosa usingizi au kulala kupita kiasi, litakwisha.

No comments: