Tuesday, May 4, 2010

Unapokula hakikisha unatafuna chakula


you are WHAT YOU EAT
Kuna watu wana matatizo ya ukosefu wa choo kwa muda mrefu, licha ya kula chakula sahihi na kufuata kanuni zingine za ulaji. Hali hiyo hutokana na tabia ya kumeza chakula bila kutafuna, ambayo katika makala ya leo tutaona athari zake zilivyo kwa mfumo mzima wa usagaji chakula tumboni.

Iwapo unahitaji kukamilisha kanuni za ulaji sahihi na mwishoni kupata matokeo unayotarajia ya kuwa na afya bora, huna budi kuzingatia suala la kutafuna chakula kwanza kabla ya kukipitisha kwenye koromeo lako na kukimeza.

Utafunaji wa chakula ni muhimu kwa sababu ndiyo hatua ya kwanza ya usagaji chakula tumboni inapoanzia. Kutafuna huchanganya chakula na mate ambayo hulainisha chakula na kuwezesha ‘enzymes’ kuvipata vipande vya chakula na kuanza mchakato wa kusaga wanga na mafuta kwa wepesi.

Unapokula bila kutafuna vya kutosha, chakula huingia tumboni kikiwa katika vipande vikubwa kupita kiasi. Kwa kuwa ‘enzymes’ wana uwezo wa kusaga vipande laini, hali hiyo husababisha chakula kushindikana kusagika sawasawa tumboni.

Hali hiyo inapotokea, siyo tu virutubisho vilivyomo kwenye chakula huenda kwenye utumbo mpana bila virutubisho vyake kutumika mwili, bali pia hugeuka na kuwa chakula cha ziada cha ‘bakteria’ na chakula cha ziada husababisha kukukua kwa ‘bakteria’ na kuongezeka kwa gesi tumboni na ukosefu wa choo hujitokeza.

Ili upate choo cha uhakika kila siku, ni lazima mfumo wa usagaji chakula tumboni ufanye kazi yake vizuri na mfumo huo hauwezi kufanya kazi sawaswa kama chakula kikiliwa bila kutafunwa ipasavyo.

Aidha, chakula kinapoingia tumboni, kinahitaji msaada zaidi wa kuwezesha usagaji wake kwa kuimarisha ufanisi wa vimeng’ enya (enzymes) kwa kula mananasi fresh pamoja na mapapai ambayo yanaelezwa kuwa na virutubisho vya kutosha vya kuimarisha vimeng’enya vya chakula tumboni.

Ili kujiepusha na tatizo la ukosefu wa choo kwa muda mrefu kunakotokana na mfumo mbovu wa usagaji chakula, suala la kujiepusha na mfadhaiko wa akili (stress) ni lazima. Utafiti umeonesha kwamba ‘stress’ huathiri mfumo wa usagaji chakula pia.

Mtu anaweza kujikuta anakosa choo kwa sababu ya kuwa na stress za maisha, hivyo inashauriwa kuishi katika mazingira yasiyokuwa na bugudha. Zingatia ratiba ya chakula na kula chakula chako katika mazingira tulivu.

Ulaji kwa kiwango kikubwa wa sukari na unywaji wa pombe na kahawa kupita kiasi, hauna budi kuachwa ili kuondoa tatizo la ukosefu wa choo wa muda mrefu.

Ni muhimu kujua kwamba ukosefu wa choo wa muda mrefu, ni dalili ya tatizo lingine la kiafya ambalo linaweza kuibuka wakati wowote na kudhuru mwili wako.

Kwa kawaida, kama unakula kila siku, unatakiwa kupata choo kila siku pia, angalau mara moja kama siyo mara 2 au 3 kwa siku, choo ndicho kinachotoa nje sumu na uchafu mwingine usiohitajika mwilini, hivyo unapobaki mwilini bila kutoka, hugeuka kuwa sumu na maradhi.

1 comment:

Disminder orig baby said...

Mada nzuri sana, nashukuru sana. tafadhali kaka zidi kutuelimisha, nakubaliana na stress. Ni wiki imepita sasa toka nitoke hospital niliambiwa hili suala. nawe umemaliza kabisa. na huwezi amini nimejitahidi kufuata ushauri wa dokta, naendelea vizuri.