Monday, September 12, 2011

SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUTOKA JUMUIYA YA WATANZANIA LONDON...!!!

 Jumuiya ya Watanzania London kwa ujumla tumepokea taarifa ya ajali kuzama meli iitwayo Spice Islander iliyotokea Nungwi njiani kuelekea Pemba kwa masikitiko na mshtuko mkubwa. Tunaungana na Watanzania wote wa visiwani Zanzibar na hata wa bara kwa msiba huu mkubwa kwa Taifa. Jumuiya ya Watanzania London inawapa pole sana wafiwa wote, walioathirika na janga hili moja kwa moja ikiwa ni pamoja Watanzania wote na zaidi wale waliofiwa na ndugu zao, jamaa na marafiki. Jumuiya ipo nanyi kwa hali na mali kushirikiana nanyi katika kipindi hiki kigumu.

Pia jumuiya inawashukuru waokoaji maana idadi kubwa wameweza kuokolewa kama tulivyoona kwa magazeti ya leo likiwemo “The Independent” (London,UK) kwamba waliokufa ni 197 na walioweza kuokolewa ni 619, tofauti na ilivyokuwa MV Bukoba ambapo kati ya wengi waliokufa, 114 tu ndio waliookolewa. Kwa hili tunamshkuru Mungu na tunajiunga na Watanzania katika kuamini kwamba ajali kama hizi hazitatokea tena pale ambapo zinaweza kuzuilika, hasa kwa hatua itakayochukuliwa baada ya kubaini meli ilizidiwa na idadi ya watu na mizigo.

Aidha, jumuiya ya Watanzania-London, tunaishukuru serikali ya Tanzania bila kumsahau Mh. Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutangaza siku tatu za maombolezo. Siku hizi tunaamini Watanzania kwa ujumla hasa walio nchini Tanzania wameweza kupata nafasi ya kupeana faraja wakati huu wa msiba. Walioweza kuzitembelea familia zilizoathirika, na hata walioweza kutumia mtandao au simu za mkononi kuwasiliana na ndugu jamaa na marafiki katika kupeana pole kwa namna moja au nyingine Mungu awabariki sana.
Mungu ibariki Zanzibar, Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Africa na dunia nzima kwa ujumla. Zaidi sana Mungu wabariki Watanzania wote popote pale walipo duniani.


Jumuiya Ya Watanzania London
 Tanzania Association London
 123 Old Ford Road
 London E2 9QD
 Cell: +44 (0) 794 0929 447
 Email: info.ta.london@gmai.com

 www.watanzanialondon.blogspot.com

No comments: