Saturday, October 22, 2011

Mhe. Maige: Dar es salaam ni jabali lililolala

WMU AKIULIZA SWALI KWA MMOJA WA WAONYESHAJI TOKA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
  
WAJUMBE
 DT AKISISITIZA JAMBO
 WADAU WAKUBWA WA UTALII NCHINI WAKITETA NA WMU
WANAMUZIKI WA MSONDO OMARIO9KULIA) GURUMO NA WMU
..KIKUNDI CHA NGOMA CHA ASILI


HOTUBA YA MHE. EZEKIEL M. MAIGE (MB) WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII  ALIYOITOA WAKATI WA  KUADHIMISHA SIKU  YA UTALII DUNIANI  ILIYOFANYIKA  KITAIFA TAREHE 21/10/2011 - DAR ES SALAAM

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Katibu Mkuu- Wizara ya Maliasili na Utalii,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,

Kwa niaba ya Serikali napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wageni wote waalikwa kwa kuacha shughuli na ratiba zenu muhimu mno na kuitikia mwito wetu na  kujumuika pamoja nasi katika Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani. Pia shukrani zangu za kipekee ziende  kwa Kamati ya Maandalizi yenye wajumbe kutoka  Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi  zake, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Tanzania Private Sector Foundation (TPSF),  Bodi ya Utalii Dar es Salaam (DTEB), Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania (TCT) na  Halmashauri ya  Jiji la Dar es Salaam.

Nchi yetu ni mwanachama hai wa Shirika la Utalii Duniani kuanzia 1975.
Shirika la utalii Duniani limetenga siku ya tarehe 27 Septemba kila mwaka kuwa siku maalum duniani  kwa jamii ya kimataifa  katika kutafakari, kudumisha na kuchochea maendeleo ya utalii kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Kila nchi hupanga namna itakavyoadhimisha siku hiyo chini ya Kauli Mbiu itolewayo na Shirika la Utalii Duniani kila mwaka.

Mwaka 2011 kimataifa Siku ya Utalii Duniani ilisherekewa Mjini Aswan nchini Misri chini ya Kauli Mbiu isemayo Tourism Linking Cultures ikiwa na maana Utalii huunganisha Tamaduni.



Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Mabibi na Mabwana,

Kuadhimisha Siku ya Utalii Duniani chini ya Kauli mbiu isemayo Utalii huunganisha Tamaduni (Tourism- Linking Cultures) ni kutambua uwezo mkubwa wa utalii katika kuunganisha tamaduni mbali mbali. Kupitia utalii watu wenye  tamaduni  mbali mbali  husafiri kutoka maeneo mbali mbali na kukutana na watu wenye tamaduni tofauti katika maeneo waliyoyatembelea, hivyo kujenga mahusiano baina yao, hali ambayo hupelekea kuvumiliana, kuheshimiana, kuelewana na kuleta amani duniani. 

Ujumbe wa Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii Duniani  kwa siku hii maalum  ni mwito kwa wote wanaojihusisha na biashara ya utalii kuheshimu tamaduni na kuendeleza shughuli za utalii zitoazo fursa na faida kwa wanajamii.

Katika kuadhimisha siku hii nimefahamishwa kuwa yameandaliwa maonesho ya wadau mbalimbali wa sekta ya utalii ambapo  bidhaa na huduma mbalimbali za utalii zitaoneshwa.  Pia  mdahalo maalum baina ya  wadau wa sekta ya utalii umeandaliwa.

Ni imani yangu kuwa mtatumia muda huu vizuri na mtaweza kutushauri nini kifanyike, na nani, wakati gani katika kuifanya Dar es Salaam kuwa kituo cha utalii, kuendeleza utamaduni kuwa zao la utalii, kuunganisha wazalishaji wa bidhaa za utalii na walaji ili kuhakikisha kuwa utalii Tanzaina unakua na kuweza kutoa mchango mkubwa zaidi katika Pato la Taifa na kuwapatia wananchi kipato hivyo kujiondolea umaskini.

Mabibi na Mabwana,
Utalii ni miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi duniani kiuchumi, ambapo takwimu zinaonesha mwaka 2010 Idadi ya watalii duniani ilifikia 940 milioni sawa na ongezeko la asilimia 6.6 kutoka mwaka 2009. Mapato yatokanayo na utalii duniani yalifikia Dola za Kimarekani 919 milioni mwaka 2010 wakati mwaka 2009 mapato yalikuwa Dola za Kimarekani 851 milioni sawa na ongezeko la asilimia 4.7

Takwimu zinaonesha idadi ya watalii Barani  Afrika iliongezeka hasa kutokana na kuwa wenyeji wa  mashindano ya Kombe la Dunia 2010 yaliofanyika  Afrika Kusini. Idadi ya watalii ilifikiai 49 milioni mwaka 2010 ambayo ni ongezeko la asilimia 7 kutoka mwaka 2009 na mapato yatokanayo na utalii yalifikia Dola za Kimarekani 31 milioni sawa na ongezeko la asilimia 4 sawia .

Sekta ya utalii Tanzania  ni ya pili kwa ukubwa   katika kuchangia  pato la Taifa ambapo utalii unachangia asilimia 17. Takwimu zinaonesha mwaka 2010 Idadi ya watalii waliotembelea Tanzania iliongezeka kufikia watalii 782,679  wakati mapato yatokanayo na utalii yalifikia Dola za Kimarekani  1.25 Bilioni. Mwaka 2009 watalii waliotembelea Tanzania walikuwa 714,367 na waliliingizia taifa Dola za Kimarekani 1.15 Bilioni.
Utalii huchangia zaidi ya asilimia 25 kwa fedha za kigeni.

Serikali imekusudia kuongeza mchango wa utalii katika pato la taifa na katika kutoa fursa za ajira.  Mkakati mmojawapo unaotumika kama ulivyoainishwa katika Sera ya Utalii ya mwaka 1999 ni  kupanua wigo wa utalii ikiwa ni pamoja na kufungua maeneo mapya ya utalii na kuendeleza mazao mapya ya utalii hivyo kuongeza muda wa mtalii kukaa nchini na kufanya matumizi zaidi. Hii ni pamoja na kutumia  fursa nyingi tulizo nazo zikiwemo tamaduni zetu, sanaa zetu nk.

Mkoa wa Dar es salaam ndio mwenyeji wetu Mwaka huu. Ni vyema tuongeze jinsi ya kulifanya Jiji liwe kivutio cha utalii. Hivi sasa Dar es salaam ni jabali lililolala.   

Kwa mfano Jiji la London ni moja kati ya Jiji la Kimataifa kati ya Majiji 150 ambayo yanapokea Watalii mbalimbali wa Kimataifa.  Hivi sasa Jiji la London linapokea Watalii takriban m. 20 kwa mwaka.  Mji mingine ambayo hupokea watalii kwa wingi ni pamoja na  Bankok, Paris, New York na Singapore.

Majiji 150  ulimweguni huchangia theluthi ya watalii wote wanaotembea sehemu mbalimbali ulimweguni.  Mji ni kichocheo cha uchumi kwa kukuwa kwa Sekta ya Utalii ambapo fursa za uwekezaji, miundo mbinu, majengo, na usafiri wa anga ni moja ya changamoto zinazosukumwa na ukuaji  wa Sekta ya Utalii Katiaa mijini.

Miji yetu ikiwemo jiji la Dar es salaam inawezekana kuwa vivutio vikuu vya utalii na kuchangia katika kuongeza kipato na kutoa ajira kwa wakazi wake. Ili kufikia lengo hilo lazima yawekwe mazingira yatakayochochea maendeleo ya vivutio na huduma kwa watalii.

Ili watalii wakae na kutumia fedha zao lazima tuwe na sehemu mbalimbali takazowafanya wafanye hivyo. Kwa mfano tunahitaji kuwa na hoteli zenye huduma za ziada kukidhi matakwa ya watalii wa kileo. Kwa mfano tuwe na maduka bora ya zawadi na souvenir. Tunahitaji kuwa na maeneo ya wazi yenye kuwa na huduma za viwango na kwa mpangilio. Watalii wanahitaji kutembea wakiwa huru na ndani ya maeneo yaliyo safi na yenye usalama

Katika majiji mengine watalii wa ndani na wa nje hufanya burudani na kutumia fedha nyakati za jioni na usiku. Hawawezi kufanya hivyo katika mitaa iliyo na giza kwa kutokuwa na taa za barabarani. Hawataweza kufanya hivyo kama barabara zetu haziwi na maeneo ya watembea kwa miguu. Hawawezi kufanya hivyo huku wakinyemelewa na wachuuzi na vibaka.

Haya maendeleo ya huduma katika nchi za wenzetu hufanya na Halmashauri za majiji yao na huchagizwa na madiwani na mameya wao. Kwa nini Manispaa za jiji la Dar es salaam haziweki maaskari wao na mgambo kuimarisha usalama kwenye maeneo muhimu ya kitalii. Kwa nini huduma bora za vinywaji hazitolewi maeneo ya Mnazi mmoja saa za jioni huku kukiwa na ulinzi wa kutosha. Kwa nini eneo la coco beach haliendelezwi kama walivyofanya wenzetu wa Mji Mkongwe Zanzibar.  Water front za wenzetu ni maeneo makuu ya burudani na huduma za kuvinjari. Kwetu ni eneo la kutupa takataka, kuegesha magari na maficho ya vibaka. Kwa nini eneo la kuanzia fukwe iliyo mbele ya hoteli ya Kilimanjaro Hyatt hadi mbele ya posta mpya halisafishwi, kuendelezwa na kuruhusu huduma kwa watalii ili jioni watu wavinjari eneo hilo. Nafahamu Mamlaka ya Bandari wanahodhi eneo hilo na mipango ya kuliendeleza ipo kwenye michoro na makabrasha yana vumbi la zaidi ya miaka 20 bila kutekelezwa kwa sababu ya kigugumizi na maamuzi ingawa Wakurugenzi wamefanya study tour mabara yote ya ulimwengu kuona wenzetu wanafanya nini.

Kuwekeza mijini ni rahisi ikilinganishwa na mbugani. Kwa mfano ujenzi na uendeshaji wa hoteli na migahawa mijini ni rahisi ikilinganishwa na mbugani, ambapo huduma na mahitaji mbalimbali yanapatikana mbali na kusafirishwa kwa gharama. Ni changamoto kwa jiji na watu wa mipango-miji kuweka mazingira yatakayowezesha uwekezaji katika huduma za malazi na burudani. Tukifanikisha hili tutaongeza ushindani na kupunguza ughali wa huduma kwa wageni wetu. Tukifanya hivi tutapanua wigo na kupunguza utegemezi wetu kwa aina moja au mbili tu za utalii wa mbugani na kupanda mlima.

Huu ni muda wa kujirekebisha, na kujipanga ili kulifanya Jiji la Dar es salaam livutie watalii. Natoa wito kwa wadau wote wakiwemo viongozi na wanasiasa tuwe na msukumo wa kuelekea huko. Nafahamu wadau wetu wa maendeleo wapo tayari kutuunga mkono, wafanyabiashara wapo tayari kuwekeza lakini lazima tuondokane na umangimeza na tuongeze uwazi na uwajibikaji.

Kazi ya kuendeleza utalii inahitaji ushirikiano wa wadau mbali mbali kuanzia Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa ambao ndiyo wenye maeneo yenye vivutio vingi,  Serikali kuu, Sekta binafsi, jamii na watalii wenyewe. Pia vyuo na taasisi zitoazo mafunzo ya utalii na taasisi za utafiti vina mchango mkubwa katika uendelezaji utalii. Bila kusahau mchango mkubwa wa vyombo vya habari  katika kutangaza fursa na kuelimisha umma juu ya umuhimu wa utalii na namna wanavyoweza kunufaika na shughuli mbalimbali za utalii. Rai yangu kwenu leo ni kuwa mje na  maazimiao yatakayopeleka mbele utalii wetu.

Tunapoadhimisha Siku ya Utalii Duniani sambamba na miaka 50 ya uhuru, tuendelee kuitunza, kuipenda na kuijenga nchi yetu na watu wake kwa kutunza na kudumisha hazina ya utamaduni ambao ni pigo la roho ya taifa letu.

Baada ya kusema hayo nawatakia siku njema na majadiliano yenye kuzaa matunda.

Asanteni kwa kunisikiliza

No comments: