KABWE ZUBERI ZITTO, MP
KIGOMA KASKAZINI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
1. Baadhi
ya vyombo vya habari vimehusisha kauli yangu ya kutaka kupunguza umri wa
kugombea urais na mimi ‘kuutaka urais’. Mimi nikiwa mwanachama na kiongozi wa
chama chama changu cha CHADEMA naelewa na kuziheshimu taratibu na kanuni
tulizojiwekea za kuomba nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo nafasi ya urais.
Nafasi ya uongozi ndani ya CHADEMA haiombwi kwenye warsha. Iwapo chama change,
wakati muafaka ukifika na kutokana na matakwa ya jamii, kikiona nipewe jukumu
lolote sitasita kutekeleza wajibu huo niwe au nisiwe mgombea.
2. Kwa
hivyo, nilichozungumza jana ni kutoa maoni yangu kwamba muda umefika kwa Taifa
letu kupunguza umri wa kugombea urais. Maoni yangu haya yanatokana na ukweli
kwamba hakuna sababu zozote za kisayansi zinazomfanya mtu aliye chini ya umri
wa miaka 40 akose sifa za kuwa Rais. Msimamo huu nimekuwa nao tangu zamani
nikisoma shule na haujawahi kubadilika. Hakuna mahala popote katika maoni yangu
niliyotoa jana niliposema kwamba nataka umri wa urais upunguzwe ili nipate fursa
ya kugombea nafasi ya urais.
Pia siwezi kutaka katiba iandikwe kwa ajili yangu.
Vilevile kamwe isionekane kwamba matakwa ya muda mrefu ya vijana ya kutaka umri
wa kugombea Urais kupunguzwa yanalenga kunipa fursa mimi kwani mimi ni
binaadamu naweza nisiwe na sifa za kuwa Rais lakini kukawa na vijana wengine
wengi wenye umri chini ya miaka 40 wenye Uwezo na Uzalendo wa kutosha kushika
usukani wa nchi yetu. Ni maoni yangu kwamba tupate mabadiliko ya vizazi katika
uongozi wa nchi yetu ili kukabili changamoto za sasa zinazokabili Taifa letu.
3. Tunapojiandaa
kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya ni vizuri vyombo vya habari vikajikita kutoa
taarifa bila kuweka tafsiri au kuwatafasiria maoni ambayo wananchi na viongozi
watakuwa wanayatoa kuhusu maudhui ya Katiba Mpya.
Dar
es Salaam
29
Februari 2012
No comments:
Post a Comment