Wednesday, June 27, 2012

DK. ULIMBOKA NUSURA KUUAWA!

Mweneyikiti wa Jumuia ya Madaktari nchini Dk Stephen Ulimboka, amepigwa na kujeruhiwa vibaya na watu wasiofahamika.

Dkt Ulimboka anadaiwa kuvunjwa mbavu, miguu yote miwili, kung’olewa meno yote ya mbele na kuumizwa vibaya katika sehemu mbalimbali za mwili wake.

Tukio hilo la kikatili na kusikitisha limetokea usiku wa kuamkia leo jijini Dar es Salaam, na linadaiwa kufanywa na watu wa sio julikana ambapo kabla ya kufanya unyama huo walidaiwa kumteka na kumpiga kabla ya kumtelekeza katika eneo la msitu wa Pande Mabwepande.

DKT. ULIMBOKA ASIMULIA TUKIO
Akisumulia tukio hilo Dkt Ulimboka alisema kuwa  jana usiku alipigiwa simu na mtu aliyejitambulusha kwake kuwa anaitwa Hemed, aliyemwambia kuwa anahitaji kuongea naye, na ndipo walipopanga kuonana katika eneo la Leaders Kinondoni.

Dk Ulimboka aliyekuwa akiongea kwa tabu, aliendelea kusimulia kuwa wakati akiongea na mtu huyo anayekiri kuwa alikuwa akifahamiana naye kabla, alikuwa na wasiwasi kwani kila mara alikuwa akipokea simu na kuwasiliana na watu wengine ambao hawakuwapo eneo hilo.

Alisema baada ya muda alishangaa kuona wanaongezeka watu wengine watano wakiwa na silaha, kisha wakamwambia kuwa anahitajika kituo cha Polisi na kumvuta na kumuangusha barabarani kabla ya kumuingiza katika gari lenye rangi nyeusi na kuondoka naye.

Dkt Ulimboka alisema kuwa wakiwa njiani walimpiga, na kumfikisha katika msitu huo wa pande na kuendelea kumpiga paka alipoteza fahamu.

MADAKTARI NAO WALONGA
Akisimulia mkasa huo mmoja wa madaktari wenzie aliyefahamika kwa jina moja la Dkt Deo, alisema kuwa alipigiwa simu na mtu hasiyemfahamu na kumfahamisha tukio hilo.

Alisema alipofika katika kituo cha Polisi cha Bunju, alimkuta akiwa katika hali mbaya na ilikuwa ngumu kumtambua kwakuwa alikuwa na majeraha mengi eneo la usoni.

Aliongeza kuwa akiwa na wenzie waliamua kumchukua na kumkimbiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwaajili ya matibabu.

"Hali yake kwakweli ni mbaya sana, amepigwa mno na ameumizwa kwakweli tumemleta hapa hili aweze kupata matibabu, lakini mimi nilivyomkuta mara ya kwanza nilishindwa hata kumtambua kwa jinsi alivyokuwa ameumizwa"alisema Dkt Deo

Alisema kuwa alisimuliwa na Dkt Ulimboka kwamba watu hao waliomteka na kumpiga walikuwa na silaha na kwamba alishindwa kuwatambua.

Aliongeza kuwa Dkt Ulimboka alidai kuwa wakati akiwa katika halimbaya alikuwa akisikia mazungumzo yao, wakibishana juu ya kumuua wengine wakisisitiza achomwe sindano, na wengine wakitaka kumpiga risasi.

Alisema wakati mabishano yakiendelea kati yao, Dkt Ulimboka aliinuka akiwa na lengo la kukimbia lakini watu hao walipiga risasi hewani iliyomshtua na kuangua chini.

Kwa upande wake Dkt Cathbeth Mcharo ambaye ndiye aliyempokea Dkt Ulimboka Hospitalini hapo, alisema kuwa hali yake ni mbaya na kwamba wanajitahidi kumpatia huduma za haraka.

Alisema kuwa kwa hatua za awali amefanyiwa vipimo mbalimbali, hili iweze kufahamika aina ya matibabu anayotakiwa kupatiwa.

POLISI
Kamanda wa polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam Kamanda Suleiman Kova amezungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo la utekaji nyara na kujeruhi lililompata kiongozi mgomo wa Madaktari Steven Ulimboka anayedaiwa kutekwa na watu watano wakati akipata kinwaji katika klabu ya Leaders Kiondoni jijini Dar es salaam.

Kamanda Kova amesema Ulimboka aliokotwa na msamaria mwema ambaye hakutaka kumtaja jina lake kiusalama na kutoharibu upelelezi kuwa msamaria mwema huyo alimuokota Ulimboka katika msitu wa Mabwepande na kutoa taarifa kituo cha polisi cha Bunju, ambapo polisi aliyekuwa zamu alichukua maelezo yake na baadae Steven Ulimboka kuletwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Kamanda Kova amesema jeshi la Polisi Kanda Maalum limeunda jopo maalum kwa ajili ya uchunguzi na upelelezi wa tukio hilo la utekaji nyara, kwani ni tukio la kwanza kutoke nchini, ameongeza kwamba wahusika wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo wachukuliwa hatua za kisheria na sheria itafuata mkondo wake ili kukomesha matukio mengine kama hayo

MUHIMBILI
Wakati hayo yakitokea inadaiwa kuwa Askari Kanzu mmoja alikumbana na kipigo kikali kutoka kwa madaktari hapo Muhimbili kwa kile kilochodaiwa kutambuliwa na Dkt Ulimboka kuwa mmoja wa watu walio mjeruhi.

Pia inadaiwa kuwa Askari huyo aliingia chooni na kufanya mawasiliano na wenzake huku Madaktari hao wakimsikiliza na kutokana na alichokua akiongea chooni humo ndipo alipotoka aliambulia kichapo kikali.

Pia baadhi ya madkatari na wauguzi walikuwa wakisukuma gari alilokuwa amepanda Dkt Ulimboka huku wakiimba nyimbo za Umoja na Mshikamano Daima miongoni mwao.

Hali ya ulinzi ilikuwa kali Hospitalini hapo kwani Picha zilikuwa haziruhusiwi kupigwa.
Source Father Kidevu Blog

No comments: