Ndugu zangu,
Imekuwa ni utamaduni wangu kutuma salamu
za Mwaka Mpya kwa wanakijiji wa Mjengwablog, marafiki zangu kwenye FB
na wengine walio ndani na nje ya mitandao ya kijamii.
Nimefanya hivyo tangu mwaka 2006
ilipoanzishwa Mjengwablog.
Na mwaka huu naendeleza utamaduni huo. Nina mambo makubwa mawili kwenye
salamu za mwaka huu, lakini, nitaanza salamu hizi kwa kukumbushua ahadi
muhimu ya Mwana –TANU; kwamba;
” Nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa manufaa ya wote”.
Ndugu zangu,
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita nilikuwa ndani ya garimoshi la Tazara nikielekea Dar kutokea kijijini kwetu Nyeregete.
Nikiwa Nyeregete kwenye likizo ndefu ya
kusubiri matokeo ya Kidato cha Nne, zilinifikia taarifa kuwa nahitajika
haraka Dar es salaam kwenda kufanya maandalizi ya kuanza Kidato cha
Kwanza shule ya Sekondari Tambaza. Masomo yetu pale Tambaza yalianza
Januari 13, 1983.
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita
nilivuka kwa kuogelea korongo la Lihamile ili kuifikia Rujewa na
hatimaye stesheni ya Tazara kule Ihanga. Korongo hilo lilijaa maji ya
mvua ya masika yaliyokuwa yakipita kwa kasi.
Hakukuwa na daraja.
Baadae likajengwa daraja la magogo wakati wa kipindi cha Ubunge wa
Kanali Mstaafu, Edmund Mjengwa. Daraja hilo sasa limeoza. Halipitiki.
Ahadi nyingi zimetolewa kulijenga upya. Zimebaki kuwa ahadi.
Ni daraja muhimu kiuchumi na kijamii kwa watu wa Nyeregete na wengine
wengi wenye kulitumia. Ni kero kubwa kwa wananchi wa Nyeregete.
Nimeongea na baadhi ya viongozi wa
Nyeregete. Na nimewaambia, kuwa tushirikiane kuhakikisha, kuwa mwaka
2013 daraja hizo linajengwa hata kama ni kwa nguvu za wananchi. Tayari
tumeshafanya utafiti na kuona inawezekana likajengwa kwa kiwango cha
zege na chini ya shilingi milioni 20.
Hivyo basi, mwaka 2013 nitashirikiana na
wananchi wa Nyeregete na wengine wote watakaokuwa tayari kusaidia
kuhakikisha tunapitisha harambee ya kujenga daraja hilo. Miaka 30 baada
ya mimi kuvuka Lihamile kwa kuogelea itakuwa ni aibu kubwa kuwaona tena
wananchi wa Nyeregete na wengine wakivuka korongo hilo kwa kuogelea. Ni
nini basi maana ya kwenda shule?
Ndugu zangu,
Maji ni kero kubwa kwa wananchi wengi wa Bonde la Usangu, Mbarali Mbeya.
Badala tu ya kuilalamikia na kuisubiri
Serikali iwasaidie wananchi kutatua kero ya maji, mwaka 2013 nimeazimia
nitashirikiana na wanakijiji wa vijiji vya Magwalisi na Lihamile
wilayani Mbarali ili tuweze kuchangisha fedha za kuchimba visima vya
pampu kimoja katika kila kijiji husika.
Nitashiriki kuchangisha sehemu ya fedha
zinazohitajika kugharamia visima hivyo kwa kupanda Mlima Kilimanjaro,
kitu ambacho nimependa nikifanye katika maisha yangu lakini sijapata
bahati ya kufanya.
Ndugu zangu,
Hayo ni mawili makubwa niliyotaka kuyasema kupitia salamu za mwaka mpya wa 2013.
Ni matumaini yangu, Desemba 31, 2013
Mungu atanijalia uhai na kurudi tena hapa kutoa tena salamu za mwaka
mpya huku hayo mawili yakiwa tayari yameshafanyiwa kazi kwa nguvu za
pamoja, ikiwamo ushirikiano wenu.
Nawatakia Heri na Fanaka Za Mwaka Mpya wa 2013.
Maggid Mjengwa,
Morogoro
http://mjengwablog.com
No comments:
Post a Comment