Monday, July 28, 2014

SHIRIKA LA NYUMBA NHC LAENDELEA KUONGEZA AJIRA KWA VIJANA

1
Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa Bi Rachel Kasanda akikabidhi mashine za kufyatulia matofali kwa Hassan Soud Katibu wa kikundi cha Changamoto kwa niaba ya vikundi vingine vya wilaya ya Ilala ambazo zimetolewa na shirika la Nyumba nchini NHC jana wakati wa mpokezi ya Mwenge wa Uhuru Ilala Boma mara baada ya Meneja wa Shirika hilo wilaya ya Ilala Bw. Jackson Maagi kumkabidhi kiongozi huyo wa mbio za mwenge ikiwa ni juhudi za shirika hilo kusaidia kupunguza uhaba wa ajira kwa vijana ili waweze kujiajiri kwa kuyatua matofali na kuuza.
3
Askari wa Kikosi cha FFU wakiulinda mwenge mara baada ya kuwasili Ilala Boma mahali ambapo ndiyo kituo ulipolala mwenge huo.
4
Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC Bw. Jackson Maagi wa pili kutoka kushoto akiwa pamoja na wafanyakazi wnzake kabla ya kukabidhi mashinne hizo jana.
2
Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC Bw. Jackson Maagi akizungumza wakati wa kukabidhi mashine hizo jana
............................................................................................
HOTUBA FUPI YA MENEJA WA NHC ILALA KWA KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA
Ndugu kiongozi wa Mbio za mwenge, Ninayo furaha kubwa sana kusimama mbele yenu na kuongea nanyi kama mwakilishi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa.
Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge; Shirika la Nyumba la Taifa lina mpango mkakati wake wa miaka mitano ambao moja ya malengo yake sita makuu ni kuboresha taswira ya Shirika. Katika utekelezaji wa lengo hili, Shirika lina sera ya huduma kwa jamii ambayo imejikita katika kusaidia vijana kujiajiri. Ili kuwezesha vijana kujiajiri, Shirika limeamua kuzisaidia Halmashauri za Miji na Wilaya kote nchini mashine za kuwezesha vikundi vya vijana kutengeneza matofali ya kujengea nyumba. Nchi yetu ina Halmashauri 160 na kila Halmashauri itapewa mashine 4 kwa ajili ya kusaidia vikundi vya vijana. Katika mpango huu jumla ya mashine 640 zitatolewa na Shirika na kugharimu shilingi 288,000,000/. Aidha, kila Halmashauri itapatiwa shilingi laki tano (500,000/=) kama mtaji kwa vijana kuanzia shughuli yao ya kutengeneza matofali. Kadhalika, Shirika limegharamia shilingi 800,000/= kwa kila Halmashauri kwa ajili ya kuwalipa wakufunzi kutoka VETA wanaotoa maelekezo kwa vijana namna ya kutumia mashine hizo. Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge,katika kutekeleza mradi huu jumla ya shilingi milioni mia saba (700,000,000/=) zitatumika. Aidha, tunatarajia kuwa ajira zaidi ya 8,000 za moja kwa moja na ajira nyingine zaidi ya 200,000 zisizo za moja kwa moja zitapatikana. Katika mpango huu kila Wilaya inatakiwa kuwa na vijana 40 watakaokuwa katika vikundi vya watu 10 kila kimoja. Msaada huu ni mkubwa lakini kutokana na ukubwa wa tatizo la ajira jitihada zaidi kutoka kwa wadau mbalimbali zinatakiwa. Ni matarajio yetu kuwa taasisi nyingine ama mtu mmoja mmoja atashiriki kukwamua vijana hawa. Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge, kupitia maadhimisho haya, Shirika linatoa mashine nne (4) kwa vikundi 4 vya vijana vilivyoundwa katika wilaya ya Ilala ambapo kila kikundi kina jumla ya vijana10 watakaotumia mashine moja. Hivyo jumla ya vijana 40 katika Wilaya hii watapata ajira kutokana na mashine hizi. Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge, mwisho Shirika linatoa rai kwa Taasisi za serikali, mashirika ya umma, binafsi na watu mbalimbali, kuunga mkono juhudi za Serikali za kupunguza tatizo la ajira kwa vijana. Ni matumaini yetu kuwa tutawaunga mkono kwa kununua matofali yao ama kusaidia upatikanaji wa mashine nyingine zaidi ili wengine ambao hawajafikiwa na mradi huu wafikiwe na wapate kufaidika. Kipekee tunaomba Serikali za Mitaa (kwa maana ya Halmashauri zetu za wilaya, miji, manispaa ama jiji) wawe ni wanunuzi wakuu wa matofali yatakayotengenezwa na vikundi hivi vya vijana ambayo ni ya gharama nafuu ili kusaidia miradi mbalimbali ya ujenzi na kuwaongezea kipato chao. Tunawaomba pia msaidie kusimamia mradi huu ili uweze kuwa endelevu.

No comments: