Saturday, December 6, 2014

MAONYESHO YA KIMATAIFA YA ELIMU KUANZA DISEMBA 17-21, 2014 JIJINI DAR

Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Abdulimalik Mollel, akisisitiza jambo kwa wanahabari (hawapo pichani)
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Kampuni ya Global Education Link (GEL) kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Wizara ya Elimu na Ufundi pamoja na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) wameandaa maonyesho ya kwanza ya kimataifa ya elimu (TIEE) yanayotarajiwa kufanyika Disemba 17 hadi  21 mwaka huu katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Global link Education, Abdulmalik Mollel, alisema lengo la maonyesho hayo ni kutambulisha wadau wa elimu kwa pamoja ili kuweza kutoa huduma ya pamoja kwa wananchi na kuwaelimisha juu ya mambo muhimu yaliyopo katika kila sekta.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan Tred), Jacqueline Mneney, akizungumza jambo.
Alisema ushiriki wa asasi mbalimbali kwa kushirikiana na sekta binafsi utakuwa na chachu ya mabadiliko ya elimu kwa kupitia mpango wa matokeo makubwa sasa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Jacqueline Mneney, alisema wakati umefika kwa Watanzania kujua umuhimu wa maonyesho ya Elimu maana yamekuja kutatua matatizo mbali mbali waliyokuwa wakiyapata wazazi pindi wanapokuwa wanawatafutia shule na vyuo watoto wao.
Aidha alisema maonyesho hayo yataleta manufaa makubwa na changamoto chanya hasa katika kuongeza ushindani katika sekta ya elimu ambayo itasaidia mpango wa matokeo makubwa sasa.
Maonesho hayo yanatarajiwa kupata washiriki zaidi ya 500 na wananchi mbalimbali zaidi ya 350,000 kutoka ndani na nje ya nchi.
Kauli mbiu ya maonesho hayo ni ‘KUWEKA JITIHADA ZA PAMOJA KATIKA KUBORESHA MFUMO WA ELIMU TANZANIA NI NJIA THABITI YA KULETA MAENDELEO ENDELEVU KATIKA TAIFA.’

No comments: