Monday, July 27, 2015

MATUKIO MAKUBWA YA MUZIKI WA DANSI NCHINI KWA NUSU YA KWANZA YA MWAKA 2015…




 By Willliam Kaijage
UTANGULIZI (PREAMBLE)
Mwanzoni mwa mwezi wa 7 ndio nusu ya mwaka. Zinakuwa zimepita siku 182 (au 183 kwa mwaka mrefu) na kubaki siku 182.
Yafuatayo ni matukio makubwa ya muziki wa dansi kwa nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2015


BENDI MPYA
Tarehe 31-Jan-2015, BMM Classic Band, ilizinduliwa katika ukumbi wa BMM Mwenge, opposite TRA.
Tarehe 21-Feb-2015,  JJ Band yazinduliwa katika ukumbi wa. JJ Band ni bendi dada ya Skylight Band itakayokuwa inatumbuiza mjini Mwanza katika hotel ya Jembe ni Jembe Resort.
 Tarehe 06-Mar-2015 (Ijumaa), Ruby Band ilitambulishwa rasmi katika ukumbi wa Coco Beach Pub ambapo pia ilizindua video ya wimbo mpya wa “Noma”.
Tarehe 18-Jul-2015 (Jumamosi), Stars Band yazinduliwa katika ukumbi wa Mzalendo Pub. Bendi hiyo inaongozwa na mwanamuziki Aneth Kushaba aka “AK47” aliyekuwa Skylight Band. Meneja wa bendi ni mpiga drums James Kibosho.

UZINDUZI WA ALBUM MPYA
Mpaka sasa (zaidi ya nusu mwaka) hakuna album yoyote mpya hata moja iliyozinduliwa.

KILI MUSIC AWARD
Tarehe 23-Mar-2015, Kililimanjaro Music Award 2015 yazinduliwa rasmi
Tarehe 25-Apr-2015, Academy ya Kili Music Award yakutana kuchagua majina ya washiriki wa kila kipengele.
Tarehe 29-Apr-2015, majina ya washiriki wa kila kipengele yatangazwa rasmi
Tarehe 13-Jun-2015 (Jumamosi), sherehe za washindi wa Kili Music Award 2015 zilifanyika katika ukumbi wa Mlimani City. Kulikuwa na jumla ya vipengele (categories) 6  vya muziki wa dansi. Washindi walikuwa kama ifuatavyo;
1. Bendi Bora ya Mwaka- FM Academia
2. Mtunzi Bora wa Mwaka Bendi-Jose Mara (Mapacha Watatu)
3. Rapa Bora wa Mwaka Bendi- Fergusson (Mashujaa Band)
4. Wimbo wa Kiswahili Bendi- ”Wale Wale” (Vijana Ngwasuma)
5. Mwimbaji Bora wa Kiume Bendi- Jose Mara (Mapacha Watatu)
6. Mtayarishaji Bora wa Nyimbo Bendi-Amoroso Sound

NB: Mwaka huu hakukuwa na Mwimbaji Bora wa Kike Bendi

WANAMUZIKI WALIOFARIKI
Tarehe 04-Jan-2015 (Jumapili), mwanamuziki wa Flowin aka “Kachumbari” aliyekuwa mpiga drums na tumba wa Chuchu Sound afariki dunia.
Tarehe 30-Jan-2015, mwanamuziki Peter Kanuti afariki dunia kwa ajali ya gari akiwa Zanzibar. Huyu anatokea familia ya wanamuziki Gaspar Kanuti, Fred Kanuti na Joseph Kanuti.
Tarehe 28-Feb-2015, mwanamuziki, mwanasiasa, mwanajeshi mstaafu, mbunge wa jimbo la Mbinga Magharibi, Mkurugenzi wa kundi la sanaa za maonesho la Tanzania One Theatre (TOT Plus) Captain John Damian Komba afariki dunia
Tarehe 16-Apr-2015, mwanamuziki Joseph Chigwele “Che” Mundugwao afarikia dunia.
Mwanamuziki Mutombo Lufungula “Audax” mmoja ya waanzilishi na wamiliki wa bendi ya Maquis du Zaire (ambayo baadaye ikaitwa Maquis Original) afariki dunia alfajiri ya alhamis tarehe 23-Apr-2015 na kuzikwa Jumapili ya tarehe 26-Apr-2015 katika makaburi ya Kinondoni.
Tarehe 17-Jul-2015 (Ijumaa), mwanamuziki Ramadhan Ally Masanja aka “Banza Stone” afariki dunia siku ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. Azikwa Jumamosi tarehe 18-Jul-2015 sikuu kuu ya Idd Mosi (Eid al Fitr) katika makaburi ya Sinza.

MATUKIO MENGINE MAKUBWA
Tarehe 18-Jan-2015 (Jumapili), Ali Choki apanda jukwaa la Twanga Pepeta siku Twanga walipokuwa wakitumbuiza Leaders Club na kusalimia kisanii. Tukio hili halijawahi kutokea tangu Ali Choki alipohama Twanga Pepeta mwaka 2008 na kwenda kujiunga na TOT Plus.
Ndani ya siku 3 kuanzia 24-26 January 2015, Wadau wa Muziki wa dansi chini ya uratibu wa admin wa BONGO DANSI Deo Mutta Mwanatanga wafanikisha harambee na zoezi la kumrudisha Dar-es-Salaam mwanamuziki Banza Stone aliyekuwa amekwama mjini Tunduma huku akiwa anaumwa baada ya matatizo yaliyoitokea bendi ya Rungwe aliyoenda nayo huko.
Tarehe 24-Jan-2015 (Jumamosi), tamasha linaloitwa TIGO KIBOKO YAO Concert lafanyika Leaders Club. Bendi za muziki wa dansi zilizoshiriki ni Msondo Ngoma, Mlimani Park Orchestra, Christian Bella & Malaika Music Band, Yamoto Band. Kila bendi ilipiga kwa dakika 45.
Tarehe 25-Jan-2015 (Jumapili), tamasha la miaka 10 ya CDS lafanyika TCC Chang’ombe na kushirikisha bendi za muziki wa dansi za Msondo Ngoma, Mapacha Watatu, Malaika Music Band na FM Academia. Kuna uwezekano tamasha hili likawa linafanyika kila mwaka.
Tarehe 30-Jan-2015, Ali Choki na Mama Asha Baraka wapatanishwa rasmi chini ya usuluhishi uliofanywa na Global Publisher.
Tarehe 07-Feb-2015 (Jumamosi), tukio la “Miaka 16 ya Luizer Mbutu” ndani ya Twanga Pepeta lafanyika Mango Garden.
Tarehe 28-Mar-2015 (Jumamosi), wafanyika mpambano kati ya FM Academia na Twanga Pepeta katika ukumbi wa Escape One.
Tarehe 08-Apr-2015, Ally Choki na Super Nyamwela watangazwa rasmi kujiunga (kurejea) Twanga.
Tarehe 18-Apr-2015 (Jumamosi), Christian Bella afanya tukio la “Usiku wa Masauti” ndani ya ukumbi wa Escape One. Christian Bella atumia tukio hilo kutambulisha/kuzindua audio na video ya wimbo wake mpya wa “Nashindwa”.
Tarehe 25-Apr-2015 (Jumamosi), show ya kwanza ya Ally Choki na Super Nyamwela baada ya kurejea Twanga Pepeta yafanyika Mango Garden.
Tarehe 25-Apr-2015 (Jumamosi), kundi la Les Wanyika kutoka Kenya latumbuiza katika kiwanja cha Escape One.
Tarehe 26-Apr-2015, Bendi ya Cuban Marimba watunukiwa nishani ya Muungano kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete katika sherehe zilizofanyika katika viwanja vya ikulu. Waliopokea nishani kwa niaba ya bendi ni Waziri Nyange (mpiga solo) na Mzee Juma Sangura (mpiga bass).
Tarehe 08-May-2015 (Ijumaa), Mashujaa Group wazindua ukumbi wao wa Mashujaa Lounge ambao zamani ulikuwa unaitwa Business Park uliopo maeneo ya Victoria, Dar-es-Salaam. Katika tukio hilo, Mashujaa Band imetumia nafasi hiyo pia kutambulisha wanamuziki wawili wapya Roggart Hegga Katapila na Dady Dipirone “Rais wa Masauti ya Chini”. Pia Mashujaa Band walitambulisha nyimbo 2 mpya. Ikumbukwe pia kuwa Mashujaa Group mwaka huu wamefanikiwa kuanzisha radio ya Mashujaa FM mkoani Lindi.
Tarehe 24-Jun-2015, mwanamuziki Ramadhan Masanja aka “Banza Stone” alizushiwa kifo baada ya kuumwa muda mrefu. Hii ni moja ya mara nyingi sana mwanamuziki huyo kuzushiwa kifo.
Tarehe 18-Jul-2015 (Jumamosi), mpambano wa Msondo na Sikinde wafanyika siku ya Idd Mosi (Eid al Fitr) katika ukumbi wa TCC Chang’ombe kwa kuandaliwa na Fred Ogot na kampuni yake ya Bob Entertainment.

No comments: