Tuesday, November 17, 2015

JIJI LA MBEYA HATARI KUKUMBWA NA UGONJWA WA KIPINDUPINDU


Wafanyabiashara ndogo ndogo katika eneo la Makunguru jijini Mbeya wakiendelea na shughuli zao kama kawaida .



Na Mwandishi wetu,Mbeya

Halmashauri ya jiji la Mbeya limewataka wafanyabiashara ndogondogo hususani wa chakula  kujijengea tabia ya kuchoma taka nyakati za jioni mara wamalizapo kuuza biashara zao na si kusubili gari ya taka kuja kuzoa.



Aidha imewataka  wakazi hao kuondokana na fikra duni  ya kuamini kuwa kazi ya uzoaji wa taka na kusafisha mazingira ni ya halmashauri ya Jiji na sio mali ya mtu.



Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji la Mbeya, Dkt. Samweli Lazaro, amesema, wananchi wanatakiwa kujenga tabia ya usafi na sio kusubili kupigizana kelele na serikali kwa kuwahimiza kufanya usafi kwani adui mkubwa wa afya ni uchafu hivyo kila mmoja anapaswa kuwa mlinzi wa mwezake katika kutunza mazingira.



Hali hiyo imesababisha kuwepo kwa malimbikizo mengi ya taka  kwenye sehemu zisizorasmi  ndani ya JIji la Mbeya na kupelekea jiji hilo kuwa chafu hususani katika maeneo ya  sokoni.



Amesema, hivi sasa halmashauri ilianzisha mpango wa uzoaji wa taka barabarani ambapo mpango huo umeonekana  kupokelewa na wananchi kwa asilimia 100 changamoto inakuja kwa upande wa halmashauri kuonekana kuzidiwa kutokana na ukosefu wa vitendea kazi.



“Halmashauri ilianzisha zoezi la kupitia taka zinazozalishwa na wananchi ambazo huziweka barabarani na magari yanapitia lakini mapango huu umeonekana kuzaa matunda kwa jamii kuupokea lakini tatizo ni uhaba wa vitendea kazi,”alisema.



Alisema, ili zoezi hilo lifanikiwe halmashauri inahitaji zaidi ya gari saba za ubebaji taka na kontena 80 lakini mpaka sasa magari yaliyopo ni manne na kontena 30 .



Hata hivyo kutokana na changamoto hiyo, Lazaro anawasihi wananchi kujenga tabia ya kuweka mazingira safi hasa kipindi hiki cha mvua kwani ndipo magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu yanapoibuka na kusababisha vifo vya watu.



Mwisho.



JAMIIMOJABLOG MBEYA

No comments: