Tuesday, November 17, 2015

Chonde Spika Mtarajiwa Ndugai; Usianze Kwa Kufufua Mjadala Uliouzika Mwaka 2012; Ni Wa Nyongeza Za Posho Za Wabunge..

Ndugu zangu,
Hata baada ya kumpongeza Spika mtarajiwa Job Ndugai kwa kupitishwa na chama chake kuwania Uspika, nataka niwe miongoni mwa wa mwanzoni kumtahadharisha Job Ndugai na kile ambacho baadhi ya Wabunge watapenda kusikia kutoka kwake. Ni heri achague kuchukiwa na wabunge kwa kuwaambia ukweli kuliko kuchagua kupendwa kwa gharama za wanyonge walio wengi. Watanzania katika hali ngumu ya kiuchumi kwa sasa, hawatarajii kabisa kusikia habari za Wabunge kuongezewa posho na marupurupu mengine, badala yake mijadala ya walau kupunguza posho zao za vikao ili fedha zitakazopatikana ziende kuboresha huduma muhimu za kijamii kama vile afya na elimu.
Na hapa nitamkumbusha Job Ndugai alichokisema mwaka 2012. Kwenye gazeti Uhuru Jumanne, Februari 7, 2012, limebeba habari hiyo kwenye ukurasa wa kwanza.
Mwandishi Lilian Timbuka akiripoti kutoka Dodoma alimnukuu Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai akitamka; ” Nyongeza ya posho ya vikao vya bunge sasa haitalipwa mpaka hapo Ofisi ya Rais, Ikulu, itakapotamka vinginevyo. Kwa kuwa Rais ndiye mwenye mamlaka ya kuidhinisha vibali vya nyongeza za malipo kwa wabunge, ikiwemo posho na hajatoa kibali, hivyo haina haja ya kuendeleza mjadala kuhusu hoja hiyo”- Job Ndugai, Uhuru, Jumanne, Februari 7, 2012.
Maggid,
Dar es Salaam.

No comments: