Wednesday, May 11, 2016

SERIKALI MKOANI MBEYA YAFUTA HATI YA KIWANJA CHA MAKAZI KILICHOTOLEWA NA HALMASHAURI YA JIJI LA MBEYA.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amosi Makala (Picha Maktaba)


Na EmanuelMadafa,Mbeya(Jamiimojablogu)
SERIKALI Mkoani Mbeya  imeagiza kufutwa kwa hati ya  kiwanja kilichotolewa na halmashauri ya Jiji la Mbeya kwenye chanzo kikuu cha maji kilichopo eneo la Nyibuko kata ya Mwakibete kwa matumizi ya makazi.

Agizo hilo, limetolwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makala mara baada ya kutembelea na kukagua chanzo kikuu cha maji cha Nzovwe, chenye uwezo wa kuzalisha mita 12 za ujazo kwa siku na kusambaza maji kwa asilimia 41 kwa wakazi wa jiji la Mbeya wapatao zaidi ya  200,000.

Kiwanja hicho ambacho kipo karibu na eneo la chanzo cha maji cha Nzovwe, kilitolewa na maafisa ardhi, idara ya mipango miji kwa ajili ya matumizi ya makazi na kumilikiwa na mtu binafsi aliyetajwa kwa jina moja la Mwakasala.

Makala amesema, chanzo hicho cha maji ndio tegemezi kwa kusambaza huduma ya maji kwa wananchi wa Jiji la Mbeya, hivyo kama kitaachwa na kuharibiwa, wananchi zaidi ya 200,000 wapo hatarini kuikosa huduma hiyo ambayo ni haki yao ya msingi.

 Mkuu huyo wa Mkoa amesema Serikali iliwaondoa wananchi wote waliokuwa wanaishi au kuendesha shughuli zao za kiuchumi ndani ya mita 60 na kuwalipa fidia zao hivyo hatua ya wananchi hao kuendelea kuishia mahali hapo ni kukaidi agizo la serikali.

 Amebainisha kuwa kiwango  kikubwa cha upotevu wa maji kwa asilimia 31  inatokana na baadhi ya vyanzo vya maji kuharibiwa kwa kufanyika kwa shughuli za kibinadamu, kulisha mifugo au kujenga nyumba za makazi pamoja na mabadiliko ya kihaidrolojia.

Hata hivyo, Mkuu huyo aliutaka uongozi wa mamlaka ya maji kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji la Mbeya, kuhakikisha wanalisiamamia zoezi hilo la kumondoa mvamizi huyo ndani ya siku tatu.
“Wananchi wengine wameondoka tena kwa hiari yao wenyewe, sasa kwa nini huyu atuchezee mchezo mchafu?.. kwa hili sikubaliani nalo, huku akiwataka wananchi ambao ni vijana kulilinda eneo hilo na kuwaonya wale ambao watakubali kutumiwa na mtu au watu kufanya fujo,”alisema.
Mwisho.

No comments: