Thursday, November 17, 2016

BANK OF AFRICA - TANZANIA (BOA) YAZINDUA PROGRAMU MPYA YA MIKOPO YA UJENZI WA NYUMBA ‘WEZESHA’

Kutoka kushoto ni Ibrahim Samuel- Meneja Uhusiano- Mikopo ya Nyumba, Wasia Mushi- Naibu Mkurugenzi Benki ya Afrika Tanzania (BOA), na Muganyizi Bisheko- Meneja Masoko Utafiti na Maendeleo wakiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani).

Kutoka kushoto ni Beatrice Mirigo- Marketing executive, Ibrahim Samuel- Meneja Uhusiano- Mikopo ya Nyumba, na Wasia Mushi- Naibu Mkurugenzi Benki ya Afrika Tanzania (BOA) wakiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani).


BANK OF AFRICA- TANZANIA leo imezindua aina mpya ya mkopo wa ujenzi wa nyumba unaoitwa ‘WEZESHA’ ambapo mtu anaweza kukopa kiasi cha shilingi milioni 40 hadi 500 kwa mrejesho wa miaka hadi 25 bila utaratibu wa kutoa malipo yoyote ya awali.

Akizungumzia progamu hiyo, Naibu Mkurugenzi wa BANK OF AFRICA- TANZANIA bwana Wasia Mushi alisema, ‘programu hii ya mkopo wa ujenzi wa makazi mapya unawapa uwezo wateja wetu kubuni nyumba zao kadiri wanavyopenda, kulingana na mahitaji yao na ndani ya bajeti zao. Kwa kiwango kidogo kabisa cha riba na katika viwango vya punguzo, Bank ya Afrika pia imetengeneza mazingira rafiki na kuondoa usumbufu kwa mteja pindi anapohitaji mkopo huu’

Aidha, huduma ya mkopo ya ‘Wezesha’ inapatikana kwa watu wote wenye mishahara katika sekta za umma na binafsi, na kwa kutoa muda wa miaka 25 ya kulipa deni, mkopaji atapata uhuru zaidi pindi atakapochukua mkopo.

Mpango wa huu wa ‘Wezesha’ kujenga makazi unalenga kutoa suluhu kwa changamoto za makazi zinazowakabili watanzania wengi ambao kwa mazingira ya kawaida hutumia zaidi ya miaka 10-15 kujenga nyumba ya kawaida ya kuishi.

Fursa hii ya kutatua changamoto ya makazi kwa watanzania wengi, inaendana na ongezeko kubwa la watu kupata ardhi iliyopimwa, hivyo kuwapa watu nafasi ya kujenga nyumba wanazozitaka kwa masharti nafuu na rahisi ambapo kwa kuanzia mteja atatakiwa kuwa na kiwanja ambacho nyumba hiyo itajengwa.

Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania ina uhaba wa nyumba kwa ajili ya makazi zaidi ya 3,000,000. Huku kukiwa na ongezeko la uhitaji huo kwa zaidi ya asilimia 1 kila mwezi.

Muganyizi Bisheko, Meneja Masoko Utafiti na Maendeleo wa BANK OF AFRICA-TANZANIA aliongeza kuwa, ‘Benki inatoa asilimia 100 ya ufadhili wa ujenzi ili watu wengi waweze kuumudu mkopo. Mara nyingi, hasa kwa mtu anayeanza maisha, kujiwekea akiba na kupata kiwango cha kulipia gharama za ujenzi wa makazi ni jambo gumu sana. Jambo hilo liliwezekana kwa wale wenye kipato kikubwa na endelevu, lakini kwa sasa, na kwa uwepo wa WEZESHA, si jambo gumu tena la kuchelewesha ndoto zako za kumiliki makazi ya kuishi, kwa kuweka akiba kwa miaka 2-5’

Aliongeza kuwa, ‘Mara mteja wetu anapopata mkopo wa makazi, yeye ndiye atachagua mkandarasi wa kujenga nyumba yake miongoni mwa makandarasi waliochaguliwa na BANK OF AFRICA- TANZANIA. Mkopo utatolewa kulingana na hatua za ujenzi, kama vile msingi, boma, paa, na umaliziaji. Na fedha hizo zitapelekwa kwenye akaunti ya Kandarasi anayejenga iliyofunguliwa kwenye Benki ya Afrika.Baada ya kukamilisha ujenzi, ripoti ya mkaguzi wa ubora itakabidhiwa kabla ya fedha za hatua nyingine ya mkopo kutolewa’

Kwa mara ya kwanza BANK OF AFRICA- TANZANIA ilizindua mkopo wa nyumba mwaka 2011 ambao ulikuwa unajumuisha mkopo wa ununuzi wa nyumba pamoja na uboreshaji wa nyumba. Toka mkopo ulipoanza kutolewa zaidi ya shilingi bilioni 10 zimeshatolewa.

Pamoja na mikopo ya nyumba, BANK OF AFRICA- TANZANIA pia imekuwa ikitoa mikopo kwa wakandarasi wa ujenzi ili kuongeza upatikanaji wa nyumba bora za makazi na wakati huo huo wakiwezesha watu wa kawaida kuzinunua nyumba hizo.

No comments: