Friday, March 3, 2017

WADAU WA MUZIKI WA INJILI KUKUTANA JUMAMOSI UKUMBI WA CHUO CHA USTAWI WA JAMII JIJINI DAR ES SALAAM

 Mtaalamu wa Sheria kutoka Jeshi la Polisi Dk. Mkaguzi wa Polisi Ezekiel Kyogo, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Hoteli ya Lamada jijini Dar es Salaam leo wakati akifafanua kuhusu sheria ya haki miliki ya kazi za wasanii wa muziki.
 Rais wa Tanzania Music Foundation (TMF) Dk. Donald Kassanga  akifafanua mambo kadhaa katika mkutano huo ikiwa ni pamoja na
TMF, kuunga mkono jitihada za serikali za kupambana na dawa za kulevya.
Mwimbaji wa nyimbo za injili, Faraja Ntaboba akizungumza katika mkutano huo.


Dotto Mwaibale na Christina Mseja

WADAU wa muziki wa injili wanatarajia kukutana kesho kutwa Machi 4 mwaka huu kwenye Kongamano la Wasanii wa muziki huo litakalofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Mtaalamu wa Sheria kutoka Jeshi la Polisi Dk. Mkaguzi wa Polisi Ezekiel Kyogo, alisema  kongamano hilo lina dhumuni kubwa katika kujenga  uelewa kwa wasanii wa muziki  juu ya kazi zao, hususani changamoto na suluhu za kazi za Sanaa.

Kyogo alisema kazi za Sanaa ni mali na zimekosa ulinzi na hakuna jitihada zozote zinazoendelea katika kusaidia wasanii hao.Wasanii wamekosa ubunifu na watu wamekata tamaa na kujiingiza katika wimbi la dawa za kulevya. Kuwepo kwa  mapungufu ya adhabu haipunguzi uhalifu kwani wasimamizi wa sheria wanatakiwa kuwa na uwezo zaidi katika  sheria hizo.

“Lazima kuwe na sheria ya makosa ya wizi za kazi za wasanii kwani itasaidia kupunguza wizi na itaongeza kipato na ajira, kwa kuwa muziki ni mali ya jamii na ni afya na tiba”, alisema Kyogo.

Rais wa Tanzania Music Foundation (TMF) Dk. Donald Kissanga aliongeza kuwa lengo kubwa kongamano ni kuhakikisha serikali inatengeneza mazingira bora  katika tasnia nzima ya muziki jambo litakalosaidia kuongeza pato la taifa.

“Watu  wamekuwa wakiiba kazi za wasanii na kama TMF tunalaaani na kuomba serikali kupitia vyombo vya dola kuziba mianya hiyo" alisema Kissanga.

Katika hatua nyingine Kissanga alisema TMF kinaungana na Serikali katika mapambano ya dawa za kulevya nchini kwani waathirika ni pamoja na wanamuziki na wasanii kwa ujumla.

Mwimbaji wa nyimbo za injili, Faraja Ntaboba, alisema kuwa wasanii wamekuwa wakiibiwa sana kazi zao wakati wanatumia nguvu kubwa kwa kuziandaa.

"Tuna amini endapo Serikali ikisimamia vizuri kwa kushirikiana na  TMF  wataweza kulipa kodi sawa sawa na kuendesha kazi  vizuri" alisema Ntaboba.

No comments: