Wednesday, November 22, 2017

MHE MWANJELWA AWAAGIZA WAFANYABIASHARA WA MBOLEA NCHINI KUACHA HARAKA KUUZA MBOLEA KWA ZAIDI YA BEI ELEKEZI

Mgeni Rasmi-Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akihutubia kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Kwanza kwa makatibu tawala na washauri wa kilimo wa mikoa ya nyanda za juu kusini kuhusu ubora wa mbolea na mfumo wa bei elekezi ambao umefunguliwa rasmi, Jana Novemba 21, 2017. Picha Zote Na Mathias CanalNaibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo wakati akihutubia kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Kwanza kwa makatibu tawala na washauri wa kilimo wa mikoa ya nyanda za juu kusini kuhusu ubora wa mbolea na mfumo wa bei elekezi ambao
umefunguliwa rasmi, Jana Novemba 21, 2017. Makatibu tawala na washauri wa kilimo wa mikoa ya nyanda za juu kusini wakifatilia hotuba ya Mgeni Rasmi-Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kwanza kuhusu ubora wa mbolea na mfumo wa bei elekezi ambao umefunguliwa rasmi, Jana Novemba 21, 2017. Mgeni Rasmi-Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akifatilia mada mbalimbali kuhusu ubora wa mbolea na mfumo wa bei elekezi Mara baada ya kufungua Mkutano wa Kwanza kwa Makatibu Tawala na washauri wa Kilimo wa Mikoa ya nyanda za juu kusini, Jana Novemba 21, 2017.Makatibu tawala na washauri wa kilimo wa mikoa ya nyanda za juu kusini wakifatilia hotuba ya Mgeni Rasmi-Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kwanza kuhusu ubora wa mbolea na mfumo wa bei elekezi ambao umefunguliwa rasmi, Jana Novemba 21, 2017. 
Na Mathias Canal, Mbeya
Makatibu tawala kote nchini wametakiwa kutafiti na kubaini wafanyabiashara wadogo wa mbolea wanaokiuka bei elekezi kutokana na wafanyabiashara wakubwa kuwauzia wafanyabiashara hao wadogo kwa bei elekezi ya rejereja badala ya bei ya jumla.
Mwito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa wakati akihutubia kwenye ufunguzi wa mkutano wa kwanza kati ya mikutano saba (7) katika Kanda saba (7) za kilimo nchini inayotegemewa kufanyika ambao ni muhimu kwa makatibu tawala na washauri wa kilimo wa mikoa ya nyanda za juu kusini wa kuelimishana kuhusu ubora wa mbolea na mfumo wa bei elekezi ambao umefunguliwa rasmi.
Mhe Naibu Waziri wa Kilimo aliwasihi Makatibu Tawala hao wa Mikoa na wataalamu wa kilimo kuhakikisha kwamba wanasimamia bei elekezi ya mbolea, Wanatoa Elimu kwa Wakulima ili wanunue mbolea bora na pia kuimarisha vikundi vya wakulima ili waweze kutumia nguvu ya umoja katika kuboresha kilimo kwa ajili ya utoshelevu wa mahitaji ya kaya zao na kuuza ziada hapa nchini na nchi za nje.
Alisema kuwa wafanyabiashara licha ya kufahamu kuwa wanatakiwa kugawana faida na wauzaji wa rejareja lakini bado wanakiuka taratibu za kisheria hivyo aliwaagiza kuacha tabia hiyo ili mawakala wauze kwa rejareja na kwa bei elekezi bila kuathiri biashara zao.
Alisema Katika Sekta ya Kilimo mbolea ni moja ya pembejeo zinazohitaji ushirikiano mkubwa kutokana na ukweli kwamba inahitajika kwa wingi na ina gharama kubwa, inahitaji utaalamu katika matumizi yake na kwamba ni bidhaa inayoharibika kwa haraka endapo viwango vya utunzaji wake havizingatiwi.
Mhe Mwanjelwa aliwaagiza wakaguzi wote wa mbolea nchini kufuatilia na kuhakikisha kwamba kila mfanyabiashara wa mbolea ana leseni ya kufanya biashara ya mbolea ambayo itatolewa bure na TFRA na pia wahakikishe kwamba wote wamepata mafunzo haraka iwezekanavyo.
“Mbolea ni moja ya vichocheo vikubwa sana katika suala hili na hivyo, mwisho wa mkutano huu tunategemea kupata taarifa ya mikakati ya namna Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zitakavyosimamia ubora na bei elekezi ya mbolea ili Mkulima aweze kuipata na kuitumia kwa lengo linalokusudiwa” Alikaririwa Mhe Mwanjelwa
Naibu Waziri huyo alisema kuwa Wizara ya kilimo ilitunga Kanuni ya Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (Fertilizer Bulk Procurement Regulations) na kuzitangaza kwenye Gazeti la Serikali kupitia tangazo G.N. 49/2017. Pamoja na kuunda kanuni hizo, Wizara ya kilimo  ilirekebisha Kanuni ya Mbolea ya mwaka 2011 kwa Kanuni zilizotangazwa katika Gazeti la Serikali kwa tangazo G.N. Na. 50/2017 ili kuipa nguvu TFRA kukokotoa, kutangaza na kusimamia bei elekezi ya mbolea.
Aliwaagiza pia wafanyabiashara wanaotunza mbolea bila kuzingatia viwango vilivyowekwa na TFRA kuacha haraka tabia hiyo kwani kwani wanasababisha mbolea kumfikia mkulima ikiwa imepungua ubora au kuharibika kabisa na hivyo kumfanya mkulima asipate tija inayotokana na matumizi ya mbolea.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa amewataka wataalamu hao Kutenda haki katika uwajibikaji wao, Kufanya kazi kwa weledi, uaminifu, uwajibikaji uliotukuka, na nidhamu ya hali ya juu.
Aliongeza kuwa kwa yeyote atakaye kwenda kinyume na matakwa ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe rais wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli itamchukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria.

No comments: