Wednesday, December 14, 2016

MAHUSIANO CUP YAHAMASISHA MAMIA KUJITOKEZA KUPIMA VVU WAKATI WA MCHEZO WAFAINALI

  Mgeni rasmi katika fainali za Mahusiano Cup, katibu tawala wa wilaya ya Kahama, Timoth Ndanya (Katikati) akipokea maelezo kutoka kwa mwamuzi wa mchezo wa fainali kati ya timu za kata ya Mhungula.Kushoto ni Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi George Mkanza, wengine katika picha ni Solomon Rwangabwoba- Meneja Ufanisi na raslimali watu (katikati ya mwamuzi na katibu tawala) wengine ni mwenyekiti wa KDFA Bwana Ibrahim Khan na Bwana Magesa Magesa Afisa Mawasiliano Mgodi wa Buzwagi.
  Katibu tawala Wilaya ya Kahama Timoth Ndanya akisalimiana
na wachezaji wa timu ya kata ya Mhungula.
  Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi George Mkanza akisalimiana na wachezaji wa timu ya kata ya Mhungula, nyuma yake ni Meneja Ufanisi na raslimali watu wa Mgodi wa Buzwagi,Solomon Rwangabwoba.
  Mgeni rasmi Katibu tawala wa wilaya ya Kahama,Timoth Ndanya akisalimiana na wachezaji wa timu ya netball ya kata ya  Zongomela.
   Mgeni rasmiKatibu tawala wa wilaya ya Kahama, Timoth Ndanyaakisalimiana na wachezaji wa timu ya netball ya kata ya Kahama Mjini.
Mgeni rasmi wakati wa fainali za Mahusiano Cup, katibu tawala wa wilaya ya Kahama Timoth Ndanya (Mwenye track suit nyekundu) akitoa mawaidha kwa wachezaji muda mfupi kabla ya kuanza kwa fainali za Mahusiano Cup
Katibu tawala wa wilaya ya Kahama Timoth Ndanya (Mwenye track suit nyekundu) akijianda kupiga mpira kuashiria kuanza kwa mchezo wa fainali ya Mahusiano Cup baina ya timu ya Kahama Mji na timu ya Mhungula.
  Wachezaji wa timu za Kahama Mji na Timu ya kata ya Mhungula wakiendelea na mchezo wa fainali za Mahusiano Cup mchezo ulioisha kwa timu ya Mhungula kuibuka kidedea kwa kuwachapa vijana wa mjini timu ya Kahama Mji jumla ya magoli matatu kwa mawili (3-2).
  Mgeni rasmi pamoja na wageni wengine wa meza kuu wakifatilia mchezo baina ya timu za Kahama Mji na timu ya Mhungula.
Timu za netball za Kahama Mji na Zongomela zikionyeshana ufundi wa kucheza mpira wa pete wakati wa fainali za Mahusiano Cup kwa upande wa mpira wa pete. Timu ya Kahama mji iliibuka mshindi kwa kuwatandika wadogo zao wa Zongomela jumla ya vikapu 47 dhidi ya 24.
Msaani wa ngoma za asili maarufu kama “Mwanawane” wa mjini Kahama akionyesha uwezo wake wa kucheza na nyoka.
Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi George Mkanza akizungumza wakati wa kuhitimisha fainali za Mahusiano Cup mwaka 2016 pamoja na kukabidhi zawadi kwa Washindi.
  Katibu Tawala wa Wilaya Kahama Timoth Ndanya akiwahutubia wachezaji na wananchi wa mji wa Kahama mara baada ya kumalizika kwa michezo wa fainali za Mahusiano Cup.
  Nahodha wa timu ya mpira wa pete ya Kahama Mji akipokea kombe la mshindi wa kwanza pamoja na kitita cha shilingi milioni moja baada ya kuibuka kidedea katika michezo hiyo
Nahodha wa timu ya Kahama Mji akinyanyua kikombe cha mshindi wa pili kwa upande wa mpira wa miguu baada ya timu hiyo kujinyakulia ushindi wa pili, timu hiyo pia ilijinyakulia kitita cha shilingi laki saba na nusu.
  Washindi wa Mahusiano Cup Mwaka 2016 timu ya Mhungula wakinyanyua juu kombe baada ya kuibuka wababe wa mashindano ya Mahusiano Cup ambapo pia walijinyakulia kitita cha shilingi milionimoja.
Baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya Acacia Buzwagi pamoja na wafanyakazi kutoka makampuni mbalimbali wilayani wakishiriki mchezo wa kufukuza kuku.
Meneja wa Kahama FM radio Marco Mipawa akifurahia mara baada ya kumkamata kuku wakati wa Bonanza la Mahusiano
Baadhi ya wananchi waliojitokeza wakati wa tamasha la Bonanza la Mahusiano wakivuta wakishiriki katika Mchezo wa Kuvuta Kamba.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii,Kanda ya Kaskazini.

Watu zaidi ya 400 wakazi wa mji wa Kahama na viunga vyake wamejitokeza kupima VVU wakati wa mashindano ya Mahusiano Cup ambayo huusisha michezo ya mpira wa miguu na mpira wa pete.



Mashindano hayo ambayo huandaliwa na Kampuni ya Uchimbaji wa madini ya Acacia kupitia Mgodi wa Buzwagi yalizinduliwa tarehe moja desemba, yakiwa na lengo la kuhamasisha Jamii kupima afya zao na kuimarisha uhusiano baina ya wenyeji na Mgodi wa Buzwagi.



Akizungumza wakati wa Kuhitimisha fainali za michezo hiyo pamoja na kampeni ya upimaji VVU katika uwanja wa mpira wa Kahama Mji, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama Timothy Ndanya amesema wao kama uongozi wa wilaya ya Kahama wanafarijika na jitihada zinazofanywa na Kampuni ya Acacia kupitia Mgodi wa Buzwagi katika harakati za kuhakikisha Jamii inajua afya zao kwa kupima afya na kupanga maisha yao vizuri.



Ameongeza pia jitihada hizo zimekuwa zikionekana kupitia katika sekta ya michezo na hii imekuwa ikijidhihirisha kupitia programu mbalimbali za michezo ambazo zimekuwa zikiendeshwa na Kampuni ya Acacia.



Akizungumzia Mashindano ya Mahusiano Cup ya mwaka huu ambayo yamehusisha timu nyingi zaidi ukilinganisha na miaka iliyopita, Katibu Tawala huyo amesema mashindano ya mwaka huu yamesaidia kuonyesha vipaji vingi vya wanamichezo ambao hapo awali hawakuwa na fursa ya kuweza kuonyesha uwezo wao kupitia michezo.



“Kwetu sisi mmeturahisishia na kwa sababu viongozi wa vyama vya michezo wako wako hapa, hapana shaka watakuwa wamevitambua vipaji ambavyo vimekuwa vikionyeshwa kwa muda wote wa mashindano haya na watatafuta namna nzuri ya kuviendeleza pamoja na kutengeneza timu imara ya halmashauri ya Kahama Mji ambayo itakuwa ikituwakilisha katika michezo mbalimbali” Alisema Timoth.



Kwa Upande wake kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi, George Mkanza amesema michezo ya mwaka huu imekuwa ya mafanikio makubwa sana na kwamba Malengo yake yamefikiwa kwa kiasi kikubwa.


“Mwaka huu Kampuni ya Acacia kupitia Mgodi wa Buzwagi tulikuwa na dhamira ya kuwafikia wakazi wengi wa Kahma kwa njia ya michezo ili kuwapatia elimu juu ya ugonjwa wa Ukimwi pamoja na kuimarisha Mahusiano yetu na wenyeji wa Kahama, ndio maana utaona mwaka huu michezo hii imefanyika nje ya eneo la kata ya Mwendakulima na kuhusisha timu za tarafa yote ya Kahama Mji” Alisema Mkanza.



Akizungumzia takwimu za upimaji VVU kwa kipindi cha wiki moja ambacho Mashindano hayo ya Mahusiano Cup yalikuwa yakiendelea, Kaimu Meneja Mkuu huyo wa Mgodi wa Buzwagi, amesema jumla ya watu 420 walijitokeza kupima VVU ambapo kati ya hao Wanawake walikuwa  89 sawa na asilimia 21.1% na wanaume 321 sawa na asilimia 76.4%. Ambapo kati ya wote waliopima  watu 11 walikutwa na maambukizi sawa na asilimia 2.6%, Wanawake 5 sawa na asilimia 1.19% na wanaume 6 sawa na asilimia 1.42%



Michezo ya Mahusiano Cup ya mwaka 2016 ilifanyika katika viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Kahama na Uwanja wa Shule ya Msingi Mwendakulima ambapo jumla ya timu kumi na nne za mpira wa mguu zilishiri na timu sita za mpira wa pete.



Timu zilizoshiriki Mpira wa Mguu:- ni kata ya Nyihogo, Nyahanga, Busoka, Kahama Mjini, Zongomela, Malunga, Mhungula, Majengo, Mwendakulima, Ngogwa, Nyasubi, Mhongolo, Wendele, Pamoja na timu ya Mgodi wa Buzwagi, na kwa upande wa Mpira wa Pete:- timu za Kata za Kahama Mjini , Mhungula, Mwendakulima, Mhongolo, Ngogwa  na Zongomela zilishiriki mashindano hayo.



Katika michezo hiyo zaidi ya wanamichezo 400 walijitokeza kushiriki ambapo timu za Kahama Mji pamoja na Mhungula ndizo zilizofanikiwa kuingia fainali, ambapo katika mchezo wa fainali timu ya Mhungula iliibuka kidedea kwa kuibamiza timu ya Kahama mji jumla ya goli tatu kwa mbili na kujinyakulia Kombe pamoja na Shilingi milioni moja huku mshindi wa pili timu ya Kahama Mji kuondoka na kitita cha shilingi laki saba na nusu pamoja na kikombe.



Kwa upande wa timu za mpira wa pete zilizofanikiwa kuingia fainali zilikuwa ni timu za Kahama Mji na timu za Zongomela ambapo timu ya Kahama Mji iliibuka Mshindi baada ya kuwafunga wenzao wa kata ya Zongomela jumla ya vikapu 47 dhidi ya 22 na Hivyo kuwafanya timu ya Kahama Mji kuwa Washindi wa Mahusiano Cup kwa upande wa timu za netball kwa Mwaka 2016 na kujinyakulia Kombe pamoja na Shilingi milioni moja huku mshindi wa pili timu ya Zongomela ikiondoka na kitita cha shilingi laki saba na nusu pamoja na kikombe.



Katika mashindano hayo hiyo timu ya Mgodi wa Buzwagi ilishika nafasi ya tatu na kujinyakulia shilingi laki tano kwa upande wa mpira wa miguu na timu ya Netball kutoka kata ya Mwendakuliam ilikuwa mshindi wa tatu kwa upande wa mpira wa pete na kuondoka pia na shilingi laki tano. Huku timu zingine zote zikiambulia kifuta jasho cha shilingi elfu sabini kila timu.



Kabla ya kufanyika kwa fainali hizo mapema asubuhi kampuni hiyo ya Acacia kupitia Mgodi wa Buzwagi iliandaa pia Bonanza maalumu la Michezo lililowahusisha wadau mbalimbali kutoka ndani ya mji wa Kahama Bonanza lililohusisha michezo kama vile kuvuta kamba, kufukuza kuku na mpira wa miguu.
Mwisho.

No comments: