Monday, July 9, 2007

KIFO CHA AMINA CHIFUPA BADO CHATAWALA

Na Makongoro Oging
Mganga wa dawa za asili nchini Dk. Maneno Tamba ametoa siri nzito juu ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Viti maalum kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) marehemu Amina Chifupa kuwa ni cha kawaida na wala hakitokani na mkono wa mtu kama inavyovumishwa.

Akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake Magomeni Mikumi wilaya ya Kinondoni jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki iliyopita Dk. Tamba alisema kuwa anashangaa kuona baadhi ya vyombo vya habari vikiandika kuwa kifo chake kinahusishwa na watu.

Aidha aliendelea kusema kuwa Amina alikufa kifo cha kawaida kilichotokana na msongo wa mawazo, ugonjwa ambao alisema kuwa anauogopa.

Aliendelea kusema kuwa licha ya vyombo vingi kuandika kuwa kifo chake kinatatanisha, pia amepata taarifa ya kunyolewa nywele kwa Amina ambapo watu walifikiri kuwa ni kwa sababu ya kuchanganyikiwa lakini alidai kuwa marehemu alikuwa mtu anayependa usafi hivyo aliamua kuzinyoa katika utaratibu wa kawaida na si vinginevyo.

"Kifo cha Amina kilinipa mshituko mkubwa sana, punde tu nilipopata taarifa ya kifo saa 2:50 usiku nikiwa ofisini kwangu Magomeni kwa kweli nilishindwa kuendelea na kazi , niliondoka hadi Hospitali ya Lugalo kwani marehemu aliyekuwa mume wa Mpakanjia tulikuwa na ukaribu zaidi na walikuwa wakiniita baba" alisema Dk. Tamba.

Aliongeza kuwa wote hao walikuwa wakipata ushauri kwake . Aidha alitoa siri nyingine kuwa mwaka huu walipanga kwenda kuhiji Macca wote watatu (yeye, Amina na mumewe) lakini kwa bahati mbaya Mungu amechukua uhai wake kabla ya kufanya hivyo.

Aliendelea kusema kuwa marehemu Amina alikuwa kipenzi cha watu na alikuwa karibu sana na watoto yatima kwa kuwapa misaada mbalimbali ambapo alishiriki pia katika mashindano ya Korani.

Siri nyingine aliyoitoa Dk. Tamba ni kwamba Amina alikuwa mlenzi na mdhaminiwa wa watoto wa kike na kiume wenye umri wa miaka 15 wa kuhifadhi msahaafu na aliweza kutoa zawadi mbali mbali kama vile cherehani na majokofu kwa washindi.

Dk, Tamba ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha katika msiba wa Amina na shughuli mbali mbali ya mazishi alisema kuwa kutokana na ukaribu wake ndiyo maana alipewa nafasi hizo na kazi aliifanyika vizuri mpaka hatua ya mwisho.

Amina alifariki dunia Juni 26 mwaka huu katika Hospitali ya Lugalo kutokana na kile kilichoelezwa na wataalamu wa Hospitali hiyo wakiongozwa na Brigadia Salum kuwa alikuwa na magonjwa ya kisukari, shinikizo la damu na malaria, kwa bujibu wa baba yake mzee Hamisi Chifupa.Aidha alikuwa mpiganaji wa dawa za kulevya nchini.


WAPI MAISHA BORA?

Na Doto Mwaibale
Hali ya maisha ya Mtanzania wa kawaida imezidi kuwa duni kutokana na kupanda kwa ghafla kwa bidhaa kutokana na serikali kuongeza nyongeza ya kodi ambapo mafuta ya petrol na disel yamepanda bei tofauti na ilivyokuwa kabla ya kusomwa kwa bajeti ya fedha ya mwaka 2007/2008.

Kutokana na hali hiyo serikali inatakiwa kufanya jitihada za makusudi ili dhana ya maisha bora kwa kila Mtanzania iliyoanzishwa na Rais Jakaya Kikwete iende sambasamba na hali halisi ya uchumi wa mtu wa kawaida.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa mara baada ya kutanganzwa kwa bajeti mpya na serikali mwaka huu na kodi ya mafuta ya petrol na disel kupanda wafanyabiashara nao wamepandisha bei ya bidhaa mbalimbali.

Uchunguzi huo umebaini kuwa bei ya disel na petrol sasa ni kati ya shilingi 1400 (DIESEL) na 1800 kwa lita, licha ya serikali kuagiza bei ya petrol kwa lita isizidi shilingi 1398 na disel shilingi 1327 kwa lita.

Aidha upandaji wa bei za diseli umefanya nauli ya mabasi ya kwenda mikoani kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani umepanda ambapo sasa kwenda Arusha, Kilimanjaro inafikia shilingi shilingi 35,000 kwa mtu mmoja wakati nauli ya kwenda kwenda Morogoro ni shilingi 5,000 badala ya 4,000 ya awali.

Uchunguzi huo umebaini kuwa nauli kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma hivi sasa ni shilingi 12,000 badala ya shilingi 9,000 na 10,000 iliyotumika kabla ya kutangazwa bajeti mpya.

Wakati hali ya maisha ikiwa imepanda kwa kiasi hicho, mishahara ya wafanyakazi bado haijapanda hivyo vyama vya wafanyakazi vimetishia kufanyika kwa mgomo nchi nzima.

Katika Bajeti yake, Serikali imetangaza ongezeko la asilimia 12 ya mishahara ya watumishi wa umma ambapo imeongeza kima cha chini kutoka shilingi 75,000 hadi 84,000 jambo ambalo limepingwa na vyama vya siasa na kutaka kima cha chini kiwe shilingi 215,000.

Kufuatia hali hiyo wanachi wengi wamelitaka Bunge kumsaidia Rais Kikwete kwa kuangalia upya bei ya dizeli ili falsafa ya maisha bora kwa kila mtu aliyoitoa iweze kufanya kazi.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili juzi walisema, Bunge bila kufanya hivyo raia wataendelea kuishi kwenye nyumba duni kama inavyoonekana pichani mbele huku wakikosa huduma muhimu kama maji safi na salama na kulazimika kusafiri kwa kutumia miguu au baiskeli badala ya magari.

“Ni vema Bunge wakaangalia upya bei ya mafuta ya dizeli la sivyo hali itazidi kuwa mbaya,” alisema Bw. Zuberi Ally, mfanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar esw Salaam.

1 comment:

Anonymous said...

nashukuru sana mr Mrisho kwa kutuanzishia kutudokeza kidogo na pia kutuonjesha habari za magazeti haya,maana nayo yana chachu yake ktk maisha siyo kila siku mtu kusoma strong magazeti tuuu na udaku una sehemu yake ktk maisha au nakosea? twashukuru saaanaaa.Salam Shigogo