Sunday, September 2, 2007

MISS AIBU!


Na Issa Mnally
Shindano la Miss Tanzania 2007-08, lililofanyika juzi (Jumamosi) kwenye Viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam, lilitia aibu, kutokana na asilimia kubwa ya watazamaji kutoridhishwa na matokeo.

Watazamaji hao wanaokisiwa kuwa 95% ya wote waliohudhuria onesho hilo Leaders, walimkataa mshindi wa taji hilo mwaka huu, Richa Adhia.

Kwa mujibu wa maoni ya watazamaji hao, akiwemo Miss Tanzania 1999-2000, Hoyce Temu, Richa hakustahili kwakuwa hana sifa zinazotosheleza kuiwakilisha nchi katika Mashindano ya Miss World.

Ilielezwa na watazamaji kuwa majaji wamelamba garasa kumchagua Richa kwa sababu asili yake ni Bara la Asia, hivyo hajui utamaduni wa kitanzania.

“Hii siyo sawa, kulikuwa na Waafrika wenye sifa na walijibu swali vizuri tena kwa kujiamini, nashaangaa majaji wamemchagua Richa, wakati rangi yake haiwakilishi Utanzania,” alilalamika Hoyce huku akitokwa machozi.

Hoyce aliwalaumu majaji, Jacqueline Ntuyabaliwe na Sophia Byanako kuwa wanaelewa hali ya mashindano ya urembo kimataifa, lakini wameruhusu mtu asiye na sifa kutwaa Taji la Miss Tanzania.

Aidha, katika kuonesha kutoridhishwa na matokeo, maelfu ya watazamaji, waliondoka kwenye Viwanja vya Leaders na kuacha viti vitupu, mara Jaji Mkuu wa shindano hilo, Miss World 2001-02, Agbani Darego, alipomtangaza mshindi.

Wengi kati ya watazamaji hao, walinung’unika kwamba Lilian Abel (Kinondoni) ndiye angechaguliwa mshindi kwakuwa alijibu swali vizuri tena kwa kujiamini.
“Hawa wanatutania, kila kitu kiliandaliwa, haiwezekani Queen David (Temeke) achaguliwe nafasi ya tatu, wakati alishindwa kujibu swali na kubabaika bila mpango.
“Hatuwezi kuwaamini majaji, ilikuwaje Miss Lake Zone (Hadija Sule), ashindwe kuingia hata tatu bora, wakati alijibu swali vizuri tena kwa kujiamini?” Alihoji Rasta Alloyce wa Tabata, Dar es Salaam.

Mbali na hilo, Miss Ilala, Latifa Warioba aliwashangaza wengi, kutokana na kushindwa kufika hata tano bora, licha ya kuongoza kwa kushangiliwa na kupewa nafasi kubwa ya kufanya maajabu.

Mpenzi wa tasnia ya urembo, Jackson Lititi wa Ilala Dar es Salaam, alisema, Latifa alistahili kushinda, lakini inawezekana aliangushwa mapema kwa sababu alikuwa akiandikwa sana kwenye magazeti.

Akijibu malalamiko hayo, Mratibu wa Miss Tanzania, Hashim Lundenga alisema, majaji walitenda haki katika kuchagua washindi na kuwabeza wanaopinga kuwa ni mitazamo yao.

“Kila mshiriki alikuwa na haki sawa, wote ni Watanzania, kwenye shindano, vigezo ndivyo vinavyozingatiwa, kila Mtanzania ana haki ya kutoa maoni, lakini uamuzi wa majaji uheshimiwe,” alisema Lundenga a.k.a Anko.

Kioja kilichojitokeza kwenye mashindano hayo ni Miss Tanga, Victoria Martin, aliyekuwa akipewa nafasi ya kutwaa taji hilo, kuumbuliwa na swali la Kiingereza aliloulizwa.

Victoria, aliyeanza kujibu vizuri na kushangiliwa, alishindwa na kusita sita katikati, kitendo kilichoibua mayowe ya watazamaji, waliodai kwamba mrembo huyo amewaangusha.

Aidha, Miss Temeke, Queen David, aliwatibua watazamaji kutokana na lafudhi yake mbovu, wakati alipokuwa akijibu swali kwa Lugha ya Kiswahili.

Baada ya ushindi huo, Richa Adhia sasa ataiwakilisha nchi kwenye Fainali za 57 za Miss World, zitakazofanyika Sanya, China, Desemba, mwaka huu.

Lilian Abel ndiye aliibuka mshindi wa pili, namba tatu alishika Queen David, wakati Hadija Sule na Victoria Martin walitinga tano bara.

Mshindi alikabidhiwa kitita cha shilingi milioni nane pamoja na gari aina ya Toyota Rav 4, lenye thamani ya shilingi milioni 45.

(ZAIDI NENDA: WWW.globalpublisherstz.com/ijumaa wikienda)

6 comments:

Anonymous said...

huyo hoyce temu kajiaibisha tu, miss hana rangi ya kuiwakilisha tanzania!! rangi ya kuwakilisha tanzania ni ipi? ende bungeni ambapo serikali ya nchi inapimwa akaone ! kuna watu weupe kuliko huyo richa, pale timu za mpira na mengineyo wakiomba wadhamini, mbona huwa hawajali rangi ya mdhamini wao!
yeye hoyce ndio hakufaa kuwa miss tanzania kwa kuwa akili yake imetawaliwa na ubaguzi ambayo sio sera ya tanzania.

Anonymous said...

huyu hoyce katia aibu kubwa sanaa atadharaulika sasa

Anonymous said...

Hakuna nyie, inauma sana nadhani hata Mimi ningekuwepo kwenye hilo shindano ningelia sana, kwani inatia uzuni kuona nijinsi gani tulivyotawaliwa na watu weupe, hata sisi wenyewe kujiwakilisha Miss World hatuwezi, jamani inauma sana, ukizingatiwa huku kwao tulipo hata uweraia maadamu ni mweusi , hawakuruhusu kushiliki kwenye mashinda yao, sasa iweje sisi leo?,inabidi tupende rangi yetu na vitu vyetu jamaniiiii eeeeeh.
Imeniuma sana , ndio ishakuwa lakini.
Nyie huko Tanzania hamjui wanavyotunyanyasa hao mbwa hao, ndio maana tuwanyenyekea sana.

Anonymous said...

Hivi nyie 'makaburu' kuwa mtanzania lazima uwe na rangi ya mpingo? Binti aliyeshinda ni mtanzania na katimiza vigezo vyote. Acheni ushamba - badilisheni katiba na masharti ya uraia basi! Tangu ngazi ya vitongoji alishinda mkawa kimya kushinda umiss tz ndo mnakuja juu! Leteni hoja zenye mantiki na si kulalama tu!

Anonymous said...

Huyo Hoyce Temu akumbuke aliposhinda enzi zake kuna walioshindwa na kuna ambao hawakuridhika na ushindi wake. Akumbuke asiyekubali kushindwa si mshindani. Inaelekea Hoyce alishakuwa na jina la mshindi kwa vigezo vyake - akumbuke kuwa mshindi anachaguliwa na majaji anaotumia vigezo mbalimbali. Naungana na Msafiri kuwa Hoyce na wengine wenye mawazo ya kibaguzi hawafai kuwa ma-miss TZ. Mkitaka kuendekeza weusi anshizeni miss mtanzania mweusi!

Anonymous said...

C'mon "Asia" girl as "Miss tanzania"?. Kweli Watanzania tumeishiwa sana tena.