Friday, October 26, 2007

SHOWBIZ


Bery Black atimba TMK

Unaweza usiamini, lakini ukweli ni kwamba, kutoka visiwani Zanzibar, kijana Bery Black aliyekuwa akifanyia kazi ndani ya kundi la 2Bery, ametia maguu ndani ya kundi la TMK Wanaume Family kwa ajili ya kufanya nalo kazi.

Akiwa anafanya vizuri na kazi kama Unisamehe na Wajua, msanii huyo ambaye jina lake kamili ni Mbaraka Abdullah Mgeni, alionesha azma hiyo ya kujiunga na TMK hivi karibuni baada ya kukamilisha albamu yake ya kwanza aliyoipa jina la Niite Black, kutoka katika studio yake, Tedy Records iliyopo Zanzibar.

Ndani ya ShowBiz, Meneja wa TMK Family, Said Fella alithibitisha hilo lakini alitamka kwamba siyo kwamba mchizi atasimama jukwaani pamoja na Wanaume na kupiga shoo, isipokuwa kazi zake zitakuwa zikisimamiwa na TMK Family. 'Kwa mfano hivi sasa tayari albamu yake nimeshaikabidhi kwa wadosi, siku chache zijazo itatinga mtaani.

'Lakini pia tutaangalia uwezekano, huenda baadae mchizi tukawa naye kundini moja kwa moja. Baadhi ya kazi zinazopatikana katika albamu yake hiyo ni pamoja na Ni wewe tu, Dance Floo, Utamu wa penzi, Ntakufuata, Nimekosa, Naitwa, Unisamehe, Wajua, Niite Black uliobeba jina la albamu na nyingine', alisema Fella.

Katika albamu hiyo jamaa kawapa shavu wasanii kibao wakiwemo Suma Lee, Shirko, Mh. Temba na wengineo.

No comments: