Friday, May 16, 2008

IJUMAA SHOWBIZ!

Akudo Impact Kukabidhiwa mikoba na Mzee Bozi mbele ya Waziri Mkuu!
Vijana wa ‘Masauti’, Akudo Impact, leo mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Pinda ambaye atakuwa mgeni rasmi kwenye onesho la utambulisho wa albamu yao, ‘Impact’ watakabidhiwa ‘mikoba’ na mkongwe wa muziki huo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, Bozi Boziana, Christopher Lissa anakupa full stori.

Akiwa sambamba na timu yake, Bozii au ‘Mzee Benz’ atawapiga tafu vijana hao wa Akudo kwa shoo iliyosimama huku akiwaonesha mambo mbalimbali ambayo yatawafanya waendelee kufunika kwenye game muda mrefu bila kupotea, kupitia shoo hiyo ambayo itapigwa ndani ya Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam na kuacha historia.

Mratibu wa Onesho hilo, Bahati Singh alisema na ShowBiz kwamba, Bozii ambaye alidondoka Bongo mwanzoni mwa wiki hii amesema kuwa mbali na yote atafanya maajabu stejini huku akiwakumbusha mashabiki miondoko ya ‘Nzawisa’ iliyotamba miaka ya nyuma. “Shoo yake itakuwa kama ni kuwarithisha mikoba yake ya ‘uchawi’ wanamuziki wa Akudo.

“Pia kutakuwa na miondoko ya Pwani ambayo itaporomoshwa na kundi zima la Jahazi Morden Taarab. Vilevile tunashukuru Mheshimiwa Pinda amekubali mwaliko wetu kitu ambacho kimezidi kututia moyo wa kufanya maandalizi makubwa, watu waje washuhudie vitu tofauti kabisa usiku wa leo kwa kiingilio cha shilingi elfu kumi tu,” alisema Sigh.

Celtel Idols: Safari ya kuelekea TOP 10 imeanza
ShowBiz bado inaendelea kulifuatilia shindano la kumtafuta kijana mwenye uwezo wa kuimba lenye jina la Celtel Pop Idols. Wiki hii washiriki wawili, Trinah kutoka Uganda na Faycal wa Zambia wamefanikiwa kuungana na wenzao Ammara kutoka Zimbabwe na Cynthia kwenye hatua ya kuelekea Top 10.

Taarifa iliyotumwa na Lucy Kihwele wa MultiChoice Tanzania kunako safu hii inasema kwamba, Trinah amepata ushindi huo kutokana na kura nyingi zilizotumwa na mashabiki baada kufanya vizuri mbele ya majaji na wimbo wenye jina la ‘When I need you’, ishu ambayo ilirushwa hewani majira ya usiku kupitia Kituo cha M-Net, Mei 12, mwaka huu.

Faycal ambaye ni miongoni mwa washiriki wachache waliosalia kunako shindano hilo, naye aliwapagawisha majaji ile mbaya kwa wimbo wenye jina la ‘Love’ ambao pia ulimpatia kura nyingi kutoka kwa mashabiki.

Zikiwa zimesalia awamu nne kukamilisha Top 10, macho ya mashabiki wengi yameelekezwa katika mpambano utakaofanyika Jumapili ya wiki hii. Washiriki wanaotabiriwa kufanya vizuri katika mchujo huo ni pamoja na Adiona (Zimbabwe), Chibwe (Zambia), Doris (Kenya), Eric (Zimbabwe), Nicollette (Uganda) na Samukeliso (Zimbabwe). Hayo ndiyo mambo ya Celtel Pop Idols kutoka M-net.

No comments: