Monday, June 15, 2009

WIKIENDA SHOWBIZ!


Diddy:mademu 17 akiwemo wa mshikaji wake B.I.G
Mkali wa Hip Hop laini, Sean John Combs mwenye a.k.a kibao, Diddy, P Diddy Puffy au Dippy ndiye tunamcheki leo kwenye ‘Ebwana Dah!’ yakiwa ni maombi ya baadhi ya wasomaji wa safu hii. Kama ilivyo kwa mastaa wengine waliopita, mchizi pia ameonesha kuwa na listi ndefu ya mastaa wa kike aliyowahi kushirikiana nao kunako ‘malove dave’.

Kwa mujibu wa mtandao unaodili na ishu hizi na kama ulikuwa haufahamu, Diddy amewahi kujiachia na mwana Hip Hop wa kike, Lil Kim ambaye pia alikuwa mpenzi wa rafiki yake mkubwa, marehemu Notorious B.I.G. Mbali na Kim mchizi alianza kutoka na mwanadada Carmen Bryan, kisha Karrine Steffans na baadaye Misa Hylton-Brim aliyedumu naye kwa miaka miwili, 1993-1995.

Mwaka 1996, Diddy aliendeleza ‘malove dave’ kwa kutoka na Kim Porter ambaye alifanikiwa kuzaa naye mtoto wa kwanza, kabla ya mapacha wawili wa kike aliowapata hivi karibuni baada ya kurudiana naye. Kabla ya mapacha hao jamaa alimshiti Kim na kudondokea kwa Jennifer Lopez (1998-2001), Alicia Douvall (2002), Naomi Campbell (2002 - 2003), Sarah Chapman (2004 - 2006) na Aubrey O`Day (2005 - 2006).

Warembo wengine aliyowahi kutoka nao ni Alexandra Cheron (2006), Diana Bianchi (2006), May Andersen (2007), Sienna Miller (2007) Cassie Ventura (2008) na Caroline D`Amore (2008). Diddy ambaye nyota yake ni Nge, akiwa na urefu wa futi tano na nchi tisa ambazo ni sawa na sentimita 175 alizal-iwa Novemba 4, 1969 huko Harlem, New York, Marekani. Mbali na kuimba pia ni mtayarishaji muziki kupitia lebo yake, Bad Boys Entertainment.
***********************
Dudubaya: Wazungu wampa ulaji
Baada ya kutulia kwa muda mrefu bila kujihusisha na ishu yoyote ya ukorofi kama alivyokuwa akifanya siku za nyuma, msanii Godfrey Tumaini a.k.a Ze Dudu, ameibukia kunako safu hii na kutamka kwamba, cheo cha umeneja alichopewa kwenye Kampuni ya Art in Tanzania kimemfanya awe na nidhamu ya kutosha, Richard Bukos alipiga nae stori.

Dudu aliyasema hayo usiku wa kuamkia Juni 13, mwaka huu ndani ya Ukumbi wa TTC Chang’ombe, Dar es Salaam ambapo kampuni yake ilikuwa imedhamini kinyang’anyiro cha kumtafuta Miss Chang’ombe 2009 kilichofanyika katika ukumbi huo.

“Kutokana na nafasi niliyonayo kwenye kampuni hiyo, nitawashangaza sana mabosi wangu ambao wengi ni watasha kama nitafanya ishu za ukorofi ambayo ni mambo ya kizamani,” alisema Dudu.

Aidha, msanii huyo alisema kwamba, siku hizi hata kwenye kumbi za burudani amepunguza kwenda labda kama atakuwa amealikwa kwasababu ya shoo, siyo kuibuka bila mpango wowote kama ilivyokuwa zamani.

Ze Dudu ambaye ametamba kuvuta mkwanja mrefu kwenye kampuni hiyo, amesema kuwa staili yake ya kufanya muziki hivi sasa ni kutoa ngoma moja moja tu, hana mpango wa kugonga albamu kwakuwa singo inapokuwa bomba shoo utakazoalikwa zinalipa kuliko kuhangaika na maandalizi ya albamu.
**************************

Suma Lee, Fid Q, Josline ndani ya Mpo Afrika
Kutoka ndani ya mradi wa muziki wa kizazi kipya ambao kuna tetesi kwamba kila kukicha unazidi kupoteza muelekeo, safu hii ilipata kupiga stori na msanii Ismail Seif a.k.a Suma Lee na kugundua kwamba pamoja na hilo kila kukicha baadhi ya watu wamekuwa wakifungua studio mpya, Rhobi Chacha anashuka nayo.

Suma alisema na safu hii kwamba baadhi ya kazi zitakazokuwa ndani ya albamu yake zimefanyika kupitia Studio za Mpo Afrika zilizopo pande za Tandika Davis Corner, Dar es Salaam kitu ambacho kiliifanya safu hii ibaini kwamba kuna studio mpya yenye jina hilo.

“Lakini pamoja na upya wa studio hiyo jamaa wako safi kuanzia prodyuza wao, Benny Msama hadi vyombo vya kisasa wanavyotumia. Ongezeko la studio hapa Bongo litazidi kuleta changamoto kwetu sisi wasanii,” alisema Suma.

Safu hii pia ilimuendea hewani Prodyuza wa studio hiyo, Benny ambaye alisema kwamba, siyo Suma Lee tu bali wasanii kibao wakiwemo Josline, Fid Q, Juma Jazz na wengine wameshapiga nao kazi.
****************************
Miss Dar City Centre hukumu imekaribia
Warembo wanaowania taji la Miss Dar City Centre ambao hukumu yao ni Juni 26, mwaka huu wameelezewa kuwa na viwango vya hali ya juu kuanzia elimu, uelewa na uzuri hali ambayo inawapa matumaini waandaaji wa kinyang’anyiro hicho ya kutoa Miss Tanzania mwaka huu, Christopher Lissa anashuka nayo.

Mratibu wa shindano hilo, John Doto kutoka Kampuni ya Sisi Entertainment, ameliambia Ijumaa Wikienda hivi karibuni kwamba, tangu warembo hao walipotinga kambini kumekuwa na mchujo mkali wa kuwasukuma nje ya shindano wasichana ‘vimeo’.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha Miss Ilala, Miss Tanzania na Miss World 2009 anatokea Dar City Centre.

Aliongeza kuwa, tayari maandalizi ya ujenzi wa jukwaa la kisasa kwa ajili ya shindano hilo litakalofanyika Juni 26, 2009 kwenye Ukumbi wa Lamada limeanza kuandaliwa huku wananchi kibao wakijotokeza kushuhudia mazoezi ya walimbwende hao.

Kwa upande wa zawadi, Doto alisema: “Tutatangaza wiki moja kabla ya fainali kufanyika. Tumeandaa zawadi nono ambazo nina hakika zitawavutia wengi.

“Lakini nitoe wito kwa wananchi na wadau wote wa masuala ya ulimbwende kujitokeza kwa wingi ndani ya Hoteli ya Lamada iliyopo Ilala siku ya Juni 26 kuja kumlaki Miss Dar City Centre ambaye baadaye atakuwa Miss Ilala, kisha Miss Tanzania na hatimaye Miss World.”
***********************

No comments: