Thursday, July 16, 2009

IJUMAA SHOWBIZ!

MWANA FA: WASHKAJI ULAYA MAISHA MAGUMU
Siku chache baada ya kudondoka kutoka pande za Uingereza anakopiga kitabu, mkali wa Bongo Flava, Hamis Mwinjuma a.k.a Mwana FA amesema na ShowBiz amejionea kwa macho yake baadhi ya watu wanaoishi huko wakitaabika bila kuwa na ishu ya kufanya.

Msanii huyo alisema kwamba, baadhi ya vijana wengi bado wana ndoto za kwenda Ulaya wakidhani kwamba maisha ni rahisi kitu ambacho siyo cha kweli kwakuwa huko pia wapo watu wengi wasiokuwa na ajira wanasota mitaani.

“Ulaya maisha magumu washkaji, mtu kama una dili yako ya kupata miambili miambili Bongo bora utulie uendelee kuongeza kipato na kuijenga nchi yako badala ya kukimbilia Ulaya. Ninachoongea watu wanaweza wasiniamini lakini anayeweza aende akajionee mwenyewe,” alisema FA ambaye hivi sasa anafanya vyema na ngoma yake mpya, ‘Nazeeka sasa’ iliyowashirikisha Prof. Jay na Sugu.

Akiizungumzia picha ya Rais Kikwete iliyopo katika baadhi ya tisheti zake (kama anavyoonekana pichani), Hamisi alisema kwamba, hivi sasa ameamua kuachana na ujinga wa kuvaa nguo zenye picha za mastaa wa Ulaya wakati yeye ni Mbongo. “Yaani mimi namfagilia sana JK kuliko Rais yeyote duniani kwa kuwa ni mzalendo wa kweli. Kwangu mimi Kikwete wa kwanza halafu anafuata Obama,” alisema FA.

Aidha, mchizi aliiambia safu kuwa, mwishoni mwa mwezi huu atarudi Uingereza kwa ajili ya kumalizia masomo yake ambapo anatarajia kukusanya mafaili yake na kurudi Bongo Desemba mwaka huu akiwa na Masters yake.
*************

KR, TEMBA, CHEGGE WAKWEA PIPA
Wasanii watatu waliopo ndani ya Kundi la TMK Wanaume Family, Rashid Ziada ‘KR’, Amani Abas ‘Mh. Temba’ na Said Juma ‘Chegge’ katikati ya wiki hii walikwea pipa na kuruka pande za Liberia kwa ajili ya kupiga shoo kadhaa kunako tamasha la amani lililoandaliwa na serikali ya nchi hiyo.

Akipiga stori na Showbiz muda mchache kabla wasanii hao hawajapaa angani, Meneja wa kundi hilo, Said Fella alisema kwamba kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao wameamua kwenda wasanii hao watatu kwa ajili ya kuliwakilisha kundi zima na Tanzania kwa ujumla katika mwaliko huo rasmi.

“Kutokana na bajeti ya waandaaji imebidi waondoke watatu tu, lakini hakijaharibika kitu kwakuwa naamini watatuwakilisha sote na Tanzania kwa ujumla,” alisema Fella. Tamasha hilo la amani Liberia limefanyika juzi na wasanii hao wanatarajia kudondoka Bongo kesho Jumamosi kwa ajili ya kujiandaa na ziara yao ya pamoja na kundi la Tip Top Connection itakayoanza Aprili 24, mwaka huu Sumbawanga, mkoani Rukwa.
******
Tolywood Kuibua vipaji zaidi ya 30, riheso kuanza wiki ijayo
Lile shindano la kutafuta vipaji vitakavyoshiriki kwenye filamu mpya za Kampuni ya Tollywood ‘Movie Star Scouting’ limeingia kunako hatua nyingine ya kupendeza zaidi.

Akipiga stori na safu hii Mkurugenzi wa filamu ndani ya kampuni hiyo, Hamie Rajab alisema kwamba, baada ya usaili uliofanyika Dar es Salaam hivi karibuni wamefanikiwa kupata vipaji kadhaa ambavyo vitaanza kufanyiwa lieso (mazoezi) wiki ijayo.

“Tumepata zaidi ya wasanii 30 ambao tutaanza nao mazoezi Jumatatu ya wiki ijayo katika sehemu ambayo tutaijata hivi karibuni kabla ya kuanza shughuli kubwa ya upigaji picha wa filamu ya ‘Tears On Valentine Day’ ambayo mpaka mwishoni mwa waka huu inatakiwa iwe imekamilika,” alisema Rajab.

Aidha, Mkurugenzi huyo alisema kwamba, mbali na wasanii hao wapya muvi hiyo pia itawapa shavu mastaa wa maigizo kama Steven Kanumba, Vicent Kigosi ‘Ray’ (pichani), Blandina Chagula ‘Johari’, Jokate Mwigelo na wengine kibao.
***********
JINI KABULA NDANI YA HOSTEL YA CHUZI
Staa wa maigizo na muvi za Kibongo, kutoka ndani ya indastri ya muvi za Kibongo, Mariam Jolwa a.k.a Jini Kabula (anayeonekana katika pozi hapo uu) ni miongoni wa wasanii waliopo ndani ya filamu ya Hostel iliyodondoka kitaani hivi karibuni chini ya maandalizi yake, Tuesday Kihangala ‘Mr. Chuzi’.

Kwa mujibu wa muandaaji, muvi hiyo ambayo imetoka chini ya Kampuni ya Tuesday Entertainment, mastaa wengine wanaopatikana ndani ya filamu hiyo ni pamoja na Mohamed Mwikongi ‘Frank’, Aunt Ezekiel, Ahmed Olutu ‘Mzee Chilo’ na wengine kibao.

“Muvi hiyo ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wa filamu za Kibongo imetoka ikiwa kwenye DVD, VCD na VHS. Tunashukuru inaendelea kufanya vizuri sokoni, hiyo inaonesha ni jinsi gani hivi sasa Watanzania walivyokuwa na muamko wa kuthamini vitu vya nyumbani,” alisema Chuzi.
********

Ijumaa Sexiest Barchelor inakuja
Shindano la ukweli lililowahi kuwavutia mashabiki wengi, Ijumaa Sexiest Barchelor linaloandaliwa na gazeti hili linakuja tena kwa kasi ya ajabu. Ili kuwapata mastaa wa kiume ambao watashiriki kwenye mpambano huo, wewe msomaji na mpenzi wa shindano hilo unahusika.

Unachotakiwa kufanya ni kututumia jina la staa wa kiume ambaye unadhani anastahili kuingia kwenye mpambano huo utakaoanza hivi karibuni. Andika ujumbe mfupi (SMS) ukilitaja jina hilo kisha tuma kwenda simu namba 0787-110 173.
*****

MKALI WA MWEZI (MONTHLY BEST PERFORMER
Kupitia shindano hili, ‘Mkali wa mwezi’ leo tunashuka na majina kumi ya mastaa mbalimbali wa Kibongo waliotajwa kuwania nafasi moja ya ushindi.

Kwa mujibu wa kura za wasomaji na wapenzi wa mpambano huu, mastaa hao ni Kanumba, Ngwea, Yusuph Mlela, Marlaw, Chid Benz, Ray C, Madee, Mrisho Ngassa, TID na Mrisho Mpoto.

Mpira unarudi kwako ‘jaji’ ambaye ni wewe msomaji, unadhani kati ya hawa nani anastahili kuwa mkali wa mwezi huu wa Julai? Tutumie ujumbe mfupi kupitia simu namba 0787-110 173, e-mail:mcgeorge2008@gmail.com.
***********
compiled by mc george

No comments: