Tuesday, July 28, 2009

Lishe ndiyo kila kitu kwa mwenye virusi-2

you are what you eat

KWA NINI MAZIWA YASIYO NA MAFUTA?
Kabla ya kuendelea zaidi, napenda kuelezea kuhusu suala la unywaji maziwa na kwamba maziwa yaliyosahihi ni yale yasiyo na mafuta. Kwa kawaida maziwa yana mafuta, tena mengi ambayo kiafya siyo mazuri, japo ndani ya maziwa kuna virutubisho muhimu sana katika miili yetu. Justify Full

Hivyo unapokunywa maziwa, tahadhari kubwa inapaswa kuzingatiwa. Kuna utayarishaji wa maziwa wa aina tatu. Aina ya kwanza ni maziwa yenye mafuta yake yote (Full Cream Milk), pili ni maziwa yenye kiasi kidogo cha mafuta (Low Fat Milik) na tatu ni maziwa yaliyoondolewa mafuta kabisa (fat Free Milk). Kiafya inashauriwa kunywa maziwa yenye mafuta kidogo au yale yasiyo na mafuta kabisa. Hivyo unaponunua maziwa na kukawa na nafasi ya kuchangua, pendelea Fat Free Milk kuliko Full Cream Milk, maziwa yenye mafuta huchangia matatizo ya presha na magonjwa ya moyo.

Kwa wale wanaokamua maziwa wenyewe na kutumia moja kwa moja, wanashauriwa kuyachemsha kwanza na kisha kuyaacha yapoe, maziwa yanapopoa, hujenga utandu juu ambao wengine huuita ‘malai’. Utandu huo ni mafuta yanayotakiwa kuenguliwa na kuwekwa pembeni, ili ujiepushe na matatizo ya moyo usipende kula mafuta hayo.

Tukirejea kwenye mada yetu kuhusu lishe bora, kwa muhtasari unapaswa kuelewa kiwango au uwiano wa vyakula unaopaswa kula kulingana na mahitaji ya mwili wako, uwiano huo ni: Vyakula vya Protini unapaswa kula asilimia 15 hadi 20. Vyakula vya wanga unapaswa kula asilimia 50 hadi 60 ya vyakula unavyokula kila siku na mafuta unapaswa kula asilimia 25 tu.

Hii ina maana kwamba vyakula vya wanga ndivyo ambavyo tunapaswa kula kwa wingi sana vikifuatiwa na protini na mwisho ni mafuta. Kwa wale waathiriki ambao wanaendelea kupoteza uzito licha ya kujitahidi kula lishe bora, wanashauriwa pia kutumia vidonge vyenye virutubisho (Food Supplements) ili viwasaidie kujaza mapengo ya lishe waliyonayo na hivyo kuongeza uzito.

Vidonge vya aina hiyo ambavyo vinaaminika duniani kwa ubora, huwa vinatengenezwa na kampuni ya GNL na mengine kama hayo, vidonge hivyo vinapatikana sehemu mbalimbali nchini kupitia mawakala maalum. Kwa wenye nafasi ya kutumia vidonge hivyo, afya zao huimarika haraka sana kutokana na kuwa na virutubisho asilia vitokanavyo na matunda, mboga au nafaka. Mwisho, ukisha kuwa muathirika wa virusi vya ukimwi, suala la kuzingatia lishe bora linabaki kuwa muhimu na la lazima kwako kuliko kitu kingine chochote. Wakati huu, huna hiyari ya kutokula kwa kufuata ushauri wa wataalamu, kama ilivyo kwa yule asiyeathirika, vinginevyo utakuwa unaharakisha kifo chako.

No comments: