Friday, June 19, 2009

IJUMAA SHOWBIZ!

Shaa: Nina zawadi kutoka kwa Jide
Kutoka pande za Masaki, Dar es Salaam anakofanyia kazi zake kupitia Studio za MJ Records, msanii wa bongo flava anayesumbua stejini, Sarah Kaisi a.k.a Shaa amesema na ShowBiz kwamba mwanadada Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ amemzawadia wimbo mmoja mkali baada ya kuvutiwa na kazi anazofanya, Edna Katabalo anajiachia nayo.

Ndani ya safu hii, Sara alisema kwamba, ngoma hiyo ambayo hakuwa tayari kuitaja jina hivi sasa anaifanyia mazoezi ya nguvu ili atakapoingia studio atoke na kitu cha nguvu ambacho kitamfanya Lady Jaydee afurahi na kuamini kwamba zawadi hiyo ameidondosha mahali pake.

“Niliifurahia zawadi hiyo kutoka kwa dada Judith kwani ni heshima ya pekee aliyonipatia, ukizingatia kwamba wapo wasanii wengi ambao wanafanya vizuri katika muziki wetu lakini kaamua kuniandikia wimbo mimi na siyo wengine,” alisema Shaa ambaye hivi sasa anapoteza na ngoma zake mbili, ‘Zamu yangu’ na ‘Pambazuko’ ambao kampa shavu Ambwene Yesaya ‘A.Y’.
********
Chid Benz

Yakuza Mob

Chid Benz, Yakuza ndani ya Beach Party
Msanii Rashid Makwilo a.k.a Chid Benz ni miongoni mwa wakali wa Bongo Flava watakaowakilisha kwenye tamasha maalum la ufukweni lililopewa jina la ‘Beach Party Concert’ litakalogongwa Juni 27, mwaka huu pande za Maeese Beach, Kigamboni.

Akipiga stori na ShowBiz mratibu wa tamasha hilo, George Mushi ‘G-Body’ alisema kwamba, ishu hiyo ni maalum kwa ajili ya kuwakutanisha vijana wenye umri tofauti ili waweze kubadilishana mawazo.

“Mbali na Chid Benz, wasanii wengine watakaopiga shoo siku hiyo ni pamoja na Stopper Rhymes, Nemo, PNC, Hemed, Yakuza Mobb na Wa-Don Town, huku JS’s Entertainment wakiangusha disko la ukweli,” alisema George.
*********
Bobby Wine akiwa na AY (kulia)
Chamelione (kushoto) akiwa na Bebe Cool
Bob Wine, Bebe Cool wazigonga
Kutoka pande za Uganda au ‘UG’, ShowBiz iliinyaka ishu kwamba, mastaa wawili wa muziki, Bebe Cool na Boby Wine hivi karibuni walichapana makonde hadharani kiasi cha kuumizana vibaya, Christopher Lissa anashuka nayo.

Chanzo chetu cha habari kutoka nchini humo kilisema kwamba, mastaa hao wenaopewa heshima kubwa nchini humo na Afrika Mashariki kwa ujumla, walipeana mikono hiyo kwenye ‘konseti’ moja kubwa la muziki lililosababishwa kunako Jiji la Kampala.

“Chanzo cha ugomvi huo inasemekana kuwa ni baada ya Boby Wine kumshutumu Bebe Cool kuwa amemkashifu kwenye baadhi ya nyimbo zake. Sakata hilo limesababisha Bebe Cool kuumia vibaya na kulazwa katika Hospitali ya Mulago iliyopo Kampala,” kilisema chanzo hicho.

Akihojiwa na kituo kimoja cha Televisheni nchini humo, Boby Wine alikiri kumchapa Bebe Cool huku akijifagilia kwamba yeye ni mwanamasumbwi mzoefu (japo ajawahi kupanda ulingoni).

Kufuatia tukio hilo, Boby Wine ambaye anamiliki jumba kubwa na magari ya kifahari nchini humo, ameingizwa kwenye orodha ya wasanii wakorofi kwani hivi karibuni aliingia kwenye mzozo mkali na Halmashauri ya jiji hilo, uliosababisha aburuzwe mbele ya Pilato katika mahakama moja akituhumiwa kujenga nyumba kwenye eneo lisiloruhusiwa.
*******
Lamar

Marehemu mama Lamar
Kila ninachofanya ni sababu ya mama
Prodyuza Lamar kutoka ndani ya Studio za Fish Club zilizopo pande za Kariakoo, Dar es Salaam ameiambia ShowBiz kwamba kila kitu kizuri anachokifanya hivi sasa katika game ya muziki wa kizazi kipya kinatokana na mapenzi ya marehemu mama yake, Christopher Lissa alicheki naye.

Mchizi alisema kuwa, utundu wake katika ishu za muziki ulitokana na malezi mazuri aliyoyapata kwa mama yake huyo ambaye alipenda mwanawe aoneshe kipaji chake na kukitumia kama kazi.

“Japokuwa mama hayupo duniani lakini namshukuru kwa kunifikisha hapa nilipo. Alinipenda na nilimpenda. Alinipa muongozo mkubwa kimaisha ikiwemo uhuru wa kuchagua fani niipendayo, leo hii naonekana niko juu kwasababu ya mapenzi yake,” alieleza Lamar ambaye ndani ya studio anayofanyia kazi ametundika picha ya marehemu mama yake ukutani ikiwa ni ishara ya kumuenzi.
*******



Madee: Pesa imewatenganisha Matonya na Tunda
Kiukweli ni mmoja kati ya wasanii ambao hawajawahi kufanya vibaya katika kila ngoma anayotoa akitumia staili yake ya huzuni huzuni, kama ilivyo kunako kazi yake mpya, ‘Pesa’ iliyomshirikisha mkali wa kulalamika, Tundaman.

Namzungumzia kijana Hamad Ally a.k.a Madee, anayependa aitwe Rais wa Manzese ambaye hivi karibuni amedondoka na ngoma hiyo ambayo mashairi yake yanazungumzia ukweli wa mambo fulani yaliyowahi kumkuta yeye na wasanii wenzie waliopo kwenye mradi wa muziki wa kizazi kipya.

“Pesa zimewafanya Matonya na Tunda wachuniane, pesa zilimfanya TID akafungwa jela, pesa zilimfanya demu wangu avue pete ya uchumba na kusepa kwa mwanaume mwingine,” hayo ni baadhi ya maneno ya ukweli ambayo yapo ndani ya ngoma hiyo, ‘Pesa’,” alisema Madee.
********

Thursday, June 18, 2009

BINADAMU HATUKUUMBWA TUUGUWE

You are what you eat
SIDHANI kama utabisha ukiambiwa kuwa binadamu hatukuumbwa ili tuuguwe, iwe malaria, kisukari, presha, saratani, uti wa mgongo au ugonjwa wowote unaoujua wewe.

Mungu alituumba tukiwa na afya njema na alitaka tuendelee kuwa na afya njema katika maisha yetu yote. Lakini alituwekea pia sheria za mwili (physical laws) za kufuata ili tuishi hivyo alivyokusudia, sheria hizo, ambazo ni sheria za afya, zinapokiukwa ndipo tunapougua!

Kwa wengine jibu linaweza kuwa rahisi kuwa; ni mipango ya Mungu-binadamu huwezi kuishi bila kuugua! Pengine ni sawa, lakini elewa kwamba kila ugonjwa una sababu ambayo mara nyingi hutokea pale sheria za afya alizotuwekea Mungu ili tuzifuate, zinapokiukwa. Iwe kwa makusudi au kwa kutokujua. Ili kuilewa dhana hii, tunahitaji kujiuliza swali lifuatalo:

KWA NINI TUNAUGUA?
Ugonjwa unapotokea, huwa ni jitihada za asili za mwili inazozifanya ili kuuweka huru mfumo wake baada ya kutokea kwa ukiukwaji wa sheria za afya. Hii ina maana kwamba;

1. Dalili za ugonjwa, kama vile(maumivu, homa, uvimbe, n.k) hujitokeza pale mwili unapotaka kujiponya wenyewe.
2. Na kwamba, magonjwa hutokea kwa sababu ya kukiuka sheria za mwili alizotutungia Mungu.

DALILI ZA UGONJWA ZAWEZAJE KUWA JITIHADA ZA MWILI KUJITIBU?
Unapopatwa na ugonjwa au maumivu katika mwili wako, hiyo huwa ni njia inayotumiwa na mwili kujaribu kufikisha taarifa kuwa kuna kitu hakiko sawa ndani, hivyo hatua ya haraka inapaswa kuchukuliwa.

VIPI UGONJWA NI MATOKEO YA KUKIUKA SHERIA ZA MWILI?
Mara zote utakapokwenda hospitali ukiwa na tatizo la kiafya, utaambiwa ugonjwa unaokusumbua kisha utapewa dawa, ni mara chache sana unaweza kuelezwa sababu za ugonjwa wako na njia za kufuata ili ujikinge nao siku nyingine. Pengine ni kwa sababu za kibiashara!

Katika hali halisi, maradhi ni matokeo ya uchaguzi wetu wenyewe na sababu zinazosababisha maradhi hayo zinazuilika. Vijidudu vinavyosababisha magonjwa mbalimbali mwilini ni sawa na ndege wala mizoga (Scavengers), ambao huonekana sehemu yenye mizoga na sehemu ambayo hakuna, kamwe huwezi kuwaona.

Vivyo hivyo kwa vijidudu vya maradhi, mwili ambao ni mchafu na usiyo na kinga ndimo huwa makazi yao na kamwe hawawezi kuweka makazi katika mwili msafi na wenye kinga ya kutosha.

Aidha, inaelezwa kwamba vijidudu kama bakteria, virusi au minyoo, siyo ndiyo chanzo cha msingi kinachosababisha maradhi, bali ni matokeo ya kuwepo kwa maradhi. Mwana nadharia ya ‘Germ’, Dk. Pateur anaufananisha uhusiano wa vijidudu na mwili kama uhusiano wa mbegu na udongo kwa kusema “mbegu si lolote, ardhi ndiyo kila kitu,” akiwa na maana kwamba mbegu haiwezi kumea sehemu ambayo udongo hauna rutuba.

Hii ina maana kwamba vijidudu vinavyosababisha maradhi huweza kufanya hivyo pale vinapoingia mwilini na kukuta mwili mchafu na hauna kinga ya kutosha. Pale penye kinga imara na mwili msafi, vijidudu hivyo huwa havina nguzu na hufa vyenyewe ndani ya muda mfupi bila mtu kutumia aina yoyote ya dawa.

Sheria za mwili zilizoandikwa na Mungu, ziko kila mahali, kuanzia kwenye mishipa, misuli, damu na mifumo yote ya mwili tuliyopewa naye. Mungu aliweka utaratibu tunaopaswa kuufuata katika kudhibiti mavazi yetu, staili zetu za maisha, hamu yetu ya kula na jinsi tunavyopenda.

Baada ya Mungu kutuwekea utaratibu huo wa maisha, sisi hatuna budi kuufuata. Katika kutekeleza utaratibu wake, wapo tunaofuata na wapo tusiozifuata, hili ndilo linaloamua hali za afya zetu pia. Maradhi au afya njema tulizonazo, zina uhusiano wa moja kwa moja na kufuata au kutokufuata kwa sheria za afya za asili zilizowekwa na Mwenyezi Mungu.

Itaendelea wiki ijayo.

Wednesday, June 17, 2009

PALIKUWA HAPATOSHI!



Ras Makunja na kikosi chake cha kutuliza ghasia Ngoma Africa Band aka FFU aka wazee wa kukaanga mbuyu, siku ya Jumapili 14-06-2009 jioni mzimu wa mziki wa dansi wa bongo, ulifanikiwa kuziteka nyoyo za washabiki katika maonyesho makubwa ya mziki ya kimataifa Masala World Beat Festival, mjini Hannover, Ujerumani.

Majira ya saa 12 jioni Ras Makunja aka "Bw.Kichwa Ngumu" alikioongoza jukwaani Kikosi cha The Ngoma Africa band, kilichokuwa kimesheheni wanamziki washambuliaji akiwamo yule mchawi wa solo Christian Bakotessa aka Chris-B,Pia kulikuwa na mwanamziki mgeni mwalikwa Mr.Buti Jiwe ambaye alikuwa (Guest Artist), wengine alikuwapo yule mwadada anaekwenda samba samba na wanamziki wa kiume katika kushambulia jukwaa Dada Severn Onkomo aka Sevasha.

Kiongozi wa bendi hiyo Ebrahim Makunja aka ras Makunja alikiamrisha kikosi chake nacho bila kuremba remba kilianza kuporomosha mziki mkali ambao mdundo wao huo wa bongo dansi aliwazidi nguvu washabiki na dakika chache washabiki walidata ! na kujikuta wapo katika Kindumbwe Ndumbwe cha na Nguo Kuitia moto!

Wataalamu wa mziki na maporomota walikuwa roho juu kila moja akiwa anataka kufanya kazi na bendi hiyo ambayo imetajwa kuwa ni "mzimu wa mziki wa dansi." watayarishaji wa onyesho hilo wamesema haijawi kutokea katika historia ya maonyesho hayo kuwa "Mziki wa dansi wa kiafrika" kuwadatisha washabiki kwa kasi kubwa ! Wamesema mziki wa The Ngoma Africa Band una nguvu isiyo ya kikawaida!

Bendi hiyo ipo katika medani ya dansi kwa muda wa miaka 16, sasa na imefanikiwa kulitangaza dansi la bongo na kujinyakulia nafasi ya pekee za kimataifa Wasikilize hapa www.myspace.com/thengomaafrica pia ukiwataka wasiliana nao at: ngoma4u@ngomaafrica

Tuesday, June 16, 2009

KAMATA MCHUMA!




INAUZWA: Gari aina ya Nissan Rasheen

ex - Japan, ipo katika hali nzuri, inatembea.

Mawasiliano: 0715-110 173

BEI: Tshs: 5 Mil Tu!

Au fika Sinza, Bamaga ili uione na kuijaribu.

Monday, June 15, 2009

WIKIENDA SHOWBIZ!


Diddy:mademu 17 akiwemo wa mshikaji wake B.I.G
Mkali wa Hip Hop laini, Sean John Combs mwenye a.k.a kibao, Diddy, P Diddy Puffy au Dippy ndiye tunamcheki leo kwenye ‘Ebwana Dah!’ yakiwa ni maombi ya baadhi ya wasomaji wa safu hii. Kama ilivyo kwa mastaa wengine waliopita, mchizi pia ameonesha kuwa na listi ndefu ya mastaa wa kike aliyowahi kushirikiana nao kunako ‘malove dave’.

Kwa mujibu wa mtandao unaodili na ishu hizi na kama ulikuwa haufahamu, Diddy amewahi kujiachia na mwana Hip Hop wa kike, Lil Kim ambaye pia alikuwa mpenzi wa rafiki yake mkubwa, marehemu Notorious B.I.G. Mbali na Kim mchizi alianza kutoka na mwanadada Carmen Bryan, kisha Karrine Steffans na baadaye Misa Hylton-Brim aliyedumu naye kwa miaka miwili, 1993-1995.

Mwaka 1996, Diddy aliendeleza ‘malove dave’ kwa kutoka na Kim Porter ambaye alifanikiwa kuzaa naye mtoto wa kwanza, kabla ya mapacha wawili wa kike aliowapata hivi karibuni baada ya kurudiana naye. Kabla ya mapacha hao jamaa alimshiti Kim na kudondokea kwa Jennifer Lopez (1998-2001), Alicia Douvall (2002), Naomi Campbell (2002 - 2003), Sarah Chapman (2004 - 2006) na Aubrey O`Day (2005 - 2006).

Warembo wengine aliyowahi kutoka nao ni Alexandra Cheron (2006), Diana Bianchi (2006), May Andersen (2007), Sienna Miller (2007) Cassie Ventura (2008) na Caroline D`Amore (2008). Diddy ambaye nyota yake ni Nge, akiwa na urefu wa futi tano na nchi tisa ambazo ni sawa na sentimita 175 alizal-iwa Novemba 4, 1969 huko Harlem, New York, Marekani. Mbali na kuimba pia ni mtayarishaji muziki kupitia lebo yake, Bad Boys Entertainment.
***********************
Dudubaya: Wazungu wampa ulaji
Baada ya kutulia kwa muda mrefu bila kujihusisha na ishu yoyote ya ukorofi kama alivyokuwa akifanya siku za nyuma, msanii Godfrey Tumaini a.k.a Ze Dudu, ameibukia kunako safu hii na kutamka kwamba, cheo cha umeneja alichopewa kwenye Kampuni ya Art in Tanzania kimemfanya awe na nidhamu ya kutosha, Richard Bukos alipiga nae stori.

Dudu aliyasema hayo usiku wa kuamkia Juni 13, mwaka huu ndani ya Ukumbi wa TTC Chang’ombe, Dar es Salaam ambapo kampuni yake ilikuwa imedhamini kinyang’anyiro cha kumtafuta Miss Chang’ombe 2009 kilichofanyika katika ukumbi huo.

“Kutokana na nafasi niliyonayo kwenye kampuni hiyo, nitawashangaza sana mabosi wangu ambao wengi ni watasha kama nitafanya ishu za ukorofi ambayo ni mambo ya kizamani,” alisema Dudu.

Aidha, msanii huyo alisema kwamba, siku hizi hata kwenye kumbi za burudani amepunguza kwenda labda kama atakuwa amealikwa kwasababu ya shoo, siyo kuibuka bila mpango wowote kama ilivyokuwa zamani.

Ze Dudu ambaye ametamba kuvuta mkwanja mrefu kwenye kampuni hiyo, amesema kuwa staili yake ya kufanya muziki hivi sasa ni kutoa ngoma moja moja tu, hana mpango wa kugonga albamu kwakuwa singo inapokuwa bomba shoo utakazoalikwa zinalipa kuliko kuhangaika na maandalizi ya albamu.
**************************

Suma Lee, Fid Q, Josline ndani ya Mpo Afrika
Kutoka ndani ya mradi wa muziki wa kizazi kipya ambao kuna tetesi kwamba kila kukicha unazidi kupoteza muelekeo, safu hii ilipata kupiga stori na msanii Ismail Seif a.k.a Suma Lee na kugundua kwamba pamoja na hilo kila kukicha baadhi ya watu wamekuwa wakifungua studio mpya, Rhobi Chacha anashuka nayo.

Suma alisema na safu hii kwamba baadhi ya kazi zitakazokuwa ndani ya albamu yake zimefanyika kupitia Studio za Mpo Afrika zilizopo pande za Tandika Davis Corner, Dar es Salaam kitu ambacho kiliifanya safu hii ibaini kwamba kuna studio mpya yenye jina hilo.

“Lakini pamoja na upya wa studio hiyo jamaa wako safi kuanzia prodyuza wao, Benny Msama hadi vyombo vya kisasa wanavyotumia. Ongezeko la studio hapa Bongo litazidi kuleta changamoto kwetu sisi wasanii,” alisema Suma.

Safu hii pia ilimuendea hewani Prodyuza wa studio hiyo, Benny ambaye alisema kwamba, siyo Suma Lee tu bali wasanii kibao wakiwemo Josline, Fid Q, Juma Jazz na wengine wameshapiga nao kazi.
****************************
Miss Dar City Centre hukumu imekaribia
Warembo wanaowania taji la Miss Dar City Centre ambao hukumu yao ni Juni 26, mwaka huu wameelezewa kuwa na viwango vya hali ya juu kuanzia elimu, uelewa na uzuri hali ambayo inawapa matumaini waandaaji wa kinyang’anyiro hicho ya kutoa Miss Tanzania mwaka huu, Christopher Lissa anashuka nayo.

Mratibu wa shindano hilo, John Doto kutoka Kampuni ya Sisi Entertainment, ameliambia Ijumaa Wikienda hivi karibuni kwamba, tangu warembo hao walipotinga kambini kumekuwa na mchujo mkali wa kuwasukuma nje ya shindano wasichana ‘vimeo’.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha Miss Ilala, Miss Tanzania na Miss World 2009 anatokea Dar City Centre.

Aliongeza kuwa, tayari maandalizi ya ujenzi wa jukwaa la kisasa kwa ajili ya shindano hilo litakalofanyika Juni 26, 2009 kwenye Ukumbi wa Lamada limeanza kuandaliwa huku wananchi kibao wakijotokeza kushuhudia mazoezi ya walimbwende hao.

Kwa upande wa zawadi, Doto alisema: “Tutatangaza wiki moja kabla ya fainali kufanyika. Tumeandaa zawadi nono ambazo nina hakika zitawavutia wengi.

“Lakini nitoe wito kwa wananchi na wadau wote wa masuala ya ulimbwende kujitokeza kwa wingi ndani ya Hoteli ya Lamada iliyopo Ilala siku ya Juni 26 kuja kumlaki Miss Dar City Centre ambaye baadaye atakuwa Miss Ilala, kisha Miss Tanzania na hatimaye Miss World.”
***********************