Thursday, June 18, 2009

BINADAMU HATUKUUMBWA TUUGUWE

You are what you eat
SIDHANI kama utabisha ukiambiwa kuwa binadamu hatukuumbwa ili tuuguwe, iwe malaria, kisukari, presha, saratani, uti wa mgongo au ugonjwa wowote unaoujua wewe.

Mungu alituumba tukiwa na afya njema na alitaka tuendelee kuwa na afya njema katika maisha yetu yote. Lakini alituwekea pia sheria za mwili (physical laws) za kufuata ili tuishi hivyo alivyokusudia, sheria hizo, ambazo ni sheria za afya, zinapokiukwa ndipo tunapougua!

Kwa wengine jibu linaweza kuwa rahisi kuwa; ni mipango ya Mungu-binadamu huwezi kuishi bila kuugua! Pengine ni sawa, lakini elewa kwamba kila ugonjwa una sababu ambayo mara nyingi hutokea pale sheria za afya alizotuwekea Mungu ili tuzifuate, zinapokiukwa. Iwe kwa makusudi au kwa kutokujua. Ili kuilewa dhana hii, tunahitaji kujiuliza swali lifuatalo:

KWA NINI TUNAUGUA?
Ugonjwa unapotokea, huwa ni jitihada za asili za mwili inazozifanya ili kuuweka huru mfumo wake baada ya kutokea kwa ukiukwaji wa sheria za afya. Hii ina maana kwamba;

1. Dalili za ugonjwa, kama vile(maumivu, homa, uvimbe, n.k) hujitokeza pale mwili unapotaka kujiponya wenyewe.
2. Na kwamba, magonjwa hutokea kwa sababu ya kukiuka sheria za mwili alizotutungia Mungu.

DALILI ZA UGONJWA ZAWEZAJE KUWA JITIHADA ZA MWILI KUJITIBU?
Unapopatwa na ugonjwa au maumivu katika mwili wako, hiyo huwa ni njia inayotumiwa na mwili kujaribu kufikisha taarifa kuwa kuna kitu hakiko sawa ndani, hivyo hatua ya haraka inapaswa kuchukuliwa.

VIPI UGONJWA NI MATOKEO YA KUKIUKA SHERIA ZA MWILI?
Mara zote utakapokwenda hospitali ukiwa na tatizo la kiafya, utaambiwa ugonjwa unaokusumbua kisha utapewa dawa, ni mara chache sana unaweza kuelezwa sababu za ugonjwa wako na njia za kufuata ili ujikinge nao siku nyingine. Pengine ni kwa sababu za kibiashara!

Katika hali halisi, maradhi ni matokeo ya uchaguzi wetu wenyewe na sababu zinazosababisha maradhi hayo zinazuilika. Vijidudu vinavyosababisha magonjwa mbalimbali mwilini ni sawa na ndege wala mizoga (Scavengers), ambao huonekana sehemu yenye mizoga na sehemu ambayo hakuna, kamwe huwezi kuwaona.

Vivyo hivyo kwa vijidudu vya maradhi, mwili ambao ni mchafu na usiyo na kinga ndimo huwa makazi yao na kamwe hawawezi kuweka makazi katika mwili msafi na wenye kinga ya kutosha.

Aidha, inaelezwa kwamba vijidudu kama bakteria, virusi au minyoo, siyo ndiyo chanzo cha msingi kinachosababisha maradhi, bali ni matokeo ya kuwepo kwa maradhi. Mwana nadharia ya ‘Germ’, Dk. Pateur anaufananisha uhusiano wa vijidudu na mwili kama uhusiano wa mbegu na udongo kwa kusema “mbegu si lolote, ardhi ndiyo kila kitu,” akiwa na maana kwamba mbegu haiwezi kumea sehemu ambayo udongo hauna rutuba.

Hii ina maana kwamba vijidudu vinavyosababisha maradhi huweza kufanya hivyo pale vinapoingia mwilini na kukuta mwili mchafu na hauna kinga ya kutosha. Pale penye kinga imara na mwili msafi, vijidudu hivyo huwa havina nguzu na hufa vyenyewe ndani ya muda mfupi bila mtu kutumia aina yoyote ya dawa.

Sheria za mwili zilizoandikwa na Mungu, ziko kila mahali, kuanzia kwenye mishipa, misuli, damu na mifumo yote ya mwili tuliyopewa naye. Mungu aliweka utaratibu tunaopaswa kuufuata katika kudhibiti mavazi yetu, staili zetu za maisha, hamu yetu ya kula na jinsi tunavyopenda.

Baada ya Mungu kutuwekea utaratibu huo wa maisha, sisi hatuna budi kuufuata. Katika kutekeleza utaratibu wake, wapo tunaofuata na wapo tusiozifuata, hili ndilo linaloamua hali za afya zetu pia. Maradhi au afya njema tulizonazo, zina uhusiano wa moja kwa moja na kufuata au kutokufuata kwa sheria za afya za asili zilizowekwa na Mwenyezi Mungu.

Itaendelea wiki ijayo.

No comments: