Friday, June 19, 2009

IJUMAA SHOWBIZ!

Shaa: Nina zawadi kutoka kwa Jide
Kutoka pande za Masaki, Dar es Salaam anakofanyia kazi zake kupitia Studio za MJ Records, msanii wa bongo flava anayesumbua stejini, Sarah Kaisi a.k.a Shaa amesema na ShowBiz kwamba mwanadada Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ amemzawadia wimbo mmoja mkali baada ya kuvutiwa na kazi anazofanya, Edna Katabalo anajiachia nayo.

Ndani ya safu hii, Sara alisema kwamba, ngoma hiyo ambayo hakuwa tayari kuitaja jina hivi sasa anaifanyia mazoezi ya nguvu ili atakapoingia studio atoke na kitu cha nguvu ambacho kitamfanya Lady Jaydee afurahi na kuamini kwamba zawadi hiyo ameidondosha mahali pake.

“Niliifurahia zawadi hiyo kutoka kwa dada Judith kwani ni heshima ya pekee aliyonipatia, ukizingatia kwamba wapo wasanii wengi ambao wanafanya vizuri katika muziki wetu lakini kaamua kuniandikia wimbo mimi na siyo wengine,” alisema Shaa ambaye hivi sasa anapoteza na ngoma zake mbili, ‘Zamu yangu’ na ‘Pambazuko’ ambao kampa shavu Ambwene Yesaya ‘A.Y’.
********
Chid Benz

Yakuza Mob

Chid Benz, Yakuza ndani ya Beach Party
Msanii Rashid Makwilo a.k.a Chid Benz ni miongoni mwa wakali wa Bongo Flava watakaowakilisha kwenye tamasha maalum la ufukweni lililopewa jina la ‘Beach Party Concert’ litakalogongwa Juni 27, mwaka huu pande za Maeese Beach, Kigamboni.

Akipiga stori na ShowBiz mratibu wa tamasha hilo, George Mushi ‘G-Body’ alisema kwamba, ishu hiyo ni maalum kwa ajili ya kuwakutanisha vijana wenye umri tofauti ili waweze kubadilishana mawazo.

“Mbali na Chid Benz, wasanii wengine watakaopiga shoo siku hiyo ni pamoja na Stopper Rhymes, Nemo, PNC, Hemed, Yakuza Mobb na Wa-Don Town, huku JS’s Entertainment wakiangusha disko la ukweli,” alisema George.
*********
Bobby Wine akiwa na AY (kulia)
Chamelione (kushoto) akiwa na Bebe Cool
Bob Wine, Bebe Cool wazigonga
Kutoka pande za Uganda au ‘UG’, ShowBiz iliinyaka ishu kwamba, mastaa wawili wa muziki, Bebe Cool na Boby Wine hivi karibuni walichapana makonde hadharani kiasi cha kuumizana vibaya, Christopher Lissa anashuka nayo.

Chanzo chetu cha habari kutoka nchini humo kilisema kwamba, mastaa hao wenaopewa heshima kubwa nchini humo na Afrika Mashariki kwa ujumla, walipeana mikono hiyo kwenye ‘konseti’ moja kubwa la muziki lililosababishwa kunako Jiji la Kampala.

“Chanzo cha ugomvi huo inasemekana kuwa ni baada ya Boby Wine kumshutumu Bebe Cool kuwa amemkashifu kwenye baadhi ya nyimbo zake. Sakata hilo limesababisha Bebe Cool kuumia vibaya na kulazwa katika Hospitali ya Mulago iliyopo Kampala,” kilisema chanzo hicho.

Akihojiwa na kituo kimoja cha Televisheni nchini humo, Boby Wine alikiri kumchapa Bebe Cool huku akijifagilia kwamba yeye ni mwanamasumbwi mzoefu (japo ajawahi kupanda ulingoni).

Kufuatia tukio hilo, Boby Wine ambaye anamiliki jumba kubwa na magari ya kifahari nchini humo, ameingizwa kwenye orodha ya wasanii wakorofi kwani hivi karibuni aliingia kwenye mzozo mkali na Halmashauri ya jiji hilo, uliosababisha aburuzwe mbele ya Pilato katika mahakama moja akituhumiwa kujenga nyumba kwenye eneo lisiloruhusiwa.
*******
Lamar

Marehemu mama Lamar
Kila ninachofanya ni sababu ya mama
Prodyuza Lamar kutoka ndani ya Studio za Fish Club zilizopo pande za Kariakoo, Dar es Salaam ameiambia ShowBiz kwamba kila kitu kizuri anachokifanya hivi sasa katika game ya muziki wa kizazi kipya kinatokana na mapenzi ya marehemu mama yake, Christopher Lissa alicheki naye.

Mchizi alisema kuwa, utundu wake katika ishu za muziki ulitokana na malezi mazuri aliyoyapata kwa mama yake huyo ambaye alipenda mwanawe aoneshe kipaji chake na kukitumia kama kazi.

“Japokuwa mama hayupo duniani lakini namshukuru kwa kunifikisha hapa nilipo. Alinipenda na nilimpenda. Alinipa muongozo mkubwa kimaisha ikiwemo uhuru wa kuchagua fani niipendayo, leo hii naonekana niko juu kwasababu ya mapenzi yake,” alieleza Lamar ambaye ndani ya studio anayofanyia kazi ametundika picha ya marehemu mama yake ukutani ikiwa ni ishara ya kumuenzi.
*******



Madee: Pesa imewatenganisha Matonya na Tunda
Kiukweli ni mmoja kati ya wasanii ambao hawajawahi kufanya vibaya katika kila ngoma anayotoa akitumia staili yake ya huzuni huzuni, kama ilivyo kunako kazi yake mpya, ‘Pesa’ iliyomshirikisha mkali wa kulalamika, Tundaman.

Namzungumzia kijana Hamad Ally a.k.a Madee, anayependa aitwe Rais wa Manzese ambaye hivi karibuni amedondoka na ngoma hiyo ambayo mashairi yake yanazungumzia ukweli wa mambo fulani yaliyowahi kumkuta yeye na wasanii wenzie waliopo kwenye mradi wa muziki wa kizazi kipya.

“Pesa zimewafanya Matonya na Tunda wachuniane, pesa zilimfanya TID akafungwa jela, pesa zilimfanya demu wangu avue pete ya uchumba na kusepa kwa mwanaume mwingine,” hayo ni baadhi ya maneno ya ukweli ambayo yapo ndani ya ngoma hiyo, ‘Pesa’,” alisema Madee.
********

2 comments:

Anonymous said...

Nasikia matonya alikuwa anatungiwa nyimbo na tunda man.

Rashid Mkwinda said...

Duuu kamanda mambo vp, blogu yako imetulia,Bg up Maan!!! karibu kijijini kwangu, tunaweza kushare uzoefu(mkwinda.blospot.com)