Tuesday, May 18, 2010

Blogu Ya Jamii Yapiga Hatua Nyingine Kadhaa Katika Kuendeleza Libeneke



Asalaam Aleikhum,
Bwana Asifiwe,
Tumsifu Bwana,
Shalom,
Namaste,
konnichiwa,
Nihao,
olá
Shikamooni
Mambo?

KWA heshima na taadhima nawaamkia wadau wote popote mlipo ulimwenguni. Salamu nilizotoa hapo juu naomba ifahamike kuwa hizo nilizozimudu ni kama kielelezo kwamba nia ni kumuamkua kila mmoja kwa nafasi yake popote alipo. Mie sijambo na naendelea vyema na Libeneke kama kawaida.

Waama, baada ya salamu, napenda kuwafahamisha kwamba Globu ya Jamii hivi karibuni itaingia kwenye awamu mpya ya dot com. Hii ni katika jitihada za kuboresha Libeneke liendelee mbele zaidi.

Imechukua muda kuchukua hatua hii kutokana na mazoea kwani toka September 8, 2005 hadi leo si kidogo ati. Hivyo mabadiliko kama yapo inabidi yafanywe kwa uangalifu wa hali ya juu ili kutoleta usumbufu wa aina yoyote kwa wadau wa Globu ya Jamii ambao kwangu ndiyo waajiri wangu wakuu.

Naam, wakati wowote kuanzia sasa libeneke la
issamichuzi.blogspot.com litaingia katika awamu ya www.imichuzi.com. unakaribishwa kujaribu na kutoa maoni yako.

Mabadiliko haya tayari yameshafanyiwa kazi na sasa yako katika hatua za nchani. Kilichosalia ni kuhamisha 'mzigo' wote wa miaka takriban mitano toka
issamichuzi.blogspot.com na kuutua katika www.imichuzi.com ili libeneke liendelee vile vile kama ilivyo siku zote - ukaicha mabadiliko kiasi ya muonekano.

Ni kweli jina litabaki lile lile la 'MichuziBlog' na 'Globu ya Jamii' lakini si uwongo kwamba hivi sasa itakuwa tovuti kamili ila katika sura ya globu kama siku zote. Hii yote ni katika juhudi za kuongeza ufanisi, tija na vionjo vingi zaidi pamoja na kuondoa kero ya kusaka mitundiko iliyopita. Nadhani sasa itaeleweka kwa nini kulikuwa na kwikwi katika kutafuta posti za zamani.

Mdau usihofu kwamba labda utapata shida kusaka
www.imichuzi.com. La, hasha. hautopata shida kwani hata kama utaingia Globu ya Jamii kwa kutumia issamichuzi.blogspot.com ama hata kwa kutumia 'michuzi' pekee utapelekwa moja kwa moja kwenye kurasa mpya bila matatizo. Isitoshe, posti zitabakia kwenye ukurasa wa mwezi husika na kuingia kwenye 'archive' baada ya mwezi huo kwisha.

Hivyo basi, kwa unyenyekevu mkubwa naomba niwashukuru wadau wote popote mlipo kwa kampani yenu wakati wote huu ambayo kwa kweli bila nyie Libeneke lisingefikia hapa lilipo, hususan katika wakati huu wa kulifanya bora zaidi. Na kwa unyenyekevu huo huo naomba tuendelee kushirikiana kwa hali na mali, sera ikiwa ile ile ya "sibagui, sichagui; atayenizika simjui"

Maoni, ushauri na mawazo vinakaribishwa kwa mikono miwili, pasina kusahau kukosoana kwa kujenga na mawazo mbadala ili kieleweke na Libeneke liendelee mbele kwa ufanisi zaidi zaidi na zaidi.

Kwa kuwa nawapenda wadau wote, nitakuwa mtovu wa fadhila endapo kama sintowaonjesha Libeneke litalokuja kwa muonekano mpya. Hivyo basi ni ruksa kubofya http://www.imichuzi.com/ na kuangalia ni nini kinaendelea.

Hapo hapo naomba radhi kwa usumbufu wowote utaotokea kwani kama inavyofahamika si rahisi kwa binadamu kuwa sahihi kwa kila jambo. Hivyo n penye kwikwi na tusameheane na tushtuane haraka iwezekanavyo kupitia anuani ile ile ya issamichuzi@gmail.com ambayo nayo itabadikika mambo yakikaa sawa muda si mrefu ujao itakuwa info@imichuzi.com


Angalizo: Wakati tukielekea huko kwenye http://www.imichuzi.com/ libeneke hapa litaendelea kama kawaida na hakutakuwa na mabadiliko yoyote hadi siku utapokuta unapelekwe huko. Na hii itafanyika wakati wowote kuanzia sasa.
Na wale Wadau 100 walioshinda katika ule mtanange wa mdau wa milioni 8 na mnaotakiwa kupata ze fulanazzz za Blobu ya Jamii kaeni mkao wa kula, maana zilisitishwa kusubiri anwani mpya. Wala Msikonde email zenu zote zipo kibindoni na nyote mtafurahi. Fanyeni subira kidogo na samahani kwa kuchelewa kwa hilo

Shukrani za pekee zifike kwa
wanaowezesha yote haya na memngine mengi tu.
Asante sana MK
Wenu mtumishi mtiifu,
Muhidin Issa Michuzi

No comments: