Monday, September 13, 2010

WIKIENDA SHOWBIZ!

Tupac: Dunia kumkumbuka leo, miaka 14 ya kifo chake, hasahauliki, ni nembo ya mapinduzi ya Mwafrika

Tarehe kama leo mwaka 1996, mchawi wa mauzo katika Hip Hop duniani, Tupac Amaru Shakur alifariki dunia baada ya kuishi duniani miaka 25 tu.

Alifariki dunia baada ya kutawala ‘game’ kwa miaka 6 mfululizo lakini kazi yake imeendelea kumuweka chati ya juu mpaka leo. Wachambuzi wengi wanapendekeza Tupac a.k.a Makavelli The Don kuwa Mfalme wa Hip Hop Duniani wa muda wote.

Tupac anapewa cheo hicho kwa kutazama vitu vingi, tungo zake zilivyobamba, mapinduzi makubwa aliyoyafanya katika Hip Hop, jinsi alivyoweza kubadili vijana wengi Marekani ambao waliishi kwa itikadi zake lakini yote kwa yote, Tupac a.k.a King Killuminat anasimama kuwa mtetezi wa haki za binadamu.

Alikuwa na kipaji kikubwa, aliweza kurap kila kitu alichohitaji, alipoamua kuimba jiwe aliandika mashairi yanayojitosheleza na kukuvutia usikilize. Staili yake ngumu imebaki kumuweka wa kipekee, kwani wengi wamejitahidi kumuiga wameshindwa.

Uwezo wake wa kuandika mashairi siyo tu ulitokana na kipaji, bali pia ulinolewa na shule. King Makaveli baada ya kumaliza Paul Laurence Dunbar High School, alipelekwa na mama yake kwenda kusomea sanaa Baltimore School for the Arts ambako alijifunza kuigiza, kuandika mashairi, staili ya Jazi na kucheza kwa kuigiza bila kutoa sauti (ballet).

Alivyorap kiitikio cha Hit em Up imebaki mtihani hata kwa mastaa wakubwa wa Hip Hip wa sasa, wengi wamejaribu wameshindwa lakini inaaminika Eminem peke yake ndiye anayeweza. Alikuwa mwana Hip Hop aliyefungua njia kwa wengine kwa kukamata namba moja mfululizo kila alipotoa rekodi zake.

Gazeti la Blender lilifanya tathmini na kumtaja Tupac kwamba ndiye mtu anayeheshimiwa zaidi kwenye muziki duniani (Most Overrated Person in Music). Maajabu yake makubwa ni kwamba aliuza nakala nyingi baada ya kufa kuliko akiwa hai, hii imetokana na hazina ya mamia ya nyimbo alizoacha amerekodi studio lakini akafa kabla hajaziachia.

Ameuza zaidi ya nakala milioni 75 duniani na hiyo imemuweka kwenye kundi la wanamuziki bora kwa mauzo duniani. Katika Hip Hop anashikilia nafasi ya pili nyuma ya Eminem, lakini Pac anapewa heshima kwa sababu alifanya muziki kwa muda mfupi mno.

Akina Jigga, P Diddy na wengineo licha ya kuishi muda mrefu kwenye muziki lakini hawajaingia kwenye rekodi ya kuuza. Walikuwepo wakati Pac akitawala soko la Hip Hop enzi za uhai wake na ameendelea kuwapiga bakora sokoni akiwa kaburini.

Sifa kuu ya Tupac ni kwamba hajawahi kuharibu sokoni, albamu zote akiwa hai ziliuza Gold na Platinum. Ni albamu moja tu ya mwaka 2006, iliyotoka miaka 10 baada ya kifo chake “Pac’s Life” ndiyo haikufikia hadhi ya Gold lakini zilizotangulia alifumua Multi-Platinum za kutisha. “Alistahili kila alichopata. Umaarufu na fedha.

Alikuwa milionea akiwa kijana mdogo (miaka 19), alistahili kwa sababu kichwa chake ni madini,” hii ni comment iliyotolewa na mdau wa muziki kusindikiza kifo cha mwanamuziki huyo. Kuna wanaoamini kuwa mapinduzi ya Tupac kwa kumtetea mtu mweusi Marekani hasa kupitia albamu yake ya kwanza ya mwaka 1991 (2Pacalypse Now) yana maana kubwa kuliko hata maajabu ya Barack Obama kuchaguliwa kuwa Rais wa taifa hilo kubwa duniani. Kwamba Tupac alibadili fikra za watu, akawapandisha watu mizuka na kuishi kwa itikadi zake.


SAFARI YA KIFO: Septemba 7, 1996, Tupac alihudhuria onesho la ndondi la Mike Tyson na Bruce Seldon kwenye Ukumbi wa MGM Grand, Las Vegas. Picha za mwisho zinamuonesha akikumbatiana na Tyson baada ya pambano. Baadaye wakiwa MGM, mpambe wa prodyuza wa Pac, Suge Night alimwambia Pac kwamba Orlando Anderson ‘Baby Lane’ alikuwepo ukumbini hapo.

Pac alimshambulia Anderson ambaye alikuwa memba wa Kundi la Southside Crips kwa kushirikiana na Suge pamoja na wapambe wao. Walipotoka hapo walielekea Klabu ya Death Row inayoitwa 662 na alikuwa anaendeshwa na Suge kwenye gari aina ya BMW 75il sedan 1996 (toleo jipya kwa wakati huo).

Walikuwemo pia wapambe kibao. Saa 4:55 usiku gari likiwa limesimama kwenye taa nyekundu za barabarani, Tupac alishusha kioo akapigwa picha na ‘kameramani’ aliyemwomba. Kati ya saa 5:00–5:05 usiku, walikamatwa Las Vegas Blvd na polisi wa pikipiki kwa kuendesha gari wakiwa wameweka sauti kubwa na kutokuwa na leseni ambayo baadaye ilipatikana, hivyo wakaachiwa bila faini yoyote.

Saa 5:10 usiku walisimama kwenye taa nyekundu kwenye Barabara ya Flamingo, Tupac alisimama kupitia rufu ya gari na kuzungumza na warembo wawili kwenye gari nyingine, akawaalika Klabu 662. Saa 5:15 usiku gari toleo la zamani aina ya Cadillac ambalo lilikuwa na namba isiyojulikana, lilishusha kioo usawa wa Tupac na kumshambulia kwa risasi kifuani. Moja ya risasi ilipiga kwenye pafu la kulia la Pac.

Alipelekwa Hospitali ya University Medical Center ambako alifariki siku sita baadaye (Septemba 13) baada ya upasuaji wa kubadilisha pafu lililoharibika kufeli. Miezi sita baadaye, yaani Machi 1997, Biggie naye aliuawa kwa risasi, shambulio ambalo linadaiwa kufanywa na watu wa Pac.


MAJIVU YAKE YAVUTIWA BANGI Tupac alianzisha Kundi la Outlawz Immortalz mwaka 1995 ambalo alilitumia kwenye matamasha yake pamoja na kulishirikisha katika kibao cha kihistoria, Hit em Up.
Mwili wake ulizikwa kwa kuchomwa. Kituko ni kwamba memba wa Outlwaz walichukua sehemu ya majivu yake na kuyachanganya na bangi ambazo walivuta kama kumpa heshima.

HESHIMA Marapa karibu wote wanamtukuza. Herford, Ujerumani kuna mnara wa heshima uliojengwa kwa sanamu la Tupac ili kumuenzi. Marekani pia mnara huo upo na una sanamu lake. Bishop Lamont katika kitabu chake How to Rap, aliandika: “Tupac alikuwa na kila kitu, heshima, matarijio, kipawa cha kurap.

Alikuwa juu mno.” Fedro Starr wa Kundi la Onyx alisema: “Tupac alikuwa masta wa kurap, hakuna wa kumfikia.” 50 Cent: “Kila rapa aliyekua miaka ya tisini ana kitu kuhusu Tupac. Alikuwa na kitu cha kipekee kuliko yeyote kabla yake.” The Game: “Tupac ni rapa bora duniani. Alikuwa na ataendelea kwa maisha yangu yote.” About.com uliandika kuwa Tupac ndiye rapa anayekubalika zaidi.

ALITOKA KIMAPENZI NA MADEMU 10
Warembo ambao Tupac alipokuwa hai alijivinjari nao kwa nyakati tofauti ni Arnelle Simpson, Jada Pinkett Smith, Jasmine Guy, Salli Richardson, Lisa Lopes ‘Left Eye’, Janet Jackson, Rosie Perez, Keisha Morris, Faith Evans (mke wa Biggie) na Kidada Jones ambao jumla yao ni 10.

NUKUU YA PAC
“Siwezi kusema kuwa naweza kuibadilisha dunia, ila nina uhakika kwamba nitapanda mbegu kwenye fikra za watu ambao wataibadilisha dunia.”

NANI ALIMUUA TUPAC?
Ni swali gumu kujibika na maumivu yanayoendelea ni kwamba hakuna hata mtu mmoja aliyeshikiliwa kwa kuhusika. Hata hivyo kuna watu wanabaki kutuhumiwa. Biggie Katika interview ya siku chache kabla Tupac hajauawa alisema kuwa alikuwa anachanganyikiwa na ‘ukigeugeu’ wa Tupac. Alisema:

“Hii inanichanganya kabisa, kwanza anasema, likimtokea lolote anamgeukia Mungu, mambo yakitulia anaongea tena. Inaniudhi, sasa nimeamua mimi na Junior M.A.F.I.A hatutaki tena majadiliano.”

Mbali na kauli hiyo, Biggie anahusishwa kwa sababu kwenye wimbo wake Who Shot Ya? Uliotoka baada ya Tupac kupigwa risasi mwaka 1994, anasikika akiponda kwamba mtu (Tupac) amepewa alichostahili na asicheze na wajanja wa Brooklyn. Wimbo huo ndiyo sababu ya Tupac kurekodi Hit em Up ambapo kiitikio anasema: “Nani alinishuti? Lakini takataka zenu hazikunimaliza.” Anaendelea:

“Nazidi kuwa juu, natengeneza mamilioni ya dola zaidi yenu.” Tupac ameeleza ndani kuwa alitoka kimapenzi na mke wa Biggie, Faith Evans pamoja na malaya wake ambao inadhaniwa anatajwa Lil Kim. Biggie alitajwa kuhusika kwa sababu ya uhasama wao wa muda mrefu, ishu ya mkewe na jinsi alivyoachwa ‘uchi’ kwenye Hit em Up lakini ushahidi haukutosha. Ikaonekana kuwa siku Tupac anapigwa risasi Las Vegas, Biggie alikuwa studio na Jay Z pamoja na kundi la Junior M.A.F.I.A ingawa inasemekana alilipa fedha nyingi kwa kikundi fulani ili kutekeleza mauaji.


Orlando Anderson
Huyu jamaa alipigwa na Tupac kwa kushirikiana na Marion ‘Suge’ Night kwenye Hotel ya MGM, lakini hakwenda kuripoti polisi, kwahiyo ikahisiwa kuwa si ajabu aliamua kulipa kisasi kwa staili hiyo.

Suge Night
Mtendaji Mkuu wa Death Row Records. Aliwekeza kiasi cha dola milioni 14 ili kuhakikisha Tupac anakuwa huru alipokuwa amefungwa gerezani mwaka 1995. Inadhaniwa alipanga njama za kumuua Tupac kwa sababu mwanamuziki huyo ndiye alikuwa anashikilia pumzi ya Death Row. Iliingiza mamilioni ya dola kwa rekodi za Tupac tu!
Kwanini anahisiwa alimuua?

Tupac alikuwa amekwisharekodi mamia ya nyimbo zilikuwepo studio, kwahiyo anadaiwa alimuua ili apate kumiliki utajiri wa nyimbo hizo. Aidha, ikaelezwa kuwa Tupac alikuwa na mpango wa kuanzisha kampuni yake ya muziki baada ya kumaliza mkataba na Death Row wa kurekodi albamu tatu ambao mwanamuziki huyo aliingia na Suge kufidia fedha alizotumia kumchomoa jela. Inaelezwa kwamba Suge alihofia Death Row ingekufa endapo Pac angejitoa.
P Diddy

Anatajwa kupitia mtiririko wa matukio ya kuanzia mwaka 1994. Alitajwa kwa sababu Bad Boy ilikuwa na upinzani na Death Row ambayo ilikuwa juu mno kwa wakati huo, kwahiyo inahisiwa kuwa Diddy aliweka mpango wa kumuua Pac kwa sababu ndiye mtu pekee aliyeipa Death Row jeuri ya kutamba Marekani na dunia nzima katika Hip Hop, kwahiyo aliamini Pac akifa Bad Boy itatawala.

WAZAZI WA BIGGIE & PAC Mwaka 1999 mama wa Tupac na Biggie walitangaza kuwa kitu kimoja kufuatia kumbukumbu ya watoto wao.
****************************************

GENEVIVE MISS TANZANIA 2010
Genevieve Mpangala - Miss Tanzania 2010/11
Pichani chini, akiwa na washindi wa pili na watatu, Glory mwanga (kulia) Concolata Lukos

AY stejini
THT stejini
Waziri wa nihsati na madini, William Ngeleja (kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Dar, William Lukuvi walikuwa miongoni mwa wahudhuriaji

compiled by mc george/wikienda

2 comments:

emu-three said...

Ahsante kwa taarifa hiyo hasa habari ya Tupac...

Anonymous said...

nilifikiri ni ali kiba, kumbe ni waziri wa cabinet.Poa