Tuesday, May 10, 2011

WADAU WALIA NA UKOSEFU WA KUMBI ZA SANAA

Mratibu wa Tamasha la Kila mwaka la Visa To Dance Alloyce Makonde (kushoto) akiwasilisha mada juu ya kupotea kwa sanaa za maonyesho majukwaani kwenye Jukwaa la Sanaa BASATA. Kulia kwake ni Mzee Ballanga na Bumbuli.
Rais wa Shirikisho la Filamu nchini, Simon Mwakifwamba akitoa ufafanuzi juu ya sababu ya
wasanii wengi wa sanaa za maonyesho kukacha sanaa hiyo. Alisema kwamba,Msanii hawezi kukamilika bila kupitia kwenye sanaa za maonyesho.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Sanaa za Maonyesho nchini, Denis Mango akiwaeleza wadau wa Jukwaa la Sanaa juu ya mikakati mbalimbali ya shirikisho hilo katika kufufua sanaa za maonyesho. Hata hivyo, alisema kwamba ukosefu wa kumbi ni changamoto kubwa.
Wadau wa Jukwaa la Sanaa wakifuatilia mjadala kwa umakini.
Mjumbe wa Shirikisho la Sanaa za Maonyesho nchini na mtendaji wa Chama cha Sanaa za
Maonyesho Mzee Nkwama Ballanga (Katikati) akichokoza mada kwenye Jukwaa la Sanaa juu ya Kupotea kwa Sanaa za Maonyesho majukwaani. Kulia ni Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz), Hassan Bumbuli na Alloyce Makonde muandaaji wa Tamasha la Visa to Dance.


Na Mwandishi Wetu
Wadau wa Sanaa wamelia na ukosefu wa kumbi za sanaa na burudani nchini huku wakilalamikia kubadilishwa matumizi kwa zilizokuwa kumbi maarufu za maonyesho.

Aidha, wadau hao wameonesha kusikitishwa na kasi ndogo katika kukamilishwa kwa kumbi za sanaa na burudani zinazozojengwa eneo la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Kijiji cha Makumbusho ya Taifa Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Wakijadili mada juu ya Kupotea kwa sanaa za maonyesho katika majukwaa kwenye Programu ya Jukwaa la Sanaa inayofanyika kila Jumatatu ndani ya ukumbi wa mikutano wa BASATA, wadau hao walisema kwamba, ukosefu wa kumbi za maonyesho hapa nchini hasa baada ya kubadilishwa matumizi kwa zile zilizokuwepo ndiyo chanzo kikubwa cha kuporomoka kwa sanaa za maonyesho.

“Tulikuwa na kumbi maarufu za maonyesho kama Lumumba na vituo vya sanaa vya Singida na Musoma, watu walikuwa wakiingia ukumbini kwa wingi lakini siku hizi kumbi hizo kama ule wa Lumumba umegeuzwa supermarket" alilalamika Mzee Nkwama Ballanga kutoka Chama cha Sanaa za Maonyesho nchini.

Aliongeza kwamba, zamani serikali ilihimiza mashirika ya umma na vyombo vyake mbalimbali kuunda vikundi vya sanaa na utamaduni ambapo viliamsha hamasa ya kukuza sekta hii muhimu nchini tofauti na sasa ambapo serikali imebadili sera yake na hata kufikia hatua ya kuzibadilishia matumizi baadhi ya kumbi maarufu za maonyesho bila kujenga mpya hivyo kuwaacha wasanii wakikosa sehemu za kufanyia maonyesho.

“Tunaishukuru serikali kwa kuanza kujenga kumbi za sanaa kama huu wa BASATA na ule wa Kijiji Cha Makumbusho lakini kasi yake ni ndogo sana. Kwa mfano Ukumbi huu wa BASATA umeanza kujengwa toka mwaka 2006 hadi sasa haujakamilika. Ule wa Makumbusho ni kama ujenzi umesimama” aliongeza Alloyce Makonde ambaye ni muandaaji wa Tamasha maarufu la kila mwaka la Visa To Dance.

Mbali na ukosefu wa kumbi, changamoto kama za utandawazi, ukosefu wa hamasa miongoni mwa wananchi, malipo kidogo kwa wasanii,bajeti ndogo kwa wizara husika,wataalamu wa sanaa kutokutumia taaluma zao ipasavyo zimetajwa kama chanzo cha kufifia kwa sanaa za maonyesho na hivyo kuhitaji juhudi za makusudi katika kuzifufua.

Wadau wengi walitoa wito wa kuongezwa kwa kasi katika ujenzi wa kumbi hizo, kuongezwa bajeti kwa wizara husika,kurudisha kumbi zilizobadilishwa matumizi huku wakilitaka Shirikisho la Sanaa za Maonyesho nchini kwa kushirikiana na BASATA kubuni mbinu ya kufufua upya sanaa za maonyesho.

No comments: