Tuesday, July 12, 2011

WADAU WAOMBA BALOZI ZITUMIKE KUTANGAZA SANAA

choraji maarufu nchini Mohamed Raza (Kulia) akionesha moja ya kazi zake wakati akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu makao makuu ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA). Kulia kwake ni Katibu Mtendaji wa BASATA, Bw. Ghonche Materego.
Katibu Mtendaji wa BASATA, Bw. Materego akisisitiza jambo wakati wa majumuisho ya Jukwaa la Sanaa wiki hii. Kulia kwake ni Msanii Raza na Kaimu Mratibu wa Jukwaa hilo. Bi. Agnes Kimwaga.
Mdau Joshuia ambaye ni msanii wa Sanaa za Ufundi akichangia mada kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii. Alishauri wilaya ziwe na eneo maalum la maonyesho ya kazi za mikono.

Mwandishi wa Habari kutoka Chuo cha DSJ naye aliuliza masuala mbalimbali kuhusu sanaa za ufundi nchini na haja ya wasanii wakongwe kurithisha vipaji vyao kwa watoto.
 
Sehemu ya wadau wa Jukwaa la Sanaa wakifuatilia mjadala kwa makini

NaMwandishi Wetu
Wadau wa Sanaa wameiomba serikali kutumia balozi zake zilizoko kwenye mataifa mbalimbali duniani kutangaza kazi za wasanii nchini ili kuweza kutanua masoko yao.

Ombi hilo limetolewa wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa wakati msanii maarufu wa sanaa za uchoraji nchini, Mohamed Raza alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu ‘Mchango wa Sanaa za Ufundi Katika Soko la Utalii’ ambapo alisema kwamba, kuna kila sababu ya serikali kuwa na kitengo maalum katika balozi kinachohusika na kutangaza kazi za wasanii wa ndani.

“Inabidi tutumie balozi zetu za nje kutangaza kazi za wasanii. Balozi za wenzetu hapa nchini zimekuwa zikifanya kazi ya kutangaza bidhaa za wasanii wao hapa kwetu na sisi lazima tufanye hivyo na tushirikiane nao” alisema Raza ambaye amepata bahati ya kuchora picha za marais wote wa nchi hii.

Aliongeza kwamba, wasanii hapa nchini wamekuwa wakitengeneza kazi nyingi zenye ubora hasa za ufundi lakini tatizo kubwa limekuwa kwenye masoko hasa ya nje na kuongeza kwamba, kwa balozi kuwa na eneo maalum la kuonesha kazi za wasanii kutasaidia sana kutanua soko.
Wadau wengine waliochangia mjadala huo, waliiomba serikali kutilia mkazo matumizi ya kazi za sanaa za ufundi katika ofisi zake ili kutanua soko la wasanii wa ndani badala ya ilivyo sasa ambapo kumekuwa na uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje.

“Vijana wengi sana wamejiajiri kwenye sekta ya sanaa na hata kwenye pato la taifa wamekuwa wakichangia lakini tatizo ni kutothaminiwa kwa kazi zao. Serikali iwe mstari wa mbele kuthamini kazi za wasanii na kuzitumia katika ofisi zake” alishauri Joshua mbaye ni moja ya wasanii wa Sanaa za Ufundi nchini.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego alisema kwamba, Serikali imekuwa ikiwathamini wasanii wake ndiyo maana imekuwa ikishirikiana nao katika kazi mbalimbali yakiwemo matukio ya kitaifa.

“Makatibu Wakuu wa wizara kupitia kikao chao, wamelitaka Baraza kukusanya wasanii wachoraji kwa ajili ya kuchora nembo ya miaka 50 ya uhuru. Baraza limefanya hivyo kwa kushirikiana na Shirikisho la Sanaa za Ufundi. Mtaona ni kwa jinsi gani wasanii wamekuwa wakipewa nafasi kubwa” alisema Materego.

No comments: