'Dar inachangia asilimia 80 ya mapato. Kitovu cha Uchumi. Dar inachangia 90% ya ufisadi. Uti wa mgongo wa ufisadi nchini'
Malumbano
kati ya wananchi wa Mtwara na Serikali kuhusu matumizi bora ya utajiri
wa nchi yameendelea kwa takribani wiki moja sasa. Baada ya Mkuu wa Mkoa
wa Mtwara na Waziri wa Nishati na Madini kuwaita Watanzania wa Mtwara
Wahaini, wapuuzi na watu hatari, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
naye aliingia kwenye mjadala huo kwa kuonya watu wanaowaunga mkono watu
wa Mtwara na kuwaita watu wanaotafuta umaarufu wa kisiasa na wanaotaka
kugawa nchi. Siku moja baada ya hotuba ya Rais, Waziri wa Nishati na
Madini alifanya mkutano na waandishi wa habari kueleza suala lile lile
ambalo bosi wake alilielezea usiku wa kuamkia mwaka mpya 2013. Hii ni
dalili ya Serikali kuweweseka.
Katika
kauli ya Serikali, ambayo haikuwa na jipya zaidi ya wimbo ule ule wa
‘kugawa nchi’ ‘umaarufu wa kisiasa’ nk, Serikali ilitaka kuonyesha umma
kuwa watu wa Mtwara hawana shukurani. Kwamba miaka yote toka Uhuru watu
wa Mtwara wamekuwa wakilishwa na Pamba, Kahawa, Chai, Tumbaku, Sukari,
Kidatu nk. Kwamba watu wa Mtwara na Lindi hawakuchangia hata kidogo
kwenye hazina ya Taifa. Hivyo wao kupigia kelele gesi yao ni uchoyo na
roho mbaya na kukosa shukurani. Kauli ya Serikali ni kauli ya chombo
kinachoendelea kukosa ‘legitimacy’ ya kuongoza taifa. Ni kauli ya kukata
tamaa. Ni kauli hatari sana dhidi ya Watanzania waliojitolea damu
kulinda uhuru wa nchi yetu.
Moja,
Serikali katika kauli yake haitaji kabisa kwamba toka Uhuru watu wa
Mtwara na Lindi wamekuwa wachangiaji wakubwa sana katika uchumi wa Taifa
kupitia zao la Korosho. Takwimu za Uzalishaji wa Korosho zinaonyesha
kwamba kuanzia mwaka 1965 mpaka 2011 Korosho imeliingizia Taifa fedha
kigeni jumla ya dola za Kimarekani 4.58 bilioni ( Cashewnuts Sub-sector
study 2003, Hali ya Uchumi 2012, Cashewnuts Tanzania Report 2010).
Katika Mwaka wa Uchumi unaoishia Novemba 2012, Korosho imeliingizia
Taifa jumla ya dola za Kimarekani 151 milioni. Katika mwaka 2011 zao
hili liliingiza dola 130 milioni wakati Pamba iliingiza dola 53 milioni
tu. Licha ya Zao la Korosho kuingiza fedha hizi za kigeni (sawa ni
shilingi trilioni 7.2) kwa nchi mikoa ya Lindi na Mtwara ipo miaka 50
nyuma kimaendeleo kulinganisha na mikoa mingine ya Tanzania. Serikali
inataka kufuta historia ya mchango wa zao la Korosho kwenye uchumi wa
nchi yetu kwa sababu ya uroho wa gesi asilia. Kwa nini kauli rasmi ya
Serikali haijataja Korosho kabisa? Kauli hii ilipitishwa na ngazi zote
za Serikali? Mawaziri wa Serikali wanaotoka mikoa ya Lindi na Mtwara
walikubali kauli kama hii itoke dhidi ya wananchi wao wanaoteseka na zao
la Korosho miaka nenda miaka rudi?
Pili,
Serikali imesahau kabisa mchango wa watu wa Lindi na Mtwara katika
ulinzi wa Taifa letu. Moja ya sababu ya mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa
nyuma kimaendeleo ni juhudi za ukombozi wa kusini mwa Afrika. Kambi ya
wapigania uhuru wa Msumbiji ilikuwa Nachingwea. Kambi ya Frelimo
iliwekwa kwenye Shamba la Mkonge kilometa 17 tu kutoka mjini Nachingwea
ambapo ilikuwa makao makuu ya ukombozi wa Msumbiji. Rais Samora Machel,
Rais Joaqim Chissano na Rais Guebuza waliendesha mapambano kutoka kusini
mwa Tanzania. Makaburu wa Afrika Kusini na Wareno walikuwa
wanashambulia nchi yetu na mikoa hii miwili ya Lindi na Mtwara ikawa
‘buffer zone’. Wakati Dar es Salaam inaendelea kwa kila aina ya
maendeleo, mikoa ya Lindi na Mtwara ilikuwa inalinda ili wanaoishi Dar
es Salaam na mikoa mingine waishi wa amani na starehe. Serikali
inapimaje mchango huu wa mikoa hii? Tunaipima kwa fedha? Uroho wa gesi
asilia kuzalisha umeme wa kufurahisha walalaheri asilimia 14 nchini ndio
inaifanya Serikali kusahau kabisa ‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara katika
kulinda uhuru wa Taifa letu?
Tatu,
Serikali inasema lazima bomba lije Dar es Salaam kwa sababu Dar ndio
inazalisha asilimia 80 ya Mapato ya Serikali. Kwanza huu ni uwongo. Ni
aibu Serikali kujitetea kwa uwongo. Dar es Salaam ni kituo tu cha
kukusanyia mapato ya Serikali. Uzalishaji mkubwa wa nchi yetu wenye
kuzalisha kodi unafanyika nje ya Dar es Salaam. Walipa kodi wakubwa
wengi Ofisi zao Kuu zipo Dar es Salaam lakini uzalishaji wao unafanyika
nje ya Dar es Salaam. Serikali itoe orodha ya walipa kodi wakubwa 100
tuone uzalishaji halisi wa mapato hayo unafanyika wapi. Hata hivyo
inawezekana kuwa ikawa kweli Dar es Salaam inakusanya asilimia 80 ya
mapato ya nchi. Basi na tuseme Dar es Salaam inachangia asilimia 90 ya
ufisadi wote nchini. Kashfa zote kubwa za Ufisadi zinafanyika Dar es
Salaam na fedha nyingi za ufisadi zinatumika Dar es Salaam.
Mwisho,
maandamano ya watu wa Mtwara ni kielelezo tosha kwamba watu wa mikoa ya
Lindi na Mtwara wamechoshwa na longolongo za Serikali. Wananchi wa
Mtwara na Lindi wanataka Uwajibikaji wa Serikali kuhusu utajiri wa nchi.
Mtanzania yeyote mwenye tahadhari ya nchi yetu kutokuwa na laana ya
rasilimali ataungana mkono na watu wa Lindi na Mtwara kudai maendeleo.
Nilitoa mfano wa Mgodi wa Golden Pride ambao umemaliza dhahabu yote tani
76 katika eneo la Lusu wilayani Nzega. Kampuni ya Resolute ya
Australia iliwekeza dola 370 milioni kuanzia mwaka 1998 (mkataba wao
ulisainiwa 25th June 1997). Katika kipindi cha uhai wa mgodi, miaka 14,
Kampuni hii imeuza dhahabu ya thamani ya dola za kimarekani 3.3
bilioni. Kabla Serikali haijawaita watu Mtwara wahaini, wapuuzi na watu
hatari, iwaambie watu Watanzania kodi kiasi gani imekusanywa kutoka
mgodi huu katika kipindi cha miaka 14. Mpaka mwaka 2008, kwa mujibu wa
Taarifa ya Kamati ya Bomani, kampuni hii ilikuwa imelipa mrahaba wa dola
11 milioni na kodi nyingine dola 16 milioni. Serikali itwambie ilipofika Disemba 2012 kodi kiasi imekusanywa kutoka kampuni hii?
Pia
watu wa Mtwara na Lindi wameona historia ya bomba la Songosongo. Hata
kodi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (0.3%) ilikuwa inalipwa
Halmashauri ya Manispaa Ilala na kampuni ya Pan Africa Energy. Ilichukua
juhudi za mbunge wa Kilwa Kaskazini Murtaza Mangungu kuingilia kati
ndio kodi ikaanza kulipwa Kilwa ambapo uzalishaji unafanyika. Watu wa
Mtwara ni werevu, wanajua wafanyalo. Wanataka utajiri wa nchi unufaishe
nchi kwa kuanzia kule utajiri ulipo. Kuna dhambi gani?
Uwajibikaji
katika uvunaji wa Rasilimali ya Gesi ndio chanzo cha maandamano ya watu
wa Mtwara. Serikali isikimbilie kulaumu wanasiasa kwamba ndio
wamechochea maandamano haya. Haya ni maandamno ya wananchi wakitaka
Serikali yao iwajibike kwao. Serikali ithubutu kufanya ubabe wa kujenga
bomba la gesi bila ridhaa ya Wananchi wa Lindi na Mtwara. Wananchi
wanapohitaji uwajibikaji ni wajibu wa Serikali kuwajibika kwao ni sio
kuwaita wahaini, wachochezi, watu hatari, wapuuzi. Watu wa Mtwara
wamechangia maendeleo ya Taifa letu kwa jasho na damu. Serikali ina
wajibu wa kuwasikiliza, kuwaelimisha na kupata mwafaka. Kauli ya
Serikali imewatukana watu wa Mtwara na Lindi. Hawatakubali
kudhalilishwa. Hawatakubali historia yao kufutwa. Hawatakubali waendelee
kubaki nyuma kimaendeleo. Serikali ifikirie tena.
No comments:
Post a Comment