Ndugu zangu,
Katika ulimwengu huu kuna tabia
na hulka. Hivi viwili vina tofauti. Kuna sifa na uwezo, navyo ni viwili
tofauti.
Tabia ya mwanadamu yaweza
kubadilika, lakini si hulka yake. Na mwanadamu anaweza kuwa na sifa za kufanya
jambo lakini akakosa uwezo, na kinyume chake. Na kibaya zaidi ni pale majungu
na fitna yanapogubika sifa na uwezo wa mtu. Kwamba badala ya mwanadamu kupimwa
kwa sifa na uwezo wake, majungu na fitina dhidi ya mwanadamu huyo yanawekwa
mbele na hivyo kufanywa kuwa kipimo.
Ndio, kuna wanadamu wenye kuishi
kwa kupika majungu na fitna dhidi ya wanadamu wenzao. Tofauti na tabia, hizo ni
hulka za wanadamu hao, haziwezi kubadilika.
Ndio, nyani hata akizeeka haachi
hulka yake. Kupalamia miti ni hulka ya nyani. Hivyo, nyani hata akizeeka,
hafikiri hata siku moja kukaa chini ya mti na kupumzika, atahakikisha
anapalamia hata mti mfupi wa mpapai, alimradi akae juu ya mpapai. Hapo atajiona
ametimiza unyani wake.
Naam, Wahenga walitwambia; kiumbe mzito. Mwenyezi Mungu ametuumba wanadamu kwa usawa
kwenye mambo mengi. Wala hakutaka kubagua; ona unyayo wa mwanadamu, uko sawa,
iwe kwa tajiri au masikini.
Wewe na mimi tumepata, ama wenyewe au kusikia
mtu akilalamika kuwa soli ya kiatu chake imechakaa, kwamba anakwenda kwa fundi
viatu kubadilisha soli. Lakini, wewe au mimi hatujapata kumsikia mwanadamu
mwenzetu akilalamika kuwa unyayo wake umechakaa, anataka kwenda kwa fundi
awekewe unyayo mwingine!
Ndio, wewe na mimi ama tumeshuhudia au kusikia kuwa
upepo umeangusha mti, nyumba, ghorofa, gari na hata meli. Lakini, jiulize, je,
umepata kumwona mwanadamu mwenzako anayetembea kwa miguu akiangushwa kwa upepo?
Kamwe mwanadamu haangushwi na upepo, hata awe
mwembamba kiasi gani. Na ukimwona mwanadamu mwenzako anayumba na kuanguka
barabarani, basi, ama ni mgonjwa, au ni mlevi. Na hilo la mwisho haliwezi kuwa
na maana ya mwanadamu huyo kaangushwa na upepo, bali kaangushwa na pombe zake
alizokunywa.
Naam, kiumbe mzito.
Ni Neno La Leo.
Maggid.
Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment