Thursday, October 22, 2015

Kwanini Naiona Serikali Ya John Magufuli Inakuja

Ndugu zangu,
Nionavyo, Nchi yetu iko katika hali ya kama mgonjwa anayetafuta mawili makubwa; nafuu na uimara wa afya yake.
Kama upepo kinzani hautalizuia taifa letu katika kusonga mbele, basi, miaka ijayo itakuwa ni miaka ya ' Nchi kuanza kuwa na kukua zaidi' kutoka hali ya sasa. Nchi itarajie mabadiliko makubwa hata kwenye mitazamo yetu kuhusu kazi na nidhamu ya kazi hususan kwa watendaji.

Hata hivyo, kwenye hali ya mgonjwa kuelekea kuitafuta nafuu na uimara wa afya, uwezo , njia na mbinu za waganga zaweza kutofautiana. Uchaguzi ina maana pia ya kumtafuta yule mganga mwenye kuonyesha kuwa na uwezo, njia na mbinu za kuipata nafuu na uimara wa afya ya mgonjwa.
Hivyo, tukiwa sasa, kama taifa zima, na tunapoelekea kwenda kulijenga daraja kati ya jana na kesho, ni muhimu tukaitazama Tanzania kwanza na kuwa na mioyo ya kuvumiliana na kuheshimiana. Umuhimu wa kuilinda amani yetu.
Ndugu zangu,
Katika kuishi kwangu nina bahati ya kuwa na uzoefu wa miaka mingi wa kufuatilia siasa za kitaifa, bara la Afrika na dunia kwa ujumla.
Katika kuishi kwangu pia, sijawa na wala sifikirii kuja kuwa mwanachama wa chama cha siasa. Kwangu Watanzania wa vyama vyote, na wasio na vyama ni ndugu zangu. Na kwa kusema hivyo haina maana sina itikadi ya kisiasa inayoniongoza. Mimi naamini katika Ujamaa na Kujitegemea. Ndio, I am a Social Democrat.
Nilichokiweka mezani jana ni mtazamo wangu. Sijarudi nyuma hata robo hatua. Nimesimama pale pale, kwamba ninachokiona ni kuwa Serikali inayokuja ya Awamu ya Tano itaundwa na John Pombe Magufuli.
La Magufuli kuunda Serikali ishara zake niliziona muda mrefu na nikaweka bayana hilo mwezi uliopita. Na leo zikiwa zimebaki siku tatu kabla kufanyika Uchaguzi Mkuu, hakika sizioni ishara mpya.
Kwanini John Magufuli atashinda?
Kuna sababu moja kubwa. Kwamba wakati mgombea wa Ukawa- Chadema anabebwa na umaarufu aliokuwa nao akiwa CCM, umaarufu huo wa mtu mmoja umekuwa wa gharama kwa Chadema kama chama.
Ni kwa vile, ilitarajiwa, na haikutokea, kuwa mgombea urais wa Ukawa- Chadema angetoka CCM na kundi kubwa la wafuasi kutoka CCM. Kwa sasa wachache waliohama CCM na Edward Lowassa wako katika kundi la ' Political spent forces'. Ni waliokwishatumika kisiasa kwa sifa ya mazuri na mabaya.
Kabla ya kuhama kwao hawakuwa kwenye nafasi za juu kwenye chama na Serikali, na kuhama kwao kunaweza pia kutafsiriwa kuwa ' Wamechoshwa na masengenyo ya ndani ya chama'.
Kwamba chama chao kilishindwa kuwaonyesha umuhimu wao. Ndio, kumekuwa na kundi la ' Wanasiasa wanung'unikaji' ambao wangetimiziwa haja zao za kisiasa wangebaki huko huko CCM na wangesimama majukwaani kuimba ubora wa CCM !
Ni kweli kuwa, kwenye siasa umaarufu wa mgombea ni jambo muhimu, lakini, sadaka za kisiasa huambatana na umaarufu wa chama na kukubalika kwake kwa wananchi.
Kwa ajenda ya kupambana na ufisadi ambayo Ukawa- Chadema walikuwa nayo mpaka miezi kadhaa iliyopita, kimsingi iliwajengea umaarufu na kukubalika kama chama. Ni jambo la ajabu sana kuwa upinzani ukiongozwa na Chadema umeitupilia mbali ajenda hiyo.
Ziada ya matatizo ya upinzani kwa sasa ni hali ya kutoelewana kwa viongozi wakuu ndani ya upinzani. Hali ya hata kugombania majimbo na kata. Na kujiweka pembeni kwa Dr Slaa na Profesa Lipumba ni pigo kubwa.
Ina tafsiri ya upinzani kupoteza sehemu kubwa ya mtaji wa imani kutoka kwa wapiga kura. Upinzani umeshindwa kuonyesha mshikamano wa kiuongozi- Cohesive leadership.
Wapiga kura wanaelewa kuwa uongozi wa juu wa nchi ni jambo muhimu na nyeti. Linahusu mustakabali wa nchi na maisha yao. Kwa viongozi wa upinzani kushindwa kuonyesha cohesive leadership hakuwapi imani wapiga kura walio wengi kuwa mambo yatakuwa shwari watu hao hao wakipewa nafasi ya kuongoza nchi.
Na ujio wa Edward Lowassa Ukawa- Chadema umeliibua kundi lingine la ' Wanung'unikaji' ndani ya UKAWA. Hawa wanahoji taratibu za Lowassa kuingizwa Ukawa na kupewa nafasi ya juu ya kugombea urais. Ikumbukwe, Dr Slaa na Profesa Lipumba wamejiengua, nao wana wafuasi wao.
Watanzania huchagua zimwi..
Chama cha Mapinduzi katika Tanzania ni zaidi ya Chama cha siasa. Ni taasisi kubwa na karibu kila Mtanzania ana nasaba na CCM. Ni moja ya vyama vikongwe Afrika vyenye sifa kubwa ya kuwa na mizizi katika kila eneo la ardhi ya nchi wanakoishi watu. CCM ni sehemu ya maisha ya Watanzania.
Ni katika uhalisia huo, kuna wanaokipenda chama hicho na kuna wanaokichukia pia, kwa wenye kukichukia kwao ni zaidi ya zimwi, ni kama shetani anayewawekea giza kwenye maisha yao. Watu hawa hulilia mabadiliko, na kwao tafsiri ya mabadiliko ni kuiondoa CCM tu, basi. Hawa si wengi sana kama inavyodhaniwa, lakini, wana uwezo mkubwa wa kupiga kelele ambazo CCM hawapaswi kuzipuuzia.
Na hakika, katika kero na matatizo mengi wanayoyapata Watanzania, hufika mahali wapiga kura wengi wanajua kuwa wanakwenda kuchagua zimwi.
Kwa tabia, wapiga kura huwa ni waoga sana kuchagua wasichokijua. Na wanajua pia, kuwa Rais wa nchi ni nafasi nyeti. Kama hawawajui watakaomzunguka Rais, basi, huingiwa na mashaka.
Wahenga walisema; " Zimwi likujualo halikuli likakwisha". Hivyo, Wapiga kura wengi kwa tabia huenda kuchagua zimwi wanalolijua, na hapa ni CCM.
Edward Lowassa angehama na ' Mazimwi' mengi kutoka CCM, tena yale ambayo wapiga kura wanayajua, basi, nafasi ya Edward Lowasa kushinda urais ingekuwa kubwa.
Mimi naamini, Lowassa angebaki kuwa mgombea ndani ya CCM, bado Lowassa na CCM wangeshinda , lakini kwa tabu sana kwa mantiki ile ile ya mgombea kuzungukwa na mazimwi mengi ambayo wapiga kura wanayajua. Lakini, upinzani ungepata viti vingi zaidi kuliko ambavyo itapata kwenye uchaguzi ujao, ni kwa vile, upinzani ungebeba ajenda ya kupambana na ufisadi ambayo ni kero kubwa kwa Watanzania wengi. Na nchi yetu inahitaji siasa za upinzani kuanzia kwenye udiwani hadi ubunge.
Vinginevyo, kwa hali ninavyoiona sasa, Watanzania tutarajie ujio wa Serikali ya John Pombe Magufuli kama Rais wa Awamu ya Tano.
Ni mtazamo wangu.
Maggid,
Iringa.

No comments: