Saturday, December 5, 2015

Magufuli Anapotumia ' Dawa Chungu' Kwa Maslahi Ya Nchi..

Ndugu zangu
Kwenye kitabu chake cha " The Prince", yaani, "Mwana Mfalme", Mwanafalsafa Niccole Machiaevelli anamtaka kiongozi kuwa makini na tabaka la waliomsaidia kuingia madarakani na hata wenye kumzunguka.
Kwa mujibu wa Machiavelli, hutokea kwa Mwana Mfalme "kuwajeruhi" waliomsaidia kuupata utawala. Hii ni kwa kutowatimizia yote yale waliodhani kuwa ni haki yao kutimiziwa.
Badala yake, Mwana Mfalme huwaingiza kundini wawe kama wengine.
Katika manung'uniko yao, Mwana Mfalme hawezi kutumia dawa chungu dhidi yao kwa vile hujihisi ana deni kwao. Lakini, cha msingi kwa Mwana
Mfamle ni kuzingatia ukweli, kuwa, hata kama atakuwa na maadui
wachache, katika kuchukua nchi, muhimu ni kuwaridhisha walio wengi, na
hapa ni wananchi.
Huwezi kutawala kwa amani bila upendo na utashi wa walio wengi. Ni kwa sababu hizi, Mfalme Louis XII wa Ufaransa aliweza kwa kasi ya ajabu kuitwaa Milan na kwa kasi ya ajabu kuipoteza Milan.Hakukidhi matakwa na matarajio ya wananchi walio wengi waliomfungulia
milango.
Mtawala aliye mbali na asiyejali maslahi ya watu wake walio
wengi ni mtawala mwenye hofu. Na mtawala mwenye hofu zaidi na watu
wake kuliko adui wa nje, basi, hujijengea kasri ama ngome imara ya
kujihifadhi ingawa hilo halitamsaidia kuzuia nguvu za umma za
kumwondoa madarakani. Kwa mtawala, kasri ama ngome iliyo imara ni
kuepuka kuchukiwa na wananchi, kuacha ubinafsi na kujali maslahi ya
wengi.
Tunaona, katika kutanguliza maslahi ya wananchi walio wengi, Rais John Magufuli (pichani) ameamua kutumia dawa chungu ya ' kutumbua majipu' hata kwa wale waliodhani, kuwa hawangeguswa kwa vile wamemsaidia katika kuingia madarakani. Maana, kuna wanaodhani, kuwa kwa vile wamechangia kwenye hata kampeni za kumwingiza Magufuli madarakani, basi, Magufuli hapaswi kuhangaika na kuchunguza makandokando yao, kwamba wanastahili kuwemo kwenye Serikali ya Magufuli.
Na kwa vile, Magufuli ana kila dalili za kufanya kinyume na matarajio ya watu wa aina hiyo, basi, yumkini watu hao watageuka kuwa maadui zake.
Na tusubiri tuone.
Maggid,
Iringa.

No comments: