Monday, August 13, 2007

BWANA HARUSI AJIUA SIKU YA NDOA!

Na Dotto Mwaibale aliyekuwa Chanika
Bwana harusi mtarajiwa, Jumanne Salehe Madeng'a (35) mkazi wa Kwangwale, Chanika jijini Dar es Salaam, amefariki dunia kwa kujinyonga kwa kamba ya katani aliyoifunga juu ya paa la nyumba yake huku akiwa amebakiza masaa machache afunge ndoa.

Kifo cha bwana harusi huyo kilichotokea juzi Jumapili, kimewasikitisha watu wengi waliokuwa wakimfahamu wakiwemo wazazi na mchumba wake aitwaye Jamila Saidi Msitu (30), kwani maandalizi yote ya sherehe hiyo yalikuwa yamekamilika ikiwa ni pamoja na kumtafuta sheikhe wa kufungisha ndoa hiyo.

Akiongea na mwandishi wetu aliyekuwepo eneo la tukio, mjomba wa marehemu, Bw.Mohammed Saidi alikuwa na haya ya kueleza:

''Kifo cha kijana wetu kimetusikitisha sana kwani alikuwa afunge ndoa leo hii (Jumapili) na maandalizi yote yalikuwa yamekamilika kwani chakula kilikuwa kimenunuliwa na kupikwa huku baadhi ya ndugu wanaoishi nje ya Dar es Salaam walikuwa tayari wamewasili.

"Mbali ya ndugu hao waliofika, jamaa wengine na marafiki wamepata taarifa za kifo hicho asubuhi hii wakiwa njiani kuja kwenye harusi huku akina mama wakiwa wamevaa sare za harusi.

"Siku ya Jumamosi asubuhi bwana harusi huyo mtarajiwa aliitwa na mama yake na kuambiwa kuwa leo asubuhi aende akachukue pesa kwa ajili ya kununua mboga ya sherehe hiyo.

"Baada ya kuambiwa hivyo aliondoka na hatukumuona tena hadi tulipopata taarifa hizo za kujinyonga leo hii asubuhi,"alisema Bw. Mohamed.

Naye mchumba wa marehemu, Jamila Saidi Msitu alisema kwamba Jumamosi mchana walikuwa na marehemu sehemu ya Msumbiji anakofanya biashara zake ambapo alimuaga kuwa anakwenda Gongo la mboto kumsalimia dada yake.

Alisema saa 12 jioni mchumba wake alimpigia simu akimjulisha kuwa amerudi na yupo nyumbani kwa mchumba wake huyo eneo la Masantula hapo Chanika.

Jamila alisema kwamba baada kufunga biashara yake alirudi nyumbani kwake ambapo alimkuta mchumba wake akiwa amejipumzisha, kisha walianza kuongelea juu ya ndoa yao iliyopangwa kufanyika leo saa nane mchana.

Alisema siku zote walikuwa na kawaida ya kwenda kulala nyumbani kwa mchumba wake, lakini siku hiyo aliambiwa kuwa hataweza kwenda naye kwa sababu kulikuwa na kaka yake aliyefika kutoka Kazimzumbwi kwa ajili ya harusi hiyo.

Baada ya kumuambia hivyo aliondoka ambapo alizima simu yake akaenda kulala na asubuhi alipoifungua alikuta ametumiwa ujumbe (sms) na mchumba wake akimuambia alale salama.
Alisema baada ya kusoma meseji hiyo aliamua kumpigia simu ili kujua maandalizi ya ndoa yao ambayo ilikuwa ifanyike siku hiyo, lakini ilikuwa ikiita bila ya kupokelewa jambo lililomfanya apate wasiwasi ndipo alipomuita shemeji yake ambaye naye alipojaribu kupiga ilikuwa ikiita tu.

Wakati wakiendelea kumpigia, mama yake marehemu naye alikuwa akimpigia baada ya kuona amechelewa kwenda kuchukua pesa kwa ajili ya kununulia mboga, ndipo dada zake waliamua kwenda nyumbani kwa kaka yao ambako walikuta milango ikiwa imefungwa na walipopiga simu yake walisikia ikiita kutoka ndani.

Kutokana na hali hiyo waliingiwa na wasiwasi ambapo walikwenda kutoa taarifa kwa mjumbe wa nyumba 10 wa eneo hilo, Bw. Tullo ambaye alifungua mlango na kumkuta akiwa amejinyonga.

Habari zinasema mjumbe huyo alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Chanika ambao nao waliwataarifu wenzao wa Buguruni ambapo walifika eneo la tukio wakiwa na gari la polisi na. PT 0965 na kumkuta marehemu akiwa ananing'inia na walipopiga simu yake ilisikika ikiita kutokea sehemu zake za siri.

Askari hao walichukua maelezo kutoka kwa ndugu pamoja na ujumbe wa barua aliyoiandika marehemu na kisha waliondoka na mwili wake kwenda kuuhifadhi Hospitali ya Amana.

Ujumbe uliochwa na marehemu huyo ulisema ameamua kujiua kwa hiyari akiwa na akili timamu kwa sababu ya kutoelewana na ndugu zake katika mipango ambayo aliona haiendi sawa.

Katika ujumbe huo aliagiza nyumba, kitanda, godoro na mazao ya kudumu yaliyopo shambani mwake apewe mchumba wake.

Habari zilizopatikana kutoka kwa mmoja wa wana familia ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini, zimedai kuwa sababu ya bwana harusi huyo kuchukua uamuzi huo wa kujiua ni baada ya ndugu zake kung'ang'ania aoe siku hiyo baada ya kutoa mahari ambayo kwa kabila la Wazaramo wanaiita 'pamvu'.

Imedaiwa na ndugu huyo kwamba marehemu alitaka afunge ndoa mwezi ujao ili apate nafasi ya kualika marafiki zake walioko mbali na kufanya sherehe kubwa, lakini baada ya kuona jamaa zake wanamlazimisha ndipo aliamua kujiua.



'MTOTO HUYU ASIPOSAIDIWA HARAKA ATAKUFA'


Mariam Mndeme
Bi. Neema Paulo, mkazi Keko Magurumbasi jijini Dar es Salaam anaomba msaada kwa wasamaria wema kutokana na mwanae Mathew Pascal (pichani kulia) kukabiliwa na ugonjwa uliomfanya utumbo wake uwe nje.

Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni, Bi. Neema alisema mwanae huyo alizaliwa akiwa hana tatizo lolote lakini baada ya wiki moja alianza kuvimba tumbo ambapo sasa anaona asiposaidiwa anaweza kufa.

Alisema kuwa baada ya mwanae huyo kuvimba tumbo alimpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo alifanyiwa upasuaji na kuachwa utumbo aina mbili nje ukining'inia hivyo kumpa wakati mgumu wa kumlea mtoto huyo.

Aliongeza kuwa baadae alitafuta fedha na kumpeleka mtoto huyo kwa mara nyingine Hospitali ya Muhimbili ambapo alifanyiwa upasuaji wa kuingiza ndani utumbo mmoja na kubaki mmoja na sasa amekwama kutokana na ukata.

"Nawaomba Watanzania wenzangu wanisaidie ili mtoto akafanyiwe upasuaji wa kuuingiza utumbo uliobaki ndani, naamini zoezi hilo likifanyika ataishi kama watoto wengine, nawaomba mnisaidie mwanangu anakufa, sielewi kwanini awali madaktari waliuacha utumbo huu mmoja nje," alisema kwa masikitiko mama huyo.

Yeyote aliyeguswa na habari hizi awasiliane kwa simu namba +255 0754 325 939 au wanaoishi Dar es salaam wafike ofisi za gazeti hili Mtaa wa Aggrey, jengo la vioo, Kariakoo jijini Dar es Salaam.

5 comments:

Anonymous said...

Bwana Abdallah, Pole na Kazi.

Ningependa picha ya huyo mtoto mgonjwa ungeisambaza kwa wana blog wengine hasa Issa Michuzi na Chemi che-mponda ili taarifa iwafikie wengi wapate kuguswa na kutoa msaada wa matibabu.

Samahani kwa usumbufu

Anonymous said...

Yaani mie nashangazwa kabisa tena saaana na hawa Ma Dr. wetu wa Bongo hivi kama waliweza kuingiza utumbo mmoja kwanini wasijitolee tu wakamsaidia na huo mwengine? au ni kipi kinachowafanya wao washindwe kusaidia watu matibabu ya bure na kuacha watu wakipoteza maisha? Hao madokta hata wao ni binadamu na pia wanapaswa kuombwa misaada wajitolee misaada kuwatibu watu kama hao wasiokuwa na uwezo.

Pole Dada!! ila mungu ataleta neema zake utapata watu wa kukusaidia nam mtoto wako atapona tu kwa baraka za mungu.

Anonymous said...

JAMANI SASA VYOMBO VYA HABARI MNAANZA KUTUYUMBUSHA SASA ITABIDI TUWE TUNAFANYA UTAFITI NA SISI KABLA YA KUAMINI NA KUWEKA KICHWANI HAYA. IPP MEDIA HABARI YAO INASEMA HIVI NA HUKU HIVI UWWWIII AFADHALI SASA HIVI TUMEANZA KUAMKA TANGU ISSUE YA CHAHALI TUMEANZA KUWA WACHUNGUZI NA SISI. HABARI YA IPP HII HAPA

Kijana ajimaliza na kuwaachia ujumbe polisi

2007-08-13 16:02:24
Na Kiyao Hoza, Jijini


Mtu mmoja mkazi wa Chanika kwa Ngwale Jijini Dar es Salaam, amekutwa chumbani kwake akiwa amekufa, baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya nailoni.

Kamanda wa mkoa wa kipolisi wa Ilala, Masindoki Masindoki, amemtaja mtu huyo kuwa ni Jumanne Salehe, 30, aliyekutwa akining\'inia kwenye kenchi chumbani kwake huko Chanika kwa Ngwale.

Kamanda Masindoki amesema mtu huyo aligundulika kuwa amejinyonga jana mishale ya saa 4:30 asubuhi, baada ya watu kuona amechelewa kuamka isivyo kawaida yake.

Kwa mujibu wa Kamanda Masindoki, marehemu alicha ujumbe ambao ulitaka kifo chake kisihusishwe na mtu yeyote, kwa vile alifanya hivyo kwa sababu zake binafsi.

Ujumbe huo ulisomeka hivi: `Nimejinyonga kwa sababu zangu, hivyo asibughudhiwe mtu yeyote kuhusiana na kifo changu,`
Hata hivyo Kamanda Masindoki amesema chanzo cha kifo hicho bado hakijajulikana na kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali ya Amana.

SOURCE: Alasiri

JAMANI UMRI NA UJUMBE HATA HAVIELEWEKI NANI MKWELI SASA HAPO ALASIRI AU UWAZI. MMMMH HII NI AIBU SASA. OK MIAKA TUNAWEZA KUSEMA MMOJA WAPO AMEKOSEA BAHATI MBAYA BASI HATA UJUMBE WA MAREHEMU DUH. AU HUYU NI MWENGINE??????

Anonymous said...

Kilicho andikwa na Alasiri kina tofauti sana na kilichoandikwa na Uwazi, tofauti ni kwamba Alaasiri wameripoti taarifa ya kamanda kuhusu tukio hilo, Uwazi wameandika kutoka eneo la tukio, picha wamepiga wameongea na ndugu wa marehemu..na huo ndio uandishi.. sio kuripoti kile unachoambiwa na makamnada wetu ambao hukaa ofisini na wakati mwingine hudanganywa na askari wao...kwa hili lazima tuwaheshimu UWAZI...mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni...

Anonymous said...

hamna ......habari zinazopatikana eneo la tukio huwa hazina ushahidi wa kutosha. una uhakika gani huyo unaeongea nae hajaongeza chumvi habari hiyo?
habari kutoka vyanzo kama polisi ndio inayofaa kuaminiwa. habari za kuokotwa mtaani ndio hizo sasa unaletewa picha ya mmarekani unaambiwa mbongo !!!