Wednesday, August 8, 2007

FUMANIZI NDANI YA GESTI!

Na Waandishi Wetu

Jamaa mmoja aliyefahamika kwa jina la Saidi Abedi mkazi wa Vingunguti jijini Dar es Salaam, hivi karibuni amemfumania mkewe wa ndoa akifanya mapenzi na rafiki yake wa karibu.
Tukio hilo la aina yake na la aibu lilitokea Agosti 5 mwaka huu katika nyumba ya wageni (jina limehifadhiwa), iliyopo maeneo hayo.

Akizungumzia fumanizi hilo, Bw. Saidi ambaye ni mlinzi wa kampuni moja binafsi jijini alisema kuwa, kwa muda mrefu amekuwa akipewa taarifa kwamba, rafiki yake huyo aliyemtaja kwa jina la Fredy amekuwa akimzunguka kwa kuwa na uhusiano usiofaa na mkewe.

“Majirani zangu walikuwa wakinieleza kila mara kuwa ninapokwenda kazini usiku mke wangu anatoka na huyu rafiki yangu, lakini niliona ni uzushi kwani nilikuwa nikimuamini sana mke wangu.

“Leo nikawawekea mtego kwa kumuweka jamaa yangu karibu na gesti ambayo walikuwa wakiingia, mke wangu aliniaga kuwa anaenda gengeni kumbe alikuwa amepanga na yule rafiki yangu wakutane wakafanye uchafu wao.

“Nikiwa nasubiri matokeo ya mtego huo, jamaa yangu alinipigia simu na kuniambia kamuona mke wangu akiingia kwenye gesti hiyo ndipo bila ya kuchelewa nilienda na kufanikiwa kuwabamba laivu,” alisema jamaa huyo.

Ilizidi kuelezwa kuwa, baada ya Bw.Said kufanya fumanizi hilo, varangati zito liliibuka gesti hapo ambapo alianza kushusha kipigo cha nguvu kwa mgoni wake huku mkewe akibaki ameinamisha kichwa kwa aibu.

Hata hivyo, mgoni huyo baada ya kuona mambo yamekuwa makubwa alimuomba rafiki yake huyo alizime ‘soo’ hilo na kuahidi ‘kumpoza’ kwa kumpa shilingi laki tano lakini aliyefumania alizikataa kwa madai kuwa fedha hizo ni za shetani.

Aidha taarifa tulizozipata wakati tunakwenda mtamboni zimetanabahisha kuwa, mwanaume huyo amempa mkewe talaka na mgoni amekimbilia kijijini kwao Mlandizi kukwepa aibu hiyo.


CHUO KIKUU CHA WAISLAMU KUFUTWA...

Na Richard Manyota
Chuo Kikuu cha waislamu nchini kilichopo mjini Morogogo huenda kikafutwa na majengo yake kurejeshwa serikalini Amani limebaini.

Habari za uchunguzi zilizofanywa hivi karibuni na gazeti hili na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia (DP) Mchungaji Christopher Mtikila zimebaini kuwepo kwa uwezekano huo.

Kufutwa kwa chuo hicho kutafikiwa endapo kesi inayoandaliwa na baadhi ya viongozi wa dini ya kikristo akiwemo Mtikila watashinda shitaka la majengo ya Tanesco ambayo ni mali ya umma kugawiwa kwa waislamu.

Awali Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mhe. Benjamini Mkapa aliwamilikisha waislamu majengo hayo ambayo kwa sasa yanatumika kama Chuo Kikuu cha waislamu, jambo ambalo linapingwa na Mchungaji Mtikila na wenzake.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi nyumbani kwake Mchikichini, Dar es Salaam, Mchungaji Mtikila alisema, “Tumeandaa mashitaka kupinga waislamu kupewa majengo ya umma.

“Nchi hii sio ya waislamu peke yao, ni ya dini zote, sasa kuchukua mali ya umma ambayo inajumuisha dini zote na kuwagawia watu wa dini moja ni kosa, ndiyo maana tumeamua kufungua kesi ili majengo hayo yarudishwe kwa wananchi,” alisema Mtikila.

Aliongeza kuwa, maandalizi ya kesi hiyo yamekamilika, ingawa alisita kuwataja viongozi wa dini atakaoshirikiana nao katika kesi hiyo, ambayo alisema itaungwa mkono kwa maandamano ya wakristo kufanyika nchi nzima.

Aidha Mtikila alielekeza lawama zake kwa viongozi wa Serikali ambao alidai kuwa wamekuwa wakitumia mgongo wa dini kutafuta maslahi yao bila kujali athari zake, ambapo alitolea mfano hili la ugawaji wa majengo ya TANESCO.

Gazeti hili lilijaribu bila mafanikio kumtafuta Sheikh Mkuu wa Tanzania na baadhi ya maaskofu wa makanisa ili kufahamu jambo hili kwa kina. Kazi ya kuwasaka viongozi hao na wale wa serikali inaendelea.


No comments: