Wednesday, August 15, 2007

Hammy Jei hoi!


Na Issa Mnally
Dereva teksi wa Kinondoni, Mkwajuni jijini Dar es Salaam aliyefahamika kwa jina moja la Njaidi, a.k.a Hammy Jey, mwishoni mwa wiki iliyopita alijikuta akiwa hoi bin taaban kutokana na umbo lake kuwa kubwa na wingi wa pombe aliyokunywa iliyomfanya aheme kwa shida alipokuwa akicheza muziki.

Tukio hilo la aina yake lilitokea katika Ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni jijini wakati Bendi ya African Stars, Twanga Pepeta ilipokuwa ikifanya onyesho lake.

Dareva huyo wa teksi ambaye mashabiki wa muziki walimpachika jina la Hammy Jei kutokana na vituko alivyokuwa akivifanya, alivamia jukwaa baada ya kuitwa na mwanamuziki wa bendi hiyo, Luiza Mbutu aonyeshe manjonjo.

"Sasa namuita kibonge Njaidi , aje mbele awaoyeshe mashabiki namna ya kucheza mugongo mugongo kwa wanaume wenye vitambi," alisema Mbutu kabla shabiki huyo ambaye mashabiki walikuwa wakimwita kwa jina la Msanii wa Kundi la Ze Comedy, Lucas Mhuvile, Joti au Hammy Jei.

Huku akiwa ameonekana 'kuutwika mtungi' kisawasawa, Hammy Jei alichomoka sehemu aliyokaa na kupanda jukwaani kisha kuanza kunengua kwa staili mbali mbali na kuwaacha hoi kwa kicheko mashabiki wa bendi hiyo pale alipoamua kulaala chali huku akiigiza kuongea na simu.

Ukumbi mzima ulirindima kwa mayowe na vifijo baada ya dereva huyo kuonyesha umahiri wa kunengua kwa kutumia mgongo na wakati mwingine tumbo lake kubwa.

Baada ya kuwafurahisha watu waliokuwemo ukumbini hapo kwa burudani yake, Hammy Jei alionekana akiwa hoi kwa uchovu, lakini hata hivyo aliondoka na kitita!


Miss Mzizima afanyiwa kitu mbaya

Issa Mnally na Imelda Mtema
Aliyewahi kushiriki mashindano ya kumsaka mrembo wa Tanzania mwaka juzi na Miss Mzizima namba 2 wa mwaka huo, Jacqueline Patric, amefanyiwa kitu mbaya na mama mwenye nyumba wake kufuatia ugomvi mkubwa ulioibuka baina yao.

Tukio hilo lilitokea Agosti 12, mwaka huu saa 9 alasiri, Mikocheni, jijini Dar es Salaam.

Akiongea na mwandishi wetu kwa simu, jirani wa mrembo huyo ambaye hakupenda kutaja jina lake, alisema kuwa chanzo cha ugomvi huo ni kitendo cha mama mwenye nyumba wake kumtaka ahame ifikapo mwisho wa mwezi Septemba mwaka huu.

Habari zaidi zinasema kuwa tangu amtake kuhama kumetokea hali ya kutoelewana baina yao.

Akielezea zaidi kuhusu tukio hilo, jirani huyo alisema kuwa Jack aliegesha gari lake vibaya na kuziba njia inayopita karibu na nyumba anayoishi.

Kufuatia hali hiyo, habari zinasema kuwa, wapita njia walilalamikia kitendo hicho lakini mrembo huyo hakutaka kuliondoa.

Habari zaidi zinasema kuwa baada ya mrembo huyo kugoma kuliondoa, mama mwenye nyumba wake aliyefahamika kwa jina la Felicia Ndimbo aliingilia kati na kumtaka aliondoe.

"Mama huyo alimwambia Jack aondoe gari hilo lakini mrembo huyo hakukubali na kuanza kumtolea maneno ya kashfa," kilisema chanzo hicho cha habari.

Tukio hilo lilikuwa kama sinema au 'muvi' ya bure, kwani watu walioshuhudia walikuwa wakicheka jinsi wawili hao walivyokuwa wakipeana maneno mazito ya kashfa.

Habari zaidi zinasema kuwa wawili hao walianza kutupiana matusi na ndipo wakashikana na kupeana mkong'oto wa kutosha ambapo Felicia alikimbilia polisi na kuwataarifu kuwa kafanyiwa fujo na mrembo huyo.

Polisi walikwenda na kumkamata Jack ambapo alitupwa rumande na kufungulia jalada OB/RB/13654/07 shambulio la kudhuru mwili.
Hadi tunakwenda mitamboni, mrembo huyo alikuwa akiendelea kusota rumande.

2 comments:

Anonymous said...

Hili liwe funzo kwa warembo, wasanii na mastar wote wa Bongo wanaona ufahari kutembea na kuringa na magari wakati pa kukaa mtu huna jenga kwanza magari baadae mnaona aibu hizo zinawakuta,wenye nyumba wengine wana wivu.

Anonymous said...

Huyu Jack ameonewa kwanza ni mtoto mpole na mwenye kujiheshimu sana...