Tuesday, November 20, 2007

YOU ARE WHAT YOU EAT


SHINIKIZO LA JUU LA DAMU (High Blood Pressure):
SULUHISHO NI LISHE BORA

Baada ya wiki iliyopita kuandika makala kuhusu shinikizo la chini la damu (Low Blood Pressure), wasomaji wengine, hasa wenye tatizo hili, nao wameomba kuandikiwa makala kuhusu shinikizo la juu la damu (High Blood Pressure au Hypertension).

Kwa kuheshimu matakwa ya wasomaji wetu, tumeandika makala haya kwa lengo lile lile la kuelimisha na kuokoa maisha ya watu. Hata hivyo, kwa wasomaji wetu wa tangu kuanza kwa safu hii, makala haya ya leo yatakuwa ni marudio kwao.

Shinikizo la damu la juu (High Blood Pressure) ni ugonjwa hatari sana na unaua kimya kimya na ndiyo maana unajulikana pia kama Silent Killer. Mara nyingi dalili za ugonjwa huu zinapojitokeza hadharani, huwa tayari mgonjwa amechelewa. Kwa mujibu wa madaktari wetu, watu wengi wanakabiliwa na ugonjwa huu lakini hawajijui.

Kwa kuwa watu wengi hawajijui kama wanakabiliwa na ugonjwa hatari ambao unaweza kusitisha uhai wao wakati wowote, huendelea kuishi staili ya maisha ambayo ndiyo chanzo au huendelea kula vyakula ambavyo ndivyo vimekuwa chanzo chake, hivyo kujikuta wakiuimarisha bila wao kujijua.

Leo tunaangalia ugonjwa huu kwa upande wa staili ya maisha na ulaji wa vyakula, ambavyo ndiyo chanzo.

NINI HUSABABISHA UGONJWA HUU?
Pamoja na sababu nyingine nyingi za kitabibu, lakini kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za kisayansi, sababu kubwa za ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ni mfadhaiko (stress) utokanao na matatizo mbalimbali na staili mbovu ya kuishi.

Ulaji mbaya na wa vyakula visivyofaa kwa afya na ustawi wa binadamu ndiyo tatizo kubwa kuliko mfadhaiko. Utakuwa katika hatari zaidi kama ukiwa unaishi katika maisha yenye mfadhaiko na ulaji wako ni mbovu.

Staili mbovu ya maisha inajumuisha uvutaji wa sigara, ulaji wa kiasi kikubwa wa vyakula ambavyo huacha sumu mwilini, unywaji mkubwa wa chai, kahawa na vyakula vya kwenye makopo ambavyo vinaelezwa kuwa huzuia mfumo wa asili wa kuondoa sumu mwilini kufanyakazi yake ipasavyo.

Mfumo wa asili unapokwamishwa kufanyakazi yake ya kujisafisha, husababisha matizo mengi ya kiafya kama vile mishipa ya damu kuziba, mtu kuongezeka unene kupita kiasi, kupatwa ugonjwa wa kisukari na hatimaye shinikizo la damu (Hypertension).

Kwa upande huo wa ulaji mbovu wa vyakula, chumvi na vyakula vyenye mafuta (fats) vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu za ungonjwa huu. Kupenda kuongeza chumvi wakati unakula (table salt) ni tabia isiyofaa kiafya. Kwa kawaida, binadamu anatakiwa kula kiasi kisichozidi kijiko kimoja kidogo cha chumvi kwa siku na haitakiwi kuongeza chumvi katika chakula wakati akila.

VIJUE VIUNGO NA VYAKULA VINAVYOWEZA KUKULINDA NA UGONJWA HUU.

Kwa kuwa tumeona sababu kuu za ugonjwa wa BP ni pamoja na ulaji mbaya wa vyakula, ni vyema sasa ukavijua baadhi ya vyakula au viungo ambavyo binadamu anapaswa kula ili vimsaidie kupunguza makali ya ugonjwa huu au kujikinga nao kama bado haujakupata.
KITUNGUU SAUMU
Hiki ni kiungo muhimu sana katika chakula na kina faida kubwa sana kiafya, kinaaminika kuwa bora sana katika kushusha shinikizo la damu. Kwa mujibu wa watafiti, kitunguu saumu huondoa ile hali ya kukaza kwa mishipa midogo ya damu na hushusha mapigo ya moyo na kuyaweka katika hali yake ya kawaida pamoja na kumuondolea mgonjwa ile hali ya kuona kizunguzungu na kupumua kwa shida. Unaweza kuvila vitunguu saumu vibichi, punje mbili mpaka tatu kwa siku.

LIMAU
Limau ni tunda jamii ya machungwa, lakini lenyewe ladha yake ni kali na ya uchachu. Faida zake kiafya ni kubwa, siyo tunda la kupuuziwa na wagonjwa wa shinikizo la damu au kama unataka kujikinga na ugonjwa huo. Limau lina kiasi kikubwa cha vitamini K ambayo ni muhimu sana katika kuzuia mishipa midogo ya damu isidhoofike na kushindwa kusukuma dama ipasavyo.

Itaendelea wiki ijayo.

No comments: