Tuesday, November 27, 2007

YOU ARE WHAT YOU EAT!


Shinikizo la juu la damu (High Blood Pressure): Suluhisho nil lishe bora-2
Wiki iliyopita tulianza kuelezea tatizo la shinikizo la juu la damu na jinsi ya kukabiliana nalo kwa kutumia chakula na matunda, leo tunamalizia kuangalia orodha ya vyakula na matunda hayo:

ZABIBU NA TIKITIMAJI
Tunda aina ya Zabibu ni maarufu sana mkoani Dodoma. Kama ulikuwa hujui faida na umuhimu wa tunda hili, basi ilewa kwamba lina kiasi kikubwa cha vitamini P ambayo hufanyakazi ya kuimarisha mishipa ya damu mwilini. Mbali ya Zabibu, Tikitimaji nalo ni tunda moja muhimu sana kwa wagonjwa wa shinikizo la damu au watu wanaopenda kujikinga.

Mbegu za Tikitimaji zinaaminika kuwa na uwezo wa kuyeyusha mishipa ya damu iliyoganda na matokeo yake kushusha shinikizo la juu la damu. Unachotakiwa kufanya ili kutumia mbegu za tunda hili kama dawa, chukua mbegu zake, zikaushe kisha zikaange halafu kula kama karanga kila mara.

WALI NA VIAZI VITAMU
Wali ni chakula kingine kizuri kwa mgonjwa wa shinikizo la damu, hasa wali uliopikwa kwa ule mchele wa rangi ya kahawia (brown rice) ambao unaaminika kuwa na kiwango kidogo sana cha mafuta, chumvi na Cholestrol. Aidha mchele wa kahawia una kiwango kikubwa cha madini aina ya Calcium ambayo hutuliza mishipa ya fahamu na kuondoa dalili za ugonjwa.

Mbali na mchele, viazi vitamu, hasa vilivyopikwa na maganda yake, vinaaminika kusaidia sana ushushaji wa shinikizo la damu. Inaaminika kwamba, viazi vitamu vinapopikwa na maganda yake, hunyonya kiasi kidogo sana cha chumvi ambayo mgonjwa hatakiwa kuitumia sana. Viazi vitamu vina kiasi kikubwa cha madini aina ya Potassium na hakina chumvi. Kiwango cha Magnessium kilichomo kwenye viazi, kinasaidia sana ushushaji wa shinikizo la damu.

JUISI YA MATUNDA
Juisi ya matunda halisi, hasa karoti na spinachi, inapotumiwa kwa pamoja au moja moja, huweza kutibu au kuzuia shinikizo la damu. Tengeneza kiasi cha nusu lita ya juisi hiyo mchanganyiko na kunywa kila siku mara moja au glasi mbili kila siku za jusi moja kati ya hizo mbili ili kujitibia au kujikinga na ‘Pressure’.

Kwa kifupi, mgonjwa wa shinikizo la damu, anapswa sana kuzingatia ulaji sahihi wa vyakula (Balanced Diet) kwa kupenda kula vyakula vyote ambavyo husaidia kumpa ahueni kama tulivyoainisha hapo juu baadhi yake. Pia ajiepushe kabisa na vyakula ambavyo huchangia hali yake kuwa mbaya. Kitu kingine muhimu ni kubadili mtindo wa maisha, fanya mazoezi na kupata muda wa kupumzika na kulala usingizi mzuri angalau saa nane kwa siku.

NYAMA NYEKUNDU NA MAYAI
Kama kuna chakula ambacho mgonjwa wa shinikizo la damu anapaswa kukiona kama sumu, basi ni nyama nyekundu (nyama ya ng’ombe, mbuzi, nguruwe, n.k) na mayai. Iwe mwiko kwa mgonjwa huyu kula vyakula hivyo, kwani vinapoliwa moja kwa moja hupandisha shinikizo la damu.

Hivyo kama wewe ni mgonjwa wa ‘pressure’ na unaendelea kula vyakula hivyo, basi ujue kamwe hutapona na unajiharakishia safari ya kifo. Nyama iliyo salama kwa mgonjwa huyu ni ya samaki na kuku aliyeondolewa ngozi.

No comments: