Friday, January 25, 2008

IJUMAA SHOWBIZ!!

The Ijumaa sexiest Girl anyakua zawadi zake

Hatimaye mshindi wa shindano la kumtafuta msichana mwenye mvuto wa gazeti hili, ‘The Ijumaa Sexiest Girl’, Jokate Mwegelo (PICHANI JUU) amepata zawadi zake, yaani cheki ya shilingi laki tano na mavazi yenye thamani ya pesa hiyo kutoka ndani ya duka la Zizzou Fashion lililopo maeneo ya Victoria jijini Dar es Salaam, Hamida Hassan alishuhudia zoezi hilo.

Akipiga stori na safu hii ambayo ndiyo ilikuwa ikiendesha shindano hilo, lililomalizika mwishoni mwa mwaka jana, staa huyo wa urembo nchini alisema kwamba amefurahishwa sana na zawadi hizo kwani hakutarajia kama angezipata wakati shindano hilo lilipoanzishwa.

“Kweli nimefurahishwa na zawadi hii kubwa, sikuitarajia, wakati shindano linaanzishwa nilidhani ni mchezo tu lakini leo nimefanikisha kupata zawadi hii kubwa,” alisema mrembo huyo.

Jokate aliibuka na ushindi huo baada ya kuwabwaga warembo kumi na moja waliokuwa katika shindano hilo ambao ni Aisha Madinda, Lisa Jensen, Brandina Chagula ‘Johari’ Flaviana Matata, Nancy Sumary, Jacqueline Ntuyabaliwe ‘K-Lyin’ Irine Uwoya, Besta Prospar, Rashida Wanjara, Rehema Chalamila ‘Ray C’ na Nancy Sumari.

Naye mratibu wa shindano hilo, Hamida Hassan aliiambia safu hii kwamba, anashukuru shindano hilo kumalizika kwa kupatikana mshindi anayekubalika na wengi, kwani lilikuwa na ushindani mkubwa ukizingatia kwamba warembo wote walioshiriki walikuwa wakali.

“Nashukuru mpambano huo umeisha kwa kupatikana mshindi anayekubalika na wengi, kwani ushindani ulikuwa mkumbwa kwasababu warembo wote walikuwa na mvuto unaokaribiana. Pia nawashukuru wasomaji kwa ushirikiano waliouonesha mpaka kupatikana kwa mshindi huyo,” alisema Hamida.

Soggy asikitika kuzushiwa

Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Anselem Ngaiza a.k.a Soggy Dog, ameiambia ShoWbiz kwamba anasikitishwa na baadhi ya watu wanaomzushia kuwa amekamatwa na vitu ambavyo vinadaiwa kuwa vya wizi katika Jiji la Arusha, Frank Kadende alicheki naye.

Akipiga stori kwa njia ya simu kutoka mkoani humo alikopiga kambi hivi sasa, msanii huyo alitamka kwamba, ameshangaa kupigiwa simu na rafiki zake wa karibu wanaoishi sehemu mbalimbali nchini wakimpa pole kwa kukamatwa na vitu kama TV aina ya Sony na mashine ya kufulia nguo aina ya Lg.

“Naomba watu waelewe kwamba huo ni uzushi tu, ambao unasambazwa na washikaji wanaotaka kuniharibia jina, mimi sijatupwa selo katika kituo cha Unga Limited, wala sijanunua vitu hivyo, pia sijakamatwa na bangi kama wanavyozusha. Wanataka kunivunjia heshima kitu ambacho pia kilimshitua mama yangu ambaye alinipigia simu akaniuliza kama ishu hizo zina ukweli wowote,” alisema msanii huyo.

Jamaa amewataka mashabiki wake waelewe kwamba taarifa hizo siyo sahihi kabisa, kwani hivi sasa yupo bize akitayarisha albamu yake mpya ambayo itakuwa mtaani hivi karibuni.
Mr. Ebbo: Matusi ya nini washikaji?

Kutoka Mkoani Tanga, msanii Abel Motika ‘Mr. Ebbo’ ameuanza mwaka huu kwa kuwapa live baadhi ya wasanii wenzie wanaoitumia sanaa ya Bongo Flava kwa kuandika mashairi yenye matusi kwamba hata wasipotukana wanaweza kutoka, Fatma Amri alisema naye.

Akipiga stori na ShowBiz, kwa njia ya simu kutoka Mkoani Tanga, mchizi ambaye anatumia staili ya kabila la Kimasai alisema kuwa, mwaka huu anafungua ukurasa mpya kwa kuwahamasisha wasanii wenzie wafanye muziki safi, badala ya kuingiza matusi katika nyimbo zao.

“Nataka waone mfano kwenye albamu mpya ambayo itakuwa na jina la ‘Muziki safi’ ambayo zaidi itawahamasisha wasanii wafanye kazi safi kama hizo. “Mimi siamini, yaani wasanii waimbe nyimbo za matusi au wawatumie kina dada wanaocheza nusu uchi kwenye video zao ndio watoke au wauze sana!” alisema Ebbo.

Ebbo alisema kwamba, msanii unatakiwa uwe mbunifu ili uendelee kuwa juu na kupendwa na mashabiki wako. Albamu yake hiyo itakuwa na nyimbo kumi na mbili, zote zikiwa zimetengenezwa katika studio yake ya Motika Record iliyopo Tanga.


No comments: