Tuesday, July 15, 2008

ZAA MTOTO MZURI KWA KUFUATA ULAJI SAHIHI

You are what you eat
Kwa kawaida mama anaposhika uja uzito, mume, ndugu wa familia na mja mzito mwenyewe hutarajia kuzaa mtoto mwenye afya njema na aliyekamilika viungo vyote, lakini si mara zote hali huwa kama ilivyotarajiwa.

Wakati mwingine, mimba huharibika kabla ya kiumbe kukua na hivyo kutoka, ama mtoto huweza kufa akiwa angali tumboni au muda mfupi kabla au baada ya kujifungua. Hali hii huweza kumkuta mama mja mzito kutokana na sababu kadhaa.

Kwa mujubu wa wataalamu wetu wa afya ya uzazi, mama anaweza kupoteza mtoto katika mazingira yaliyotajwa hapo juu ama kutokana na ukosefu wa lishe bora, sababu za kurithi au matatizo ya kiafya aliyonayo mzazi. Vile vile hali hiyo huweza kusababishwa na uvutaji wa sigara, unywaji pombe au maambukizi mengine ya ugonjwa.

Tatizo hili ni kubwa duniani kwa sasa lakini ni rahisi kwa mama mja mzito kujitambua iwapo mtoto anaendelea vizuri tumboni ama ameshakufa, iwapo atakuwa akihudhuria kliniki na kuchunguzwa kwa karibu maendeleo ya mtoto tumboni ambako huwa kuna pilikapilika za hapa na pale kuashiria kuwa kiumbe kingali hai.

Wanawake wanaopatwa na matatizo ya kufiwa na viumbe vyao tumboni, huwa wanaumia sana kisaikolojia na hivyo mume hushauriwa kumfariji mke wa namna hii pamoja na ndugu na jmaa kwa ujumla ili kumuepusha na kupatwa na mfadhaiko wa akili ambao baadae unaweza kumuathiri zaidi kiakili na kiafya.

Tukirudi katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mama kuepuka kupatwa na matatizo kama hayo, madaktari wetu wanasema kuwa suala la mama mja mzito kula lishe bora na mlo kamili ni lazima kwa usalama wa mama na mtoto aliye tumboni.

Mlo kamili anaopaswa mama mja mzito kula, lazima uwe na vitamini na madini yote muhimu ambayo ni muhimu sana kwa ukuaji wa mtoto tumboni na uimarishaji wa afya ya mama na kumuepusha na matatizo mengine ya kiafya yanayoenda pamoja na uja uzito.

Wakati wa ujauzito, mlo unaoshauriwa kuliwa zaidi ni ule wenye madini ya kalisi (calcium), ‘foliki asidi’, protini na Vitamini B12. kiasi cha miligramu 1200 za madini ya kalisi zinapaswa kuliwa na mama mja mzito kwa siku. Vyakula vyenye kiwango kikubwa cha kalisi ni pamoja na mtindi, jibini, maziwa yasiyo na mafuta (skim milk), maharage, n.k.

Vyakula vyenye kiwango kikubwa cha madini ya ‘foliki asidi’ ni pamoja na karanga, siagi ya karanga (peanut butter), maharage makavu, mahindi na mboga za kijani cheusi na kiwango kinachohitajika mwilini cha madini haya ni miligramu 400 kwa siku.

Kwa upande wa protini, vyakula vyenye kiasi kikubwa cha virutubisho hivyo ni pamoja na supu ya njegere, mbaazi, kunde na maharage. Kiasi utakachotakiwa kula kitabadilika kutokana na umri wa uja uzito, lakini kimsingi ni chakula kinachopaswa kuliwa angalau gramu 10 kwa siku.

Katika kipindi chote cha uja uzito, mama anatakiwa kuhakikisha anazingatia suala la kula lishe bora ili kuhakisha ubongo wa mtoto, mifupa na viungo vingine muhimu vinakuwa vizuri. Ni vizuri kwa mama mja mzito kula kidogo kidogo kila mara kwa ratiba maalum na wala asiruke ratiba hiyo. Anywe maji mengi, angalau glasi nane kwa siku na jambo hili ni la lazima.

Mwisho, mama mja mzito siyo tu anashauriwa kula mlo kamili (balanced diet) bali pia kuacha kabisa uvutaji sigara, unywaji pombe na vinywaji vyenye ‘caffeine’, kama vile chai, soda, n.k.

No comments: