Wednesday, November 19, 2008

Mambo 7 muhimu kuzingatia kwa afya yako!


Suala la kuwa na afya bora linahitaji ujuzi wa mambo mengi, kwani unaweza kuwa unakula vizuri lakini ukawa bado hujaona mafanikio mazuri katika afya yako. Inawezekana kuna baadhi ya mambo hujayafanya kama inavyotakiwa.

USINGIZI
Utafiti unaonesha kuwa iwapo mtu atalala kwa saa chache za usingizi, kati ya saa 4 – 7 kwa kipindi kifupi tu cha siku 6, kiwango chake cha sukari kitapanda. Kwa kawaida, kila mtu anapaswa kulala kwa saa zisisopungua 8 kwa siku na inashauriwa mtu kulala kabla ya saa 6 usiku.

VYAKULA
Epuka kula vyakula vya kukaanga na vile vya kwenye makopo au paketi na vilivyoondolewa uhalisi wake, badala yake pendelea kula vyakula vya asili kadri uwezavyo. Pia ni lazima kula matunda na mboga za kutosha.

Unapokula chakula, acha tabia ya kula kwa pupa na kumeza chakula bila kutafuna. Kula taratibu na tafuna chakula vya kutosha kabla ya kukimeza. Utafunaji chakula hurahisisha usagaji wake tumboni.

VINYWAJI
Maji ni muhimu kwa mambo mengi mwilini, kama vile kusaidia usagaji chakula tumboni, kuondoa sumu mwilini na usafirishaji wa virutubisho muhimu kwenda kwenye chembechembe hai za mwili. Usipende kunywa vinywaji vyenye sukari, kama soda na vingine, kwani huongeza unene.

MATAYARISHO
Kutayarisha chakula chako mwenyewe inaweza kuwa kazi kubwa, lakini ni vizuri au muhimu kupenda kula chakula ulichokiandaa mwenyewe au kilichoandaliwa nyumbani kwako, kuliko kupendelea kula migahawani, hotelini au kwa wauza vyakula wengine.

PUMZI
Kama kuna kitu kingine ambacho ni muhimu katika mwili wa binadamu, basi ni pumzi. Kuwa na tabia ya kuvuta ‘pumzi ndefu’ kwa dakika kadhaa kila siku asubuhi, mchana na jioni. Vuta pumzi ndefu kwa kutumia pua, jizuie kwa sekunde kadhaa kisha shusha kwa kutumia mdomo. Zoezi hili ni muhimu kwani husaidia kuondoa sumu na kusafisha mapafu.

WAKATI
Kula kwa wakati mlo wako na usipende kuacha kufungua kinywa asubuhi, inaelezwa kwamba watu wanaopenda kuacha kufungua kinywa asubuhi, wana hatari ya kupatwa na unene.

MAZOEZI
Jambo la mwisho na muhimu ni mazoezi. Fanya mazoezi ya aina yoyote ili kuuweka mwili wako katika hali nzuri. Mazoezi ni moja ya vitu muhimu baada ya lishe bora na kupumzika. Kumbuka kwamba afya bora ni sawa na kitanda, kinahitaji kutandikwa kila siku kabla ya kukilalia.

No comments: