Kama ilivyo ada, chakula hutoa majibu ya maswali mengi yanayotukabili katika ustawi wa afya zetu kila siku. Chakula pia kikitumiwa ipasavyo, huwa dawa kwa kila aina ya ugonjwa, kama ambavyo tumeshaona katika makala zetu nyingi zilizopita.
Katika makala ya leo, tunaangalia baadhi ya vyakula ambavyo vimetajwa kama tiba au ufumbuzi wa tatizo fulani, iwe kwa muda mfupi ama kwa muda mrefu. Kwa mujibu wa habari iliyotolewa mapema mwezi huu na mtandao wa ‘Men’s Health’, kuna vyakula vikiliwa huongeza ufanisi wa ubongo!
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na jarida moja la saikolojia nchini Uingereza, ingawa ubongo unawakilisha asilimia mbili tu ya uzito wa mwili wa binadamu, lakini unawakilisha asilimia 20 ya utowaji wa mahitaji ya nishati mwilini, hivyo ukiupatia chakula sahihi, unaweza kuwa na nguvu ya kufanya kazi na kufikia hata kiwango cha asilimia 200, bila kujali kama una umri wa mika 15 au 40!
KAHAWA
Ingawa kahawa si miongoni mwa vinywaji bora vyenye faida kubwa mwilini, lakini ikitumika kwa kiasi ina faida moja kubwa ya kuchangamsha ubongo na kuamsha kumbukumbu kwa muda mfupi. Katika utafiti mmoja uliofanywa nchini Uingereza, ulionesha kuwa kikombe kimoja cha kahawa husaidia kuchangamsha kumbukumbuka na mbinu za kutatua matatizo, ndiyo maana watu wengi hupenda kutumia kahawa kwa sababu hii.
Lakini tahadhari inatolewa kwamba unywaji wa kahawa usiwe mkubwa. Katika jitihada za kuchangamsha ubongo, ikiwa ni kimbilio la muda mfupi, hutakiwi kunywa zaidi ya kikombe kimoja kwa siku, vinginevyo utajitakia matatizo mengine ya afya.
MATUNDA
Kahawa itakusaidia kuchangamsha ubongo wako kwa muda mfupi, lakini suluhisho la muda mrefu na la kudumu katika kuufanya ubongo ufanye kazi yake sawasawa ni kula matunda ya aina mbalimbali, hasa bluberi (blueberry) ambayo yameonesha ufanisi mkubwa katika ubongo wa binadamu.
SAMAKI NA DAGAA
Samaki na dagaa wameorodheshwa katika kundi la vyakula vinavyomuongezea mlaji uwezo mkubwa wa kufikiri mambo kwa haraka, kiwango chake cha kuongeza uwezo wa kufikiri ni kikubwa sana.
Kwenye samaki hao kuna virutubisho aina ya ‘Omega -3’ na ‘Niacin’ ambavyo vinaaminika kuwa msingi wa ujenzi wa tishu za ubongo wa mwanadamu, hivyo kwa kula kwa wingi mara kwa mara, utaimarisha uwezo wako wa kufikiri.
MTINDI AU KARANGA MCHANGAYIKO
Ili kupunguza wasiwasi katika mazingira tofauti, pendelea kunywa mtindi usio na mafuta (low fat- yogurt) au pendelea kula karanga na korosho. Wana sayansi wa nchini Slovakia waliwafanyia utafiti wa kuzungumza wanafunzi kadhaa kwa kuwapa virutubisho maalum vinavyopatikana kwenye mtindi na karanga na matokeo yalionesha kuwa waliweza kutoa hotuba bila ‘presha’ tofauti na wale waliotoa bila kutumia virutubisho hivyo.
Wakati mtindi una sifika kwa kumfanya mnywaji kuwa mtulivu wa akili, unywaji wa soda kwa wingi (kiasi cha chupa mbili na nusu) kwa siku, kunamfanya mtu kuzubaa na wakati mwingine kupatwa na mfadhaiko wa akili, hii ni kwa mujibu wa jarida moja la Marekani linalotoa machapisho kuhusu masuala ya afya za watu (American Journal of Public Health). Hivyo mnaopenda kunywa soda kwa wingi kwa siku, jueni mna uchosha mwili.
MBOGA
Tabasamu au hasira huwa haiji tu hivihivi, bali wakati mwingine huchangiwa na homoni mwilini. Ulaji wa mboga za kijani pamoja na kabichi, utafiti unaonesha kuwa hutoa kiasi kikibuwa cha Vitamini B6 ambazo ni muhimu kwa uzalishaji wa homoni zinazomfanya mtu ajisikie vizuri na kuwa na tabasamu wakati wote (feel-good hormones). Utafiti unaonesha kuwa ukosefu wa Vitamin B6 mwilini, kunaweza kumsababishia mtu wasiwasi, hasira na hata mfadhaiko wa akili.
No comments:
Post a Comment